Ticker

7/recent/ticker-posts

WAJASIRIAMALI WANAWAKE MOROGORO WAOMBA KUWEZESHWA MBINU ZA KULIMUDU SOKO LA USHINDANI KIMATAIFA

Katibu Tawala Msaidizi upande wa Biashara, viwanda na uwekezaji, Mkoa wa Morogoro, Beatrice Njawa akizungumza kwenye mafunzo ya wajasiriamali wanawake yanayoendeshwa na Chemba ya Biashara Tanzania (TWCC) mjini Morogoro mapema leo. 


 NA VICTOR MAKINDA-AFRINEWSSWAHILI MOROGORO 


 Wajasiriamali wanawake mkoani Morogoro wamewaomba wataalamu na wadau wa ukuzaji wa biashara nchini kutoishia mijini badala yake wafike pia vijijini kutoa elimu na usaidizi wa ukuzaji biashara ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika na zinazoweza kukabili ushindani wa soko la ndani na nje ya nchi. 

Wafanyabiashara hao wadogo waliyasema hayo jana Januari 21,2024 mkoani hapa, kwenye mafunzo ya wajasiriamali wanawake yaliyohusu kujua kanuni, taratibu na sheria za kufanyabiashara kwenye soko la Afrika (AICFTA) yaliyoandaliwa na Chemba ya wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC). 

Mmoja wa wajasiriamali hao Eva Kipalile mkazi wa Kijiji cha Mbingu kata ya Igima Wilayani Mlimba alisema, licha ya kuzalisha vikapu, ungo na mazao aina ya Kakao, wanakabiliwa na changamoto ya kukosa masoko ya nje kutokana na kukosa nembo ya kuhakiki ubora (TBS), Misimbomilia(Barcods) na usajili wa urasimishaji biashara kutoka BRELA. 

"Wataalamu wanapaswa kufika vijijini, wasiishie mjini, leo tumejifunza vitu vingi, wenzetu wanaweza kwenda kufanya biashara na mataifa mbalimbali, lakini sisi tunashindwa kutoka kwa sababu hatuna vitu muhimu vinavyoweza kutuingiza kwenye ushindani, vitu vingi tumevijulia hapa” alisema Kipalile. 

Makamu Mwenyekiti wa TWCC Taifa, Rose Romanus alisema ajenda yao ni kuhakikisha wanawake wanamiliki pesa kwa kutimiza malengo waliyojiwekea kwa kulifikia soko huru la Afrika. 

 Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala Msaidizi upande wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji mkoani hapa, Beatrice Njawa aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora zinazokidhi viwango vya soko la Afrika linalohudumia nchi 54.

Post a Comment

0 Comments