Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars raia wa Algeria, Adel Amrouche ameingia kwenye mvutano na mabosi wake kutokana na kauli zake tata alizozitoa hivi karibuni, akiwa Zanzibar, Misri na Ivory Coast. Amrouche kocha anayetajwa kuwa na kiburi, alianza kunukuliwa akiwaponda wachezaji wake kuwa hawana uwezo, zaidi wanachezea majina yao. Kama hiyo haitoshi, akiwa nchini Misri mara baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, aliendelea kukiponda kikosi chake hicho.
Kauli zake hizo zililazimika kuwekwa sawa na msaidizi wake ambae ni Mtanzania, Hemed Moroko.
Wapenzi wa mpira wakiwa hawajasahau kauli hizo, juzi Amrouche aliibuka tena na kauli tata kwa kuisema vibaya Morocco.
Amrouche amesema Morocco imekuwa ikilishinikiza Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuwapangia ratiba zinazowabeba ikiwa ni pamoja na kuwapangia muda mzuri wa wao kucheza mechi.
Kauli ya awali dhidi ya wachezaji wake iliwekwa sawa na msaidizi wake, lakini hii ya CAF na Morocco imepingwa na kukosolewa hadharani na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia.
Karia akiwa nchini Ivory Coast, ameweka wazi kuwa kauli aliyoitoa Amrouche dhidi ya CAF na Morocco ni yake na haina uhusiano wowote na Shirikisho lake ama Tanzania kwa ujumla.
Karia ambae pia ni mmoja wa wajumbe wa Kamati za CAF amesema kauli za uchochezi zilizotolewa na kocha huyo akiituhumu nchi ya Morocco kuwa inapanga ratiba za mechi za kimataifa za CAF ni zake.
"Hizo ni kauli zake, siyo msimamo wa TFF, inapaswa kufahamika kuwa TFF na Serikali ya Tanzania tumekuwa na ushirikiano mzuri na nchi ya Morocco pamoja na CAF."
Karia aliongeza kuwa kwa kuwa sasa wako kwenye mapambano ya michezo ya AFCON hawaoni sababu ya kukwaruzana na kocha wao, badala yake wanaelekeza nguvu zao kwenye mechi za Taifa Stars, ambapo pia amewataka wachezaji kutotilia maanani kauli za kocha wao na badala yake wajielekeze katika kupigania taifa.
Kauli za Karia dhidi ya Amrouche hazioneshi dalili yeyote ya kuendelea kumvumilia kocha huyo nje ya mashindano rasmi.
Kwamba akimalizana na AFCON naiona njia yake ikiwa nyeupe kurejea kwao kwa ajili ya kuendelea na maisha yake.
Ikumbukwe kuwa Amrouche ni raia wa Algeria na iko wazi kuwa Algeria na Morocco ni mahasimu wa kidiplomasia.
Nchi hizi mbili hazina uhusiano mzuri, hivyo basi kauli za Amrouche dhidi ya Morocco zinatazamwa na wadadisi wa masuala ya kidiplomasia kuwa ni kama ni muendelezo wa chuki zao za asili, ambazo hazina uhusiano wowote na Tanzania.
Hii inamaanisha kuwa endapo Stars itaendelea kumkumbatia Amrouche upo uwezekano mkubwa wa kuteteresha uhusiano mzuri wa kidiplomasia, kiuchumi na hasa kimichezo kati ya Tanzania na Morocco.
Lakini fikra zinakwenda mbali zaidi kuwa kauli tata za Amrouche dhidi ya CAF nazo zinaweza kuifanya Tanzania ikajitengenezea uhasama usio wa lazima na Shirikisho hilo la Afrika ambalo katika miaka ya karibuni limekuwa likifanya kazi kwa uzuri na TFF.
Uamuzi wa haraka wa Karia wa kutoka hadharani na kumkana kocha unatazamwa kama ni hatua za mapema za kuulinda uhusiano wa Tanzania, Morocco na CAF.
Haya na mengine mengi yanawasha taa ya kijani kwa Amrouche kuachwa na safari yake inaweza kuishia Ivory Coast mara baada ya kuhitimisha safari yake ya kushiriki michuano hiyo.
Salama ya Amrouche kuendelea kusalia Tanzania inaweza kupatikana kutoka kwenye matokeo mazuri ya jumla itakayoyapata kikosi chake kwenye michuako ya AFCON, nje ya hapo simuoni akifika Aprili 2024.
0 Comments