NA ELIAS SHADRACK-AFRNEWSSWAHILI-DSM Timu ya Simba, leo Februari 3,2024 imerejea kwa kishindo kwenye michezo ya Ligi Kuu ya NBC kwa kuichapa timu ya Mashujaa bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, uliopo mkoani Kigoma.
Mchezo huo ulikuwa ni sehemu ya michezo ya viporo ya Simba, ambayo ilipaswa ichezwe mwaka jana, lakini walilazimika kutoicheza kutokana na kukabiliwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ambayo hadi leo imecheza michezo 11 ni miongoni mwa timu saba zenye michezo ya viporo, huku timu tisa zikiwa zimeshacheza michezo 14 kila moja.
Ikiwa ugenini Simba ilionesha soka safi ambapo iliwachukua dakika 16 kupachika bao lililowekwa kimiani na Saido Ntibanzonkiza kwa mkwaju wa penati uliosababishwa na rafu aliyochezewa Kibu Dennis ndani ya eneo la hatari.
Ushindi huo umeisaidia Simba kuwa na alama 26 zinazowasogeza kwenye mbio za ubingwa ambazo kwa sasa zinaongozwa na timu ya Azam nafasi ya kwanza na Yanga nafasi ya pili huku zote zikiwa na alama 31.
Katika mchezo wa leo Simba iliwakosa wachezaji wake muhimu, Enok Inonga ambae yuko katika majukumu ya timu yake ya Taifa ya DRC pamoja na Che Malone ambaye anadaiwa kuwa nachangamoto za kifamilia.
Ndani ya mwezi huu Simba
inatarajiwa kucheza michezo sita ya Ligi Kuu ya NBC na mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas utakaochezwa Februari 24,2024 nchini Ivory Coast.
0 Comments