Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Matumizi ya Ardhi, Joseph Mafuru |
NA SIDI MGUMIA, DODOMA
Mkurugenzi
Mkuu wa Tume ya Matumizi ya Ardhi, Joseph Mafuru amesema
ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kuyalinda mazingira na kutekeleza kwa
urahisi mipango ya matumizi ya ardhi nchini.
Mafuru
ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi kutoka Chama Cha Waandishi wa
Habari za Mazingira Tanzania ( JET), wanaotekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili
chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani
la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), waliotembelea Ofisi za Tume ya Matumizi ya
Ardhi mjini Dododma hivi karibuni.
Ameeleza kuwa wadau hao ambao ni wa uhifadhi,
wananchi, taasisi za wanyamapori na wengineo wanapaswa kushirikishwa katika
kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kisha kusimamia kwa pamoja ili
kurahisha utekelezaji.
“Ili
uweze kuwashirkisha wadau, inafaa kuanza kuandaa mipango ya ardhi kwa pamoja na
kisha mkaisimamia kwa pamoja hivyo kuitekeleza inakuwa ni rahisi sana.
Usipowashirikisha utekelezaji wake utakuwa mgumu sana, kwahivyo kuna haja ya
wadau wote kushiriki kwa pamoja kuhakikisha zoezi hilo linafanyika vilivyo,”
alisema Mafuru
Aidha,
Mafuru alisema kuwa kama Tume wanapambana kupata wadau wakutosha ili
kuhakikisha wanaongeza kasi yakuandaa mipango ya matumizi ya ardhi. Vijiji
vilivyoandaliwa mipango kwa sasa ni vichache sana ambapo ni vijiji 3000 tu kati
ya vijiji 13,000 na hii maana yake bado kuna kazi kubwa yakufanya.
“Tukiongozwa
na Serikali ikifuatiwa na wadau wengine kwenye masuala ya uhifadhi mazingira na
wanyamapori, tunapaswa tuhakikishe tunatengeneza mipango yakutosha. Kwani kadri
tunavyozidi kuchelewa kutengeneza maana yake tunaendelea kutengeneza migogoro
kati ya wanyamapori na binadamu, hivyo ni heri tukaifanya mapema hiyo mipango
ili kuepusha hiyo migogoro,” alisema Mafuru.
Kama Tume wameweka kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha unaoendelea wa 2024-2025, wametenga bilioni tano na zaidi kwa ajili yakuhakikisha kwamba kazi hizo zinafanyika kwa ufasaha.
Mkurugenzi wa Utafiti na Uzingatiaji wa
Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Joseph Paul
Akizungumzia mafanikio ya kuwepo kwa mipango ya matumizi ya ardhi, Mkurugenzi wa Utafiti na Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dkt. Joseph Paul amesema, mipango ya matumizi ya ardhi imesaidia wanakijiji kutokuingia maeneo ya hifadhi lakini pia imesaidia kuongoa mapito ya wanyama na kuwafanya wapite kama ambavyo wanapaswa kupita.
“Kimsingi
tunafahamu wanyama kama tembo huwa hawasahau njia zao, kwa kupitia Serikali za
vijiji lakini pia wazee ambao wana uzoefu na maeneo hayo wamesaidia kuainisha
maeneo ambayo yana umuhimu wa uhifadhi kuyatenga kwa matumizi rafiki ambayo
hayatazuia wanyama kupita lakini shughuli za kibinadamu kuendelea,” alisema
Paul
Paul
alisisitiza kuwa mfano wa hilo ni upande wa Kaskazini ambapo mpango wa matumizi
ya ardhi umesaidia katika kupanga matumizi nyanda za malisho kwa jamii ya kule.
Amesema
kimsingi Tume ya Taifa ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi imeratibu na kusaidia
uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya kanda, mkoa, kwa mfano
ukanda ambao ni muhimu kwa uhifadhi kama mkoa wa Mara, mpango umeendelea
kuandaliwa ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya ardhi.
