Ticker

7/recent/ticker-posts

WANYAMAPORI NI MUHIMU KWENYE UTALII, WANACHANGIA 17.5% YA PATO LA TAIFA

  

Afisa Mhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Winniefrida Kweka.

Na Beatus Maganja 

 

Sekta ya Utalii ni moja ya maeneo yanayochangia pakubwa pato la taifa, inakadiriwa kuwa asilimia 17.5 inatoka kwenye eneo hilo la maliasili na utalii.

 

Mbali na sekta hiyo kuchangia pato la taifa, lakini pia imekuwa na mchango mkubwa kwenye kuiingizia nchi fedha za kigeno, ambapo asilimia 25 ya fedha za kigeni zinatoka kwenye eneo hilo.

 

Hata hivyo umuhimu wa sekta hiyo unakolezwa zaidi na Wanyamapori ambao wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na wale wa ndani.

 

Afisa Mhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Winniefrida Kweka amethibitisha ukweli wa hilo Agosti 4,2024 alipokuwa akitoa elimu ya uhifadhi kwa mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma waliotembelea bustani ya wanyamapori hai iliyopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maonesho ya NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni.

 


"Wanyamapori wanachangia kwa kiasi kikubwa makusanyo yanayotoka kwenye Sekta ya utalii kwa zaidi ya asilimia 17 za pato la taifa," amesema.

 

Winniefrida amesema kutokana na faida zitokanazo na wanyamapori hao kwa nchi, TAWA inatumia maonesho hayo kuwaelimisha watanzania wote kuachana na mitazamo hasi kuwa wanyamapori ni viumbe wasio na mchango chanya kwa Taifa.

 

Aidha Mhifadhi huyo amesema kutokana na changamoto inayoletwa na baadhi ya wanyamapori wakali na waharibifu kama vile mamba, tembo, fisi na wengine, TAWA imekuwa ikielimisha umma juu ya mbinu rafiki za kuweza kuishi na wanyamapori hao na  kuendelea kubaki  salama kwa kuepuka  madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.

 

 Vilevile Winniefrida amebainisha kuwa chanzo kikubwa cha migongano baina ya wanyamapori  hususani mamba na binadamu ni pale ambapo binadamu anapokuwa anahitaji mahitaji yake sehemu ambapo wanyamapori hao wapo (majini).

 


Amesema kufuatia changamoto hiyo Serikali  kupitia Taasisi zake za kiuhifadhi imekuwa ikitoa elimu ya  kujilinda dhidi ya athari zinazoweza kusababisha na wanyama hao ikiwa ni pamoja   na kusaidia katika ujenzi wa vizimba  vya mfano ili kuepusha madhara ya wanyamapori hao.

 

Winniefrida ametoa wito kwa  wavuvi  kufanya shughuli zao za uvuvi kwa njia zilizo sahihi na kuepuka kutega mitego yao ya Samaki sehemu ambazo  mamba walipo na kuachana na  dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa palipo na mamba ndipo pana samaki wengi.

 

Maonesho ya mwaka huu yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na uvuvi" yalianza tarehe Agosti 01, 2024 na yanategemewa kufika kilele Agosti 08, 2024.

 

 


Post a Comment

0 Comments