Eneo jipya lenye hazina kubwa ya nguzo za asili (Natural Pillars) zilizosimama mithili ya uyoga na kusemekana zimetokana na kumomonyoka kwa miamba yenye sifa tofauti na zenye muonekano wa kuvutia limegunduliwa nchini ambalo lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), nguzo hizo zilizosimama zinatajwa kuwa zimetokana na kumomonyoka kwa miamba yenye sifa tofauti kunakosababishwa na mwenendo mzima wa mtiririko wa maji na wakati mwingine pia zikichagizwa na upepo.
Akizungumza Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godwell Meing’ataki, amesema "Kwa mara ya kwanza tukiwa tunashuka na Helikopta katika eneo hili, tulishangazwa na wingi wa nguzo hizi za asili (Natural Pillars) na tukajua ndio hazina pekee iliyopo hapo, lakini tulipolizunguka eneo hili tuligundua lina utajiri mwingine wa masalia ya zana za mawe mithili ya zile zilizotumika nyakati za zama za mawe za mwanzo".
Zana zinazoonekana katika eneo hilo jipya ni pamoja na mawe magumu yaliyotumiwa na binadamu wa mwanzo kwenye kusagia nafaka kwa ajili ya chakula au mizizi na magome ya miti kwa ajili ya tiba asilia, miamba iliyochongwa kiustadi mithili ya mikuki, mashoka na zana nyingine zilizotumika katika shughuli za uwindaji.
Jitihada za kulitangaza eneo hilo zimeanza ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ili kuvutia watalii wengi zaidi na wawekezaji.
Eneo hilo limegunduliwa na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na kupewa jina la "Ruaha Magic Site" tofauti na hapo awali lilikuwa likijulikana kama "Magda", "Ruaha Magic Site" inasadifu zana nzima ya utalii.
0 Comments