Ticker

7/recent/ticker-posts

WAFUGAJI BABATI WAJENGEWA MAZIZI YA KISASA YANAYOZUIA MIFUGO KULIWA NA SIMBA

 

Baadhi ya Askari wa Wanyamapori wakiwa ndani ya moja ya mazazo ya kisasa yaliyojengwa kwa waya. 

Mwandishi wetu, Babati.

 

Moja ya kero wanazokutana nazo wafugaji wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya Wanyamapori ya Burunge(Burunge WMA) wilayani Babati, Mkoa Manyara ni mifugo yao kushambuliwa na kuliwa na wanyamapori wakali mara kwa mara.

 

Hali hiyo imekuwa ikiwarudisha nyuma kila mara, katika kukabiliana na zahama hiyo Taasisi ys Chem Chema ambayo inafanya shughuli za uhifadhi na Utalii katika eneo hilo, lilipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na  Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara imewajengea Mazizi ya waya (Boma Hai) jirani na maeneo hayo.

 

Mazizi hayo yanasaidia kuzuia wanyama wakali hasa Simba na Fisi kuvamia na kula  mifugo nyakati za usiku, hatua hiyo ni sehemu ya Mkakati wa Taasisi hiyo, kupunguza migongano baina ya Binadamu na  Wanyamapori.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi mazizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Babati , mkoa wa Manyara, Lazaro Twange  alisema  mradi wa ujenzi wa mazizi hayo ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kupunguza migongano baina ya Binadamu na wanyamapori.

 

Twange ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Babati, Khalfani Malipula alisema Kazi nzuri ya uhifadhi imefanyika na sasa kuna changamoto ya wanyamapori kula mifugo jambo ambalo limeanza kupatiwa suluhu.

Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii ya Chem Chem, Napendaeli Wazoeli, akimkabidhi zizi mfugaji, Peter Martin.
 

Alisema uzinduzi wa Mazizi hayo, ambao umeambatana na maadhimisho ya siku ya Askari wa hifadhi duniani(Rangers Day), unatarajiwa pia kuwaondolea wananchi adha ya kulala nje kulinda mifugo yao.

 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zizi lake, John Bagary  mkazi wa kijiji cha Vilima vitatu alisema, hadi juzi ng'ombe wake watano na mbuzi wanane wameliwa na Simba.

 

"Nimekuwa nikilala nje kulinda zizi langu la ng'ombe na mara kwa mara Simba wamekuwa wakifika hapa usiku, lakini sasa nashukuru kujengewa zizi lenye uzio na lina taa zinazotumia mwanga wa jua ili kuzuia Simba kuruka na kuingia ndani, "alisema.

 

Peter Martin mkazi wa kijiji cha Ngoley, alishukuru Chem Chem na Serikali kwa kuwajengea mazizi hayo, kwani sasa watakuwa wanalala kwa amani.

 

Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii ya Chem Chem, Napendaeli Wazoeli alisema taasisi yao kwa kushirikiana na askari wanyamapori, waliona kuna haja ya kuitumia siku ya maadhimisho ya askari wa wanyamapori duniani, kukabidhi mazizi hayo.

 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Khalfani Malipula, (aliyesimama) akizungumza na wafugaji.


Alisema kila zizi limekuwa likigharimu zaidi ya sh 2.6 milioni  na hadi jana mazizi 15 tayari yalikuwa yamejengwa na Taasisi hiyo, lengo ni kupunguza migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.

 

Mbali na Mazizi hayo, lakini pia Chem Chem walitoa vifaa vya kufukuza wanyama katika makazi ya watu, ikiwepo baruti, vuvuzela, pilipili  na tochi maalum za kufukuza wanyamapori.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge WMA, Erick Lilayoni alisema hifadhi hiyo, itaendelea kushirikiana na Chem Chem na wadau wengine ili kuhakikisha hifadhi inaendelea kuwa kivutio cha watalii.

 

Alisema wanaipongeza taasisi ya Chem Chem kwa msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitoa katika Jumuiya hiyo lakini pia kwa wananchi wanaishi ndani ya hifadhi hiyo.

 

"Leo tumeona askari wote wanaolinda hifadhi hii wamepewa medali na vifaa vya kufukuza wanyamapori , sisi tunaamini huu ni mwendelezo tu Chem Chem kusaidia uhifadhi katika eneo letu"alisema.

 

 

Malipula akimvisha medali mmoja wa Askari wa Wanyamapori.

Napendaeli Wazoeli akitoa maelezo kuhusu zizi la kisasa kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Khalfan Malipula.

Post a Comment

0 Comments