Ticker

7/recent/ticker-posts

JE, UNAMJUA MWENYE JINA LA BARABARA YA SHEKILANGO? MZEE WA ATI KALI ANAMTAJA

Hayati Hussein Shekilango

LEO NI MIAKA 43 TOKA MHE. HUSSEIN SHEKILANGO AFARIKI KWA AJALI YA NDEGE: BARABARA YA _"SINZA KWA WAJANJA"_ IMEBATIZWA JINA LAKE

Mzee wa Atikali

0754 744 557 

Alhamis, Mei 11, 2023

1. Usuli

"Shekilango Road"_ ni moja ya barabara maarufu sana hapa _Bandari Salama_. Barabara hii inaanzia maungio ya _"Morogoro road"_  karibu kabisa na nyumba za NHC hadi maungio ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kituo cha Bamaga. Barabara hii ina urefu wa kilometa 3.7, upana wa mita 22, njia 4 za magari, njia za watembea kwa miguu, taa za kileo, mitaro ya maji na bustani ya kisasa iliyo katikati ya barabara.

Hata hivyo,  baadhi ya _"Bongolanderz"_, hususan _Dot.com_ & _Diaspora_,  hawana uelewa wowote kuhusu jina hili _"Shekilango"_. _"Atikali"_ hii itaondoa ombwe hilo kwa kuhabarisha kinagaubaga.

2. _"Shekilango Road"_ imetokana na nini?


"Shekilango Road"_ imetokana na jina la marehemu Mhe. HUSSEIN RAMADHANI SHEKILANGO. Huyu alikuwa Waziri na Mbunge wa Korogwe,Tanga. Mhe. SHEKILANGO aliupata ubunge baada ya kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili,  Oktoba 26, 1975 ambapo _alimohola_ kura 34, 845 huku mpinzani wake, ATHUMANI MHINA, _akiduchua_ kwa kura 14, 224. Novemba 9, 1975, Rais JULIUS NYERERE alimteua Mhe. SHEKILANGO kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Utawala) akiwa chini ya Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu, Mhe. RASHID MFAUME KAWAWA. 

Mwaka 1977, yalifanyika mabadiliko makubwa kwenye Baraza la Mawaziri ambapo aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. EDWARD MORINGE SOKOINE, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Mhe. KAWAWA. Mhe. SHIKILANGO akabakizwa kwenye nafasi yake lakini chini ya uongozi wa Mhe. SOKOINE. 

Mhe SHEKILANGO, kabla ya ubunge, alikuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Usagaji la Taifa lililoanzishwa mwaka 1968 na Sheria ya _"The National Milling Corporation Act, 1968"_. Mhe. SHEKILANGO alikuwa amefanya kazi nzuri kama Meneja Mkuu wa shirika hili hivyo alipogimbea na kushinda ubunge, Rais NYERERE akaamua kumteua kuwa Waziri.


3. Mh. Shekilango & Mhe. Sokoine

Mhe SOKOINE alikuwa ni mwanamume wa shoka. Alikuwa ni mchapakazi hodari ambaye alikuwa hapendi _bla bla_ na akifanya kazi hadi usiku wa manani. Sifa hizi pia alikuwa nazo Mhe SHEKILANGO na hivyo wakapelekea ofisi ya Waziri Mkuu ing'are vilivyo.

4. Vita ya Kagera Yarindima

Mwishoni mwa mwezi Novemba 1978, Majeshi ya Uganda yalivamia nchi yetu bila sababu yoyote ya msingi na hivyo vita baina ya nchi hizi mbili ikarindima baada ya njia za kulitatua tatizo hili kidiplomasia kushindikana. Mhe. SOKOINE na Mhe. SHEKILANGO walikuwa ni miongoni mwa viongozi walioshiriki kikamilifu katika ufuatiliaji na utekelezaji wa kila kilichokuwa kikihitajika kwenye vita hiyo. Viongozi hawa walikuwa chini ya uongozi madhubuti wa Jemedari Mkuu na Baba wa Taifa, Mwalimu JULIUS NYERERE. Hatimaye, wanajeshi wetu shupavu walishinda vita hiyo na kupelekea nduli IDD AMIN, aliyekuwa Rais wa Uganda baada ya kumpindua Rais MILTON OBOTE aliyekuwa nchini Singapore akihudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola Januari 25, 1971, kuikimbia nchi yake kwa aibu na fedheha kubwa.

5. Mhe. Shekilango Apewa Kazi Maalum

Baada ya kumalizika vita ya Kagera mwaka 1979, Rais NYERERE alimpa Mhe. SHEKILANGO jukumu maalum la kuwa mratibu kati ya serikali ya Uganda na Tanzania.

Kupewa jukumu hili ilikuwa ni heshma kubwa kwa Mhe. SHEKILANGO kwa kuwa  alikuwa ameaminiwa na Rais NYERERE na kwa hakika lilikuwa ni jukumu zito kwani hali ya amani nchini Uganda kipindi hicho ilikuwa tete.