“Lakini
pia tumegundua kwenye tafiti zetu kwamba ili tusaidie kusiwe na muingiliano wa
kimatumizi kuna umuhimu wakuboresha maisha ya wananchi wenye maeneo yao. Moja
ya njia za kuboresha ni kuhakikisha kwamba wana uhakika wa umiliki wa ardhi,
kwahivyo tume imewezesha uandaaji hati miliki za kimila zaidi ya 20,000 kwa
maeneo yenye umuhimu wa uhifadhi. Wanakijiji wa maeneo hayo wamepewa hati
miliki za kimila kwa kuzingatia vigezo mbalimbali pamoja na kuhakikisha kuwa
jinsia katika umiliki inazingatiwa, kwenye familia tumehakikisha mume na mke
wanamilikishwa yale maeneo yao pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji
wa ndani na nje ili kusaidia wananchi kutumia maeneo yao vizuri kwa kilimo na ufugaji
wenye tija,” alisema Paul
Pamoja
na hilo, Paul alisema kuwa ukosefu wa elimu ya matumizi bora ya ardhi bado ni changamoto
kwa wanajamii, hivyo bado wanaendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa
utunzaji na umuhimu wa utekelezaji mpango wa matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Ardhi wa Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Nyirembe Munasa alisema ili kuwe na maendeleo endelevu wanapendekeza kuwe na mipango ya matumizi ya ardhi katika mikoa yote nchi nzima, na kanda zilizopo mfano ikolojia ya ziwa Victoria, Tanganyika, Serengeti na kwingineko, inahitajika kuhifadhi maeneo ya ikolojia kwa kuzingatia matumizi ya ardhi katika ngazi za mikoa.
“Kuna
umuhimu mkubwa sana kulinda mifumo ya ikolojia, lakini nchi yetu ina mifumo mingi
ya ikolojia ambayo hailindwi hasa hizi shoroba ambazo wanyama hutumia kutoka kwenye
hifadhi moja kwenda nyingine. Kwa bahati mbaya sana unakuta miongoni mwa hizi
shoroba nyingi sana zimezibwa kwa aidha shughuli za kilomo au makazi ya
binadamu jambo linalosababisha migongano kati ya wanyama na binadamu. Hakukuwa
na mikakati au mipango ambayo ilikuwa inaelekeza namna gani hayo maeneo
yahifadhiwe. Lazima tufanye uongoaji wa hizi shoroba kwa kutumia mipango
shirikishi ya matumizi ya ardhi, kuwe na maendeleo endelevu sababu yana umuhimu
wake kuchumi, kijamii na pia katika mambo ya mazingira na kiikolojia,” alisema
Munasa
Aliongeza,
“Kuhusu shoroba ziko 66 lakini ni mbili tu ndizo zimefanyiwa kazi ikiwemo
shoroba ya Ifakara. Changamoto kubwa iliyokwamisha zoezi hili ni fedha na hii
ni kwasababu shoroba ziko nyingi na tunahitaji kuwa na mipango ya matumizi
katika vijiji vyote vinavyopitiwa na shoroba,”.
Nae Mkurugenzi Msaidizi Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Rehema Kishoa ameongeza kuwa kama hakuna usimamizi mzuri hizo shoroba hazitakuwepo, mipango itapangwa lakini hazitakuwepo, kwahiyo ni vyema kuangalia namna yakuwashirikisha wananchi wakati mipango inaandaliwa kwasababu wao ndio wahusika wakuu katika suala zima la kuwepo ama kutokuwepo kwa shoroba hizo.
“Tume
ina wajibu wakuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa kwa ngazi zote
inasimamiwa kama ilivyopangwa. Muhimu kwa wanajamii, watalaamu na wadau
wengineo kushirikiana juu ya masuala ya ardhi,” alisema Kishoa
Hata hivyo, Mkurugenzi wa JET, John Chikomo ameongeza kuwa katika mapambano dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi elimu ya mazingira na haswa uhifadhi bado inahitaji ipelekwe kwenye jamii lakini pia kusisitiza uwepo wa ushirikishwaji wa sekta na wizara mbalimbali katika masuala ya mazingira.
0 Comments