NA MWANDISHI WETU
Ongezeko la Wanyamapori ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro iliyoanzishwa mwaka 1959 likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 8,292, wananchi takribani 8,000 na mifugo isiyozidi 260,000, limekuwa tishio kwa mifugo na binadamu wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Imeelezwa kuwa kwa sasa idadi ya wananchi katika eneo hilo inakadiriwa kufikia zaidi ya 110,000, mifugo zaidi ya laki nane huku idadi ya wanyamapori ikiongezeka zaidi huku ukubwa wa eneo ukisalia kuwa ni ule ule.
Ongezeko la wanyamapori limetajwa kuongeza hatari kwa maisha ya binadamu na mifugo ambapo mara kadhaa wamekuwa wakifanya mauaji ya wananchi na kwa takribani katika kipindi cha miaka sita watu 68 wameshapoteza maisha na wengine 223 kujeruhiwa.
Matukio haya kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na ongezeko la wanyamapori hasa Simba hali inayohatarisha maisha ya binadamu na mifugo yao.
Wanyamapori wanaotajwa kuwa tishio zaidi kwa binadamu na mifugo yao ni simba, tembo, Nyati, fisi na viboko.
Afisa Tarafa ya Ngorongoro, Bahati Mfungo anasema moja ya sababu iliyoisukuma serikali kuwahamisha watu kutoka kwenye hifadhi hiyo na kuwapeleka katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine ili pamoja na mambo mengine kuwanusuru majanga hayo na kuboresha maisha yao.
“Kinachotokea ni kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka na wanyamapori nao wamekuwa wakiongezeka hivyo kuwepo na hali ya kugombania eneo baina ya binadamu na wanyamapori jambo ambalo limekuwa likiwafanya wananchi katika eneo hili waishi katika mazingira magumu” alisema Mfungo.
Aliongeza kuwa jambo la msingi kwa sasa ni kwa wananchi kuitikia wito wa serikali wa kuhama katika eneo hilo ili kuokoa maisha yao kwani mamlaka zimekuwa zikithamini uhai wa wananchi na hivyo kutafuta njia ambazo zitaokoa maisha yao.
Matukio haya yameleta hofu na taharuki miongoni mwa jamii za wenyeji, wengi wakihofia usalama wao na wafamilia zao huku wengine wakikiri kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la Wanyama pori hifadhini hata kufikia hatua ya kuwa karibu na makazi ya watu.
Mkazi wa Kijiji cha Bulati, kata ya Nainokanoka, Tarafa ya Ngorongoro, Kambatai Liariti Orkedienye (32) ambaye ni mmoja wa waathirika wa matukio ya kujeruhiwa na wanyamapori yaliyotokea hivi karibuni ndani ya Hifadhi anasema ilikuwa ni siku ya jumanne ya Julai 9,2024, saa 3:00 asubuhi ambapo kama ilivyo ratiba yake ya kila siku, aliamka na kwenda kuchunga maeneo ya Embakai Kreta, akiwa huko ghafla ng’ombe wake walivamiwa na simba wawili na baada ya kusikia kelele za ng’ombe alisogea na ndipo hapo simba mmoja alimwona na kumvamia.
“Niliposikia kelele za ng’ombe nilisogea na kuwaona simba wawili wakiwa wamewavamia ng’ombe na hapo hapo simba mmoja alinikimbilia na kunijeruhi mkono na kwenye mbavu nilidondoka chini na sikuweza tena kuelewa chochote baada ya hapo nilipoteza fahamu na baadaye nilijikuta nipo hospitali”. alisema Kambatai.
Tukio hili ni miongoni mwa matukio kadhaa yaliyoripotiwa kutokea likiwemo la mzee Melau Olenjoni aliyekuwa na umri wa miaka 60 kutoka Kijiji cha Nainokanoka aliyeshambuliwa na simba usiku wa Mei 4,2024 na kupoteza maisha.
Haya ni baadhi tu ya matukio yaliyoripotiwa kati ya mengi ambayo yamekuwa yakitokea ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, usalama wa wananchi wanaoishi Hifadhini umekuwa hatarini kutokana na ongezeko la wanyama ndani ya Hifadhi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa kijiji kwenye tarafa hiyo wanasema kwamba matukio ya watu kuuawa ama kujeruhiwa yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini wananchi wengi wamekuwa hawatoi taarifa polisi na katika vyombo vingine vya usalama.
Afisa Tarafa ya Ngorongoro Bahati Mfungo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwaelimisha wananchi wa tarafa hiyo ili waweze kuhama katika tukio hilo na kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kuboresha maisha na kunusuru uhai wa wananchi hao.
Mpango wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwaelimisha wananchi hao ili waweze kuhama na kuhamia maeneo mengine ambapo inakadiriwa kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu idadi kubwa ya wananchi watakuwa wamefikiwa.
AFRINEWS SWAHILI, ilimuuliza kwa ujumbe mfupi Kaimu Meneja Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Hamis Dambaya kama kuna ukweli juu ya kuongezeka kwa kasi ya Wanyamapori wakali hasa simba ambao wanashambulia watu na mifugo katika Kijiji cha Bulati Kata ya Nainokanoka, Tarafa ya Ngorongoro, alijibu kwa kifupi kuwa ni kweli.
“Ni kweli kaka.”
0 Comments