Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dr. Stergomena Tax amesema Diaspora wa Tanzania wamekuwa na mchango mkubwa katika Taifa ambao unajionesha kwenye takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambazo zinaonesha kuanzia January hadi December 2021, Diaspora wenye asili ya Tanzania walikuwa wametuma fedha nchini zaidi ya USD milioni 569.3 na kwa mwezi January hadi December 2022 jumla ya fedha zilizotumwa na Diaspora nchini kupitia vyanzo rasmi (Miamala ya Makampuni ya Simu na Benki), ni USD bilioni 1.1, ambazo ni sawa na Tsh. Trilioni 2.6.
Dkt. Tax amesema hayo leo wakati akizindua mfumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali ambao utazisaidia Balozi za Tanzania kwenye Mataifa mbalimbali kuachana na utaratibu wa sasa wa kuwasajili Diaspora kwa kutumia Vitabu Ubalozini, na kuwawezesha kujisajili kimtandao.
“Vilevile katika mwaka 2022, Uwekezaji uliofanywa na Diaspora wenye asili ya Tanzania kwa ununuzi wa nyumba, na viwanja hapa nchini, ulikuwa ni Shilingi Bilioni 4.4. Uwekezaji huu ni nyongeza maradufu kutoka kiasi cha Shilingi Bilioni 2.3 walizowekeza Diaspora katika Nyumba na Viwanja mwaka 2021”
“Zaidi ya uwekezaji katika nyumba na viwanja, baadhi ya Diaspora wenye asili ya Tanzania, wamekuwa wakiwekeza kwa kununua Hisa hapa nchini, Takwimu kutoka Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS), zinaonesha kuwa, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2022, Diaspora wenye asili ya Tanzania waliwekeza katika Scheme mbalimbali za UTT- AMIS, kwa uwekezaji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.5”
0 Comments