Ticker

7/recent/ticker-posts

KASI YA UJENZI NA UKARABATI WA BARABARA,TARURA YAACHA KICHEKO VIJIJINI NA MIJINI

  

Mtendaji Mkuu TARURA Mhandisi Victor Seff, akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)

NA JIMMY KIANGO

Miaka saba ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetosha kuacha kicheko kizito kwa idadi kubwa ya Watanzania vijijini na mijini.

 

TARURA yenye kauli mbiu ya Barabara bora kwa maendeleo endelevu ilianza kufanya kazi rasmi Julai 1,2017  kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali Sura Na. 245 na kutangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 211 la Mei 12,2017.

 

Dhamira ya kuundwa kwa Wakala haya lilikuwa ni kukabiliana na mabadiliko katika sekta ya Barabara kwa kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika kusimamia barabara za Wilaya na kukabiliana na changamoto zilizojitokeza wakati jukumu la usimamizi wa mtandao wa barabara za wilaya lilipokuwa chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) 184.

 

Hadi kufikia Juni 2024, TARURA imefanikiwa kushughulikia kilomita 144,429.77 za barabara za wilaya kwa viwango vya lami, changarawe na udongo, ambapo kati ya hizo barabara za lami ambazo ni nzuri ni kilomita 2,743.81, wastani ni 445.18 na mbaya ni kilomita 148.68 ambazo jumla yake ni kilomita 3,337.66 sawa na asilimia 2.31.

 

Barabara za changarawe ambazo zimeshughulikiwa na TARURA kwa miaka hiyo saba ni kilomita 42,059.17 sawa na asilimia 29.12, ambapo barabara nzuri ni kilomita 21,890.53, za wastani ni kilomita 15,742.23 na mbaya ni kilomita 4,426.41.

 

Zile zilizojengwa kwa udongo hadi kufikia Juni mwaka huu nzuri ni kilomita 16,118.65, wastani ni kilomita 34,739.20 na mbaya ni kilomita 48,175.09 ambazo ni sawa na kilomita 99,032.93 sawa na kilomita 68.57.

 

Hatua hii inaifanya TARURA kuwa taasisi ya kiserikali iliyoweza kugusa maisha ya Watanzania wengi kwa muda mfupi hali inayoacha kicheko kwenye maeneo mengi ya nchi.

Wahariri wa Waandishi waliohudhuria mkutano wa TARURA

 Ukweli wa hilo umekuwa ukionekana katika maeneo mbalimbali, ambapo hata mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu wa 2024 ulitoa pongezi kwa TARURA kwa kufanya kazi kwa ufanisi pamoja na kutumia kikamilifu mfumo wa manunuzi kwa njia ya kidijitali yaani NeST wakati wa kutangaza zabuni zake kama yalivyo matakwa ya Serikali.

 

Kama hiyo haitoshi hata wakazi wa mji wa Tunduru wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma waliipongeza kwa kazi nzuri ya kujenga na kukamilisha mradi wa ujenzi wa Barabara za mitaa kwa kiwango cha lami.

 

Wameweka wazi kuwa Barabara za lami zilizojengwa kwa viwango bora katika mitaa yao zimesaidia sana kupendezesha mji wa Tunduru na kuongeza  thamani ya maeneo yao,kuondoa changamoto ya usafiri na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wilaya kwa ujumla.

 

Septemba 2,2024 Mtendaji Mkuu TARURA Mhandisi Victor Seff, alikutana na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari jijini Dar es Salaam ili kuelezea mafanikio na changamoto walizokutana nazo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Mhandisi Seff, aliwaambia Wanahabari kuwa pamoja na kukabiliwa na changamoto ya fedha, lakini wamedhamiria kuhakikisha wanatunza barabara zilizo katika hali nzuri na hali ya wastani kubaki katika hali hiyo ili kulinda uwekezaji ambao tayari umefanyika.