Ikumbukwe kuwa baada ya vita hiyo, Aprili 12, 1979,  Prof. YUSUPH KIRONDWE LULE alisimikwa kuwa Rais wa Uganda. Siku hiyo alitoa hotuba kwa Kiingereza akiahidi amani na usalama kwenye Taifa hilo. Hata hivyo, alipokuwa akimalizia hotuba hiyo _alichomekea_ kwa lugha ya kwa _"Luganda"_ maneno yamaanishayo _"It's our turn"_. Prof. LULE alikuwa amedhamiria kuwaneemesha watu wa kabila lake!. _"Waliosomea Quba"_ wakajua hatadumu kwenye nafasi hiyo kutokana na mawazo hayo mufilisi. Na kweli, mnamo Juni 20, 1979, Prof. LULE aling'olewa madarakani baada ya kutofautiana na Baraza la Ushauri la Taifa la nchi hiyo juu ya uteuzi wa nafasi za Mawaziri. GODFREY LUKONGWA BINAISA ndiye aliyechukua nafasi yake. Licha ya utawala huu mpya, machafuko yaliendekea kutaradadi nchini humo ambako baadhi ya vikosi vya majeshi yetu bado vilikuweko.


Hivyo, Mwalimu NYERERE akamteua Mhe. SHEKILANGO chini ya usaidizi wa Mhe. Balozi FARAJI ALI KILUMANGA (Mzazi wa Balozi CHABAKA FARAJI KILUMANGA), aliyekuwa balozi wetu nchini Uganda, kuisaidia serikali ya Uganda isimame. Kazi hii waliifanya kuanzia Juni 1979.

6. Mhe. Shikilango Apanga Kukutana na Rais Nyerere  Arusha

Siku ya Jumapili, Mei 11, 1980, Mhe. SHEKILANGO alikuwa na miadi ya kukutana na Rais NYERERE Arusha kwavile Rais NYERERE alikuwa kwenye ziara ya kiserikali mkoani humo.

Mhe. SHEKILANGO alikuwa akienda kumtaarifu Baba wa Taifa juu ya hali ya usalama ya Uganda baada ya mfarakano kati ya Rais BINAISA na General DAVID OYITE OJOK aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Uganda, mfarakano ulioonesha dalili zote za kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais BINAISA aliamua kumuondoa Bw. OJOK kwa kumteua kuwa Balozi wa Uganda nchini Algeria kwani nidhamu ya jeshi ilikuwa imeporomoka sana huku kukiwa na vitendo lukuki vya uporaji na ubakaji.

Bw. OJOK aligomea uteuzi huo na wanajeshi waliokuwa watiifu kwake wakatangaza kumng'oa madarakani Rais BINAISA aliyekuwa akilindwa na majeshi ya Tanzania kwenye hekalu la Rais Entebbe. Wanajeshi hao walikuwa wamekiteka kituo cha redio cha nchi hiyo na walikuwa wakisimamisha magari yote na kuyapekua kuona kama yalibeba silaha. 


7. Mhe. Shekilango Akwea _"Pipa"_ kwenda _"Geneva ya Afrika"_

Asubuhi na mapema siku hiyo ya Jumapili, Mei 11, 1980, Mhe. SHEKILANGO aliongoza msafara wa _"Bongolanderz"_ uliokuwa ukitoka Uganda kuelekea Arusha kwa ndege ndogo aina ya Casena 402 yenye uwezo wa kuchukua watu 8.

_"Bongolanderz"_ waliokuwemo kwenye msafara huo walikuwa 7:

1. Mh. Waziri HUSSEIN SHEKILANGO

2. Balozi FARAJI KILUMANGA

3. Mwanadiplomasia IDD MSECHU

4. Luteni PETER MALLYA

5. Luteni LUOGA 

6. Cpl. PETRO MAGUNDA 

7. Pte STEPHEN MTAWA

8. Ndege Yapata Ajali, Mhe. Shekilango na Msafara wake _"Kende Malamu"_

Asubuhi hiyo, Mwalimu NYERERE alienda kanisani kisha akawa anasubiri kuhabarishwa na Mh. SHEKILANGO kuhusu hali ilivyo nchini Uganda. Hata hivyo, alishangaa kuona muda wa miadi ukiwa umepita sana bila ya Mhe. SHEKILANGO kufika ili kuonana naye.

Hatimaye, alasiri, Mwalimu NYERERE aliletewa habari za kuhuzunisha na kusikitisha sana na hakuamini masikio yake alipoelezwa kwamba ndege hiyo ndogo iliyokuwa imembeba Mh. SHEKILANGO na msafara wake ilianguka wakati tayari ilikuwa imeishaingia anga ya mkoani Arusha na kwamba abiria wote walikuwa _kende malamu_!. Hakukuwa na hata abiria mmoja aliyepona.

