NA ELIAS SHADRACK-AFRINEWS SWAHILI- Dar es Salaam
Uongozi wa klabu ya Simba umeshindwa kuendelea kushikilia msimamo wake wa kumzuia kiungo wao wa kimataifa, Clotus Chota Chama kurejea kikosini. Chama raia wa Zambia, alisimamishwa kwenye timu hiyo Desemba 21,2023 kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mtovu wa nidhamu.
Kiungo huyo mwenye magoli mawili ndani ya msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, alisimamishwa pamoja na beki wa kati wa timu hiyo Nassoro Kapama ambae hatma yake hadi sasa haijawekwa wazi.
Leo Februari 2,2024 uongozi wa klabu hiyo umetangaza hatma ya mchezaji huyo kwa kudai kuwa wamekubaliana kumsamehe na tayari ameshaelekea mkoani Kigoma kuungana na wenzake tayari kwa kukamilisha maandalizi ya mchezo wao wa Ligi Kuu utakaochezwa kesho Februari 3,2024 mkoani Kigoma dhidi ya timu ya Mashujaa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma, iliyotolewa na Afisa Mtandaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Imani Kajula, uamuzi huo wa kumsamehe Chama umetokana na matakwa ya Kamati ya Ufundi ya bodi ya Simba.
“Hatua hii imefuatia uamuzi wa Kamati ya Ufundi ya bodi ya Simba, ambayo ilipitia barua ya maelezo ya Chama na maombi ya kocha wao Abdelhack Benchikha alietaka mchezaji huyo asamehewe.
" Mambo hayo yaliisukuma kamati ya ufundi ya bodi ya Simba kuridhia kumsamehe na kusitisha kumfikisha kwenye kamati ya maadili ya klabu."
0 Comments