Ticker

7/recent/ticker-posts

MELI ILIYOBEBA WATALII ZAIDI YA 2000 YATIA NANGA DAR ES SALAAM

Matunda ya filamu ya Royal Tour iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka juzi, yameendelea kuonekana, ambapo leo Meli kubwa ya kitalii iliyobeba watalii 2210, imetia nanga kwenye bandari ya Dar es Salaam. 

 Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini, Damascus Mfugale, utalii wa meli kwa sasa ni zao la kimkakati nchini na ukuaji wake ni wa kasi. Mfugale ameyasema hayo leo Januari 16, 2024 wakati wa mapokezi ya meli kubwa iliyotia nanga katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa na jumla ya watalii 2,200 kutoka mataifa mbalimbali duniani inayozunguka kwa ajili ya kufanya utalii ambapo kwa Tanzania ilianzia visiwani Zanzibar. 

 “Kwa niaba ya bodi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii tunayo furaha kubwa kupokea meli hii kubwa ya Norwegian Dawn, imefika leo saa 12 asubuhi ikiwa imechukua watalii takribani 2210.


"Watalii hawa ambao ni zao letu la kimkakati kwenye sekta yetu ya utalii wanafahamika kama ni Watalii wa Meli au Cruise Ship Tourism, tunategemea katika kipindi cha miaka miwili au mmoja kuongeza idadi ya meli hizi kuja Tanzania”, amesema Mfugale. 

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika suala ya uchumi mpana wa utalii maana yake ni kwamba wageni wakija Tanzania watatembelea sehemu mbalimbali.

 “ Kwa mfano hawa wataondoka leo kwenda Selous, wengine wataenda maeneo mbalimbali hapa Dar es Salaam , wengine Museum na wengine wanakwenda Bagamoyo. “Kila wanapokwenda huko watatumia kama kwenye migahawa, kama ni kulipa kiingilio kwenye sehemu mbalimbali za vivutio. 


Kwa hiyo tunajivunia na hizi zote ni jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunategemea meli hizi zitaendelea kuja na mwezi wa pili tutakuwa na meli nyingine kubwa itakayokuja, hiyo ni katika muendelezo wa kuhakikisha kwamba utalii wa meli unakua,” amesema Mfugale.

Post a Comment

0 Comments