Ndege hiyo ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) iliyokuwa ikiruka kati ya mita 5000 na 7000 kutoka usawa wa bahari ikielekea KIA ilipata ajali na kuanguka kati ya saa 4 na 5 asubuhi katika kijiji cha Engwiki wilaya ya Monduli, Arusha.

Vijana wawili kutoka kijiji cha Engwiki, Bw. MUNDEREI ANGERUKAI na Bw. NUSERIEKI NJONJOLOI ndio waliokuwa mashuhuda wa kwanza wa ajali hiyo waliosaidia kupatikana kwa ndege hiyo iliyolipuka baada ya kugonga kilima cha Kolomoniki kutokana na ukungu mkubwa uliokuwa umetamalaki eneo hilo. Askari wa Chuo cha Kijeshi cha Monduli walitumia masaa 5 kuitafuta ndege hiyo. Vijana hao 2 hatimaye waliweza kuiona ndege hiyo na kuwaonesha askari hao jioni hiyo ya huzuni hivyo miili yao iliyoharibika vibaya ikachukuliwa. Ni moja ya matukio yaliyomuhuzinisha sana Baba wa Taifa.

9. Mhe Shekilango Azikwa Kishujaa

Mhe SHEKILANGO, aliyekuwa Kipenzi cha wana- Korogwe, alizikwa Jitengeni, Mombo, Korogwe, Tanga. Mazishi hayo yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu ulioweka rekodi ya aina yake wilayani Korogwe. Katika kumuenzi, shule moja huko Mombo ikapewa jina lake _"Shekilango Secondary school"_. Aidha, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam kuna shule ya msingi iliyopewa jina lake pia _"Shekilango primary school"_. Shule hii ilianzishwa mwaka 2002 baada ya serikali kuamua kuigawanya shule ya msingi Mapambano na kuwa shule mbili; _Mapambano Primary School_ na _Shekilango Primary School_.

10. *Barabara ya _"Sinza kwa Wajanja"_ yapewa jina la Shekilango*

Kwakuwa wakati huo ajali hiyo ya kuhuzunisha ilipotokea ujenzi wa barabara ya Sinza ndio ulikuwa umeanza, uongozi wa jiji la Dar es Salaam ukaamua kumuenzi marehemu SHEKILANGO kwa kuipa barabara hiyo jina lake.

11. Mhe Shekilango Aacha Mjane _Ngangali_

Marehemu SHEKILANGO aliacha mke, Mwalimu ZIPPORA @ _"Mama Sheki"_, _"Dada Zippy"_. Marehemu SHEKILANGO na familia yake walikuwa wakiishi Sea view, Upanga jirani kabisa na walipokuwa wakiishi wazazi wa _"Mzee wa Atikali"_. Baadaye, familia hii ya SHEKILANGO ilihamia kwenye nyumba yao iliyoko Kinondoni Bwawani kiwanja Na. 401 Kitalu Na. 42.

Marehemu SHEKILANGO alikuwa _amepanda hewani_ na watoto wake pia walikuwa na wajihi kama wake. Urefu usio wa kawaida wa watoto wa marehemu SHEKILANGO uliwatambulisha popote walipokwenda. Wanae hao ni MUSA, SULEIMAN & SALAMA. Na pia MAMBIU SYLVIA TUMPALE.

Mama ZIPPORA, aliyezaliwa mwaka 1938, alikuwa Mwalimu hodari aliyefundisha shule nyingi za sekondari nchini. Ni mwalimu aliyekuwa na heshima kama Mwalimu NOMBO ambaye alikuwa rafiki yake mkubwa. Mama ZIPPORA alikuwa _"Headmistress"_ shule nyingi za wasichana ie Zanaki, Kisutu, Forodhani, Jangwani, Msalato na  Iringa _Girls_. Baadaye alikuwa Ofisa elimu wa jiji na kisha akawa wizara ya elimu kitengo cha sekondari.

Mama ZIPPORA alifariki Septemba 1, 2018 na kuzikwa Jumamosi Septemba 8, 2018 huko Mombo, Tanga.

12. Tamati:

Leo, Alhamis mujarab, Mei 11, 2023, nchi yetu imetimiza miaka 43 toka _"MWAMBA"_ huyu, HUSSEIN RAMADHANI SHEKILANGO aage dunia. _"Mzee wa Atikali"_, kwa mwaka wa nne sasa, amekuwa akiwaibua mashujaa hawa waliolifanyia makubwa Taifa hili lakini ama hawajulikani au wamesahaulika. _"Atikali"_ hii ya leo ni muendelezo wa jitihada hizo.

12.1. Tafakuri Jadidi

12.1.1 Je, ni kwanini kuna _"Bongolanderz"_ wengi waliolifanyia mengi Taifa hili lakini wanakuwa hawajulikani au husaulika mara tu waki- _kende malamu_?

10.1.2 Je, wana-Korogwe wa sasa wanamjua Mhe. SHEKILANGO? Je, huwa wanamkumbuka vipi hata tu siku yake aliyofariki?

Mzee wa Atikali 

0754 744 557

Post a Comment

0 Comments