Ticker

7/recent/ticker-posts

WWF: KUNA TISHIO LA KUTOWEKA BIOANUWAI DUNIANI

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-MOROGORO 

Lipo tishio kubwa la kutoweka kwa viumbe hai na ikolojia ulimwenguni. Katika kipindi cha miongo minne iliyopita kasi ya kuzaliana imeporomoka kwa viwango vya juu. 

Ripoti ya mfuko wa kimataifa wa Uhifadhi Wanyamapori WWF iliyotolewa hivi karibuni imeonesha kuwa idadi kubwa ya viumbe imepotea kutokana na uchu wa binadamu na shughuli zake na hali hiyo inayotishia ustawi wa siku za usoni. 

Taarifa za ripoti hiyo mpya iloyopewa jina la sayari hai au´the living planet´ zinaonesha kuwa kwa jumla idadi ya wanyama walio na uti wa mgongo inayojumuisha ndege, amfibia, reptilia, samaki na mamalia imepungua kwa asilimia 60 tangu mwaka 1970. 
 
WWF imesema idadi ya viumbe vinavyoishi kwenye maji baridi hususan samaki imeporomoka kwa wastani wa asilimia 83 kutokana na shughuli za ujenzi wa mabwawa makubwa, uvuvi uliopindukia, ongezeko la watu duniani pamoja na magonjwa yanayowakabili. 

Ikolojia ya eneo la ukanda wa kitropiki la amerika ya kati na kusini inakopatikana pia misitu ya amazon ndiyo imeathirika zaidi kwa wastani wa asilimia 89 sababu kubwa ikiwa ni ukataji miti uliokithiri.
 
Kulingana na WWF tangu mwaka 1500 shughuli za kilimo na uvunaji umekuwa sababu ya kupotea kutoka uso wa dunia kwa hadi asilimi 75 ya viumbe jamii ya mamalia, ndege, reptilia, amfibia na mimea. 

Kitisho kingine kilichoangaziwa na ripoti hiyo ni suala la makazi ya viumbe ambapo takwimu mpya zinaonesha ni robo pekee ya eneo la ardhi duniani lililobaki katika hali ya asili huku maeneo ya ardhi oevu yakipungua kwa hadi asilimia 87 kutokana na watu kujenga juu ya maeneo hayo, ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia nchi. 

 Matumbawe na wadudu wachavushaji nayo yako hatarini kutoweka Ongezeko la joto linalotokana na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa pia limegeuka kitisho kikubwa kwenye ikolojia ya bahari ambapo kiasi nusu ya matumbawe ambayo ndiyo chanzo cha uhai kwa hadi robo ya viumbe vya baharini imepotea.  

Jopo la Umoja wa mataifa lilionya mwezi uliopita kuwa hata ikiwa ulimwengu utafanikiwa kupunguza ongezeko la joto kwa kiwango cha nyuzi 1.5 kipimo cha selshesi bado itakuwa jambo gumu kuzuia kupotea kwa matumbawe. 

 WWF imeorodhesha pia wasiwasi wa kupotea kwa viumbe vinavyosaidia uchavushaji mimea ikiwemo nyuki, nondo, vipepeo, popo na jamii nyingine za ndege kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kuua wadudu na kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi kuwa miji. 

 Ripoti hiyo imetoa wito wa hatua za dharura kuchakuliwa ili kukabiliana na hali hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo ikiwa ulimwengu utahitaji kuokoa viumbe hai na baianui.

Post a Comment

0 Comments