Na. ZUENA MSUYA -Afrinews Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na Timu ya Serikali ya Majadiliano kuhusu mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (GNT) ili kufahamu hatua zilizofikiwa kuhusu majadiliano hayo.
Dkt. Biteko amekutana na timu hiyo Septemba 9, 2023 katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza timu hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi hatua iliyofikiwa mpaka sasa.
Katika kikao hicho Dkt. Biteko ameielekeza GNT kukutana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikiali, inayoshughulika na mikataba ili kuwaeleza kwa kina maendeleo na hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Dkt. Ameitaka timu kuwa huru katika kupokea mawazo ya kila mmoja katika kujenga uelewa wa pamoja .
Ametaka timu hiyo kuongeza kasi ili kukamilisha majadiliano hayo ili mradi huo uanze kutekelezwa kwa kuwa wananchi wanausubiri kwa hamu kubwa kutokana na umuhimu wake kwao na Taifa kwa ujumla.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, Musa Makame na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Petrol Lyatuu na viongozi wengine kutoka Wizara ya Nishati.
Timu ya Serikali ya Majadiliano kuhusu Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (GNT), wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, wakati wa kikao chake na timu hiyo kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Nishati, Jijini Dodoma, Septemba 9, 2023.
0 Comments