 

Aidha wamedhamiria kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili mtandao huo uweze kupitika misimu yote pamoja na kuongeza kazi ya matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana katika eneo la kazi katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira pamoja na kupandisha hadhi barabara za udongo kuwa za changarawe na za changarawe kuwa za lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii, mipango ya muda mrefu ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, Manispaa na miji.

 

Mtendaji Mkuu TARURA Mhandisi Victor Seff, (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa Wakala hiyo.

Kwa sasa TARURA ipo kwenye utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Pili toka kuanzishwa kwake mwaka 2017 ikiwa na lengo kuwa, ifikapo mwaka 2025 angalau asilimia 85 ya barabara za Wilaya ziwe zinapitika kwa misimu yote.

 

Mpango mkakati huo ambao umeanza kutekelezwa mwaka 2021/22 una lengo la kujenga barabara za lami km 1,450.75 ambao utasaidia nchi kutoka kuwa na km 2,404.90 na kufikia km 3,855.65, changarawe km 73,241.57 ambazo zitaifikisha nchi kwenye km 102,358.14 kutoka 29,116.57 za sasa na madaraja 945 ambayo yataongeza wingi wa madaraja na kufikia 3,758 kutoka 2,813 ya sasa.

Mhandisi Seff amesema hadi kufikia sasa utekelezaji wa mpango mkakati huo umefikia asilimia 50 ya malengo, ambapo pia aliishukuru serikali ya Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya Wakala kwa mwaka katika mkakati wa kwanza n ahata huu wa pili.

 

“Mahitaji halisi ya Bajeti ya Wakala kwa kila mwaka ni shilingi trilioni 1.635 hata hivyo wastani wa bajeti inayotengwa ni shilingi bilioni 850.

“Tathmini iliyofanywa mwaka 2022/23 ilibaini kuwa shilingi 1.635 trilioni zinahitajika kwa mwaka kuanzia mwaka 2023/24 ili asilimia 85 za mtandao wa barabara za wilaya uweze kupitika misimu yote, kwa sasa TARURA inapata wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwaka.”

Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga .
 

Aidha alisema ongezeko la bajeti ingawa halijafikia lengo, lakini limesababisha mafanikio ambapo kwa miaka mitatu ya utekelezaji wa mpango mkakati 2021/24 wameweza kujenga barabara za lami zenye urefu wa km 923.96, changarawe km 22,815.98 na madaraja 378.

 

Mbali na kushughulika na miradi midogo, pia TARURA imetekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa 58.5 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, ujenzi wa daraja la Berega lenye urefu wa mita 140 lililopo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, ujenzi wa barabara ya Visiga-Zegereni mkoani pwani yenye urefu wa km 12.5 kwa kiwango cha lami.

 

Mradi mwengine mkubwa ni ujenzi wa barabara ya Nala yenye urefu wa kilometa 5.1 kwa kiwango cha lami ambayo ipo kwenye eneo la Viwanda ndani ya jiji la Dodoma, km 12.8 za lami na mifereji mikubwa ya maji iliyopo Mbweni, jijini Dar es Salaam.

 

Mkuu wa kitenho cha Uhusiano na Mawasiliano TARURA, Catherine Sungura akizungumza jambo na Wahariri (hawapo pichani)

TARURA pia imejenga madaraja ya chuma katika maeneo ya Kihansi-Mlimba, Ruipa -Kilombero mkoani Morogoro, Mbuchi -Kibiti mkoani Pwani, Miyuge Ikungi mkoani Singida, daraja la Kalambo-Rukwa, barabara za lami Mwangaza-Kisasa-Medeli km 10.1 na Swaswa-Mpamaa-Arusha road km 8.2.

 

Mhandisi Seff, amewaahidi Watanzania kuwa TARURA itaendelea kuhakikisha inasimamia na kupandisha hadhi barabara zote zinazokidhi vigezo za  vijijini na mijini ili kuhakikisha Watanzania wanaepukana na adha ya barabara mbovu.

 

Post a Comment

0 Comments