Mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Maweni, Kata ya Terati Jijini Arusha Rashid Ismail (11), amefariki dunia baada ya kung'atwa mkono na nyoka aina ya Cobra alipokuwa amelala kwenye kitanda kimoja na wenzake watatu pamoja na wazazi wake wawili Jijini humo.
Inaelezwa kuwa usiku wa saa sita Rashid alishtuka usingizini na alisikika akisema ameng'atwa na kitu asichokijua akionyesha mkono wake sehemu alipong'atwa, baada ya muda ulimi wake ulianza kuwa mzito na kuanza kubadirika rangi na kuwa mweusi huku akiomba maji, na alipopewa maji alianza kutapika matapishi yaliyoambatana na mapovu, mwili nao ulionekana kukosa nguvu kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda.
Familia ikiwa katika mshangao usiku huo ililazimika, kupiga kelele za kuomba msaada na watu walijitokeza na kuamua kumpeleka Rashid katika Hosptali ya Murieti iliyopo Jijini humo kwa ajili ya kuchunguzwa na walipofika Hosptalini hapo Rashid alikuwa tayari ameshapoteza maisha, baada ya mwili wa Rashid kufanyiwa vipimo usiku huo familia iliambiwa kifo chake kimetokana na kung'atwa na nyoka.
Familia hiyo waliporudi nyumbani kumtafuta nyoka huyo walimkuta amejiviringisha kwenye blangeti walilokuwa wamejifunika.
0 Comments