Ticker

7/recent/ticker-posts

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA SHERIA KWENYE SHUGHULI ZA UHIFADHI


 Na.Joyce Ndunguru, Morogoro.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imesisitiza matumizi ya sheria na kanuni katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uhifadhi.

Hatua hiyo ya serikali ni imelenga kuwakumbusha watumishi walio chini ya wizara hiyo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi. 

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba ndie ametoa msisitizo huo Septemba 1,2024 katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya kwenye ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo, mkoani Morogoro.

 

Kamishna Wakulyamba alifika ofisini hapo kwa lengo la kuongea na watumishi na kuimarisha utendaji kazi pamoja na kukagua maeneo ya kazi.

 

"Kama wahifadhi tunapaswa kufahamu sheria zote zinazosimamia masuala ya uhifadhi zilizopo katika Taasisi zetu pamoja na Taasisi zingine za uhifadhi zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

"Pamoja na kufahamu sheria na kanuni zilizopo ndani ya Wizara yetu, ni vyema pia  kufahamu na kuzingatia sheria nyingine za nchi ambazo zinatuzunguka ili ziweze kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu, mfano sheria inayohusiana na ukusanyaji wa vielelezo  kuanzia kwenye ukamataji hadi kuwasilishwa mahakamani," alisema.

 

Aidha Kamishna Wakulyamba aliwapongeza Askari  kwa kazi nzuri wanazofanya na amewaasa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu.

 

Awali, Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za uhifadhi, Mlage Kabange alitoa taarifa kuhusu 

masuala mbalimbali yanayosimamiwa na TAWA huku akibainisha mafanikio na  changamoto ya wanyama wakali na waharibifu hususan katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

 

Katika ziara hii ya kikazi, Kamishna Wakulyamba aliambatana na Maafisa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi , Mrakibu wa Polisi Joseph Jingu na Mrakibu wa Polisi Ocsar Felician waliopata fursa ya kutoa mafunzo maalum kwa watumishi wa TAWA.

 


Post a Comment

0 Comments