MAUTI ILIKUWA INAIWINDA ROHO YA "RAPHAEL DWAMENA" TANGU 2017.
-------------------------------------------------
By ✍️ Green Osward
Alikuwa akipita katikati ya jiji la Accra na kuona maghorofa ya kina Asamoah Gyan, Andrew Ayew, Samuel Kuffor, Michael Essien na wengineo. Ubongo wake unavamiwa na kichaa cha kupenda soka.
Aliamini soka ni kitu pekee kinachoweza kubadilisha maisha yake. Hakuwahi kuamini anaweza kutengeneza mamilioni ya pesa au kuwa tajiri nje ya mpira.
Mpira ulimaanisha kila kitu kwake.
Miguu yake ilikuwa inajiuza yenyewe kwenye macho ya mawakala. Alijaliwa kipaji cha kulijua goal. Alikuwa ni striker anayemiliki kimo kinachohitajika katika soko la sayansi ya mpira wa sasa.
2017 akiwa na umri wa miaka 22. Mechi ya kwanza kuichezea timu ya taifa ya Ghana dhidi ya Ethiopia. Aliingia kambani mara 2 katika ushindi wa goal 5.
Maskauti wa Brighton waligundua yeye ni dhahabu iliyojificha mchangani. wakamleta England wamtunuku malisho mema. Lilipokuja suala la afya vipimo vikamsaliti. Ikagundulika ana tatizo la moyo, Brighton wakaiua deal.
"Siku zote ukitaka kufanikiwa. Simamia kile unachokiamini hata kama dunia nzima itakuwa kinyume na wewe."
Huu msemo ulijenga ngome ya kudumu ndani ya ubongo wake. Hakuamini tatizo la moyo linaweza kuwa kizingiti kwenye mchakato wa kuzipeleka ndoto zake ulipo uhalisia.
Aliendelea kucheza soka. Lengo aitoe familia katikati ya shimo linalonuka tope la ufukara.
2019 akasajiliwa Zaragoza fc. Vipimo vya afya vikatenda dhambi ya kumsaliti kwa mara nyingine tena. Ikaonekana ana miguu ya dhahabu, lakini moyo wake hauwezi kuhimili mikiki mikimiki ya kukimbizana na Lionel Messi kwa dakika 90.
Zaragoza wakavunja mkataba. Hapo alikuwa ametoka Levante kwa mkopo.
Madktari walimshauri asicheze tena soka la ushindani. Lakini hakukubali. Aliamini kufuata ushauri wa madaktari wa kizungu ni kuzisaliti ndoto zake za utotoni. Tena ni kuishi nje ya misimamo ya kile anachokiamini.
2020 alipata timu inayoshiriki ligi kuu ya Denmark "BOLDKLUB." Vipimo vya afya vikagoma kumpa ushirikiano uliotukuka. Ikaonekana ana hitilafu ya moyo wakavunja mkataba.
2021 timu ya Austaralia "FC BLAU WEISS LINZ" Ilihitaji huduma yake. Baada ya kuona clip zake jinsi anavyozitendea nyavu ukatili. Tatizo la moyo ikawa kikwazo cha yeye kufika nchi ya ahadi. Raphael Dwamena's contract was terminated.
2023 Akaingia chaka ulaya mashariki nchini Albania. Akasajiliwa na timu ya KF EGNATIA. Haieleweki alisajiliwa bila vipimo vya afya?! Au clip za magoal yake ziliwapa wendawazimu?! Au alipofanya vipimo tatizo la moyo wake lilikuwa likizo siku ile?!
Hakuna anayejua.
Mwezi wa tatu mwaka huu, "Raphael Dwamena" alipoteza fahamu uwanjani katika ligi kuu ya Albania.
Kuna wakati watu wake wa karibu waliwahi kumwambia. Angeacha tu kucheza kwa usalama wa afya yake. Yeye aliwajibu hivi.
"Kama siku itatokea nimefia uwanjani hayo yatakuwa mapenzi ya MUNGU. Mimi siwezi kufanya shughuli yoyote zaidi ya kucheza mpira."
Sababu ya mapenzi na mpira. Raphael Dwamena aliamua kuuweka rehani uhai wake.
Tangu 2017 alipokataa kufuata ushauri wa madaktari. Ndipo kifo kilianza kuiwinda roho ya Raphael Dwamena. Jumamosi ya November 11 akaingia kwenye kumi nane za mauti.
Alianguka uwanjani akiwa peke yake. Mashabiki walijua Raphael amelala. Ila hawakujua ni usingizi wa mauti hivyo hataamka tena.
"Raphael Dwamena" alizaliwa Ghana
12 september 1995. Mauti ilipoliondoa jina lake katika orodha ya wanadamu walio hai. Ilikuwa jumamosi ya 11 November 2023. Akiwa na umri wa miaka 28. Mungu ampe pumziko la milele.
#mpekeo_mtandala
0 Comments