Ticker

7/recent/ticker-posts

KOCHA STARS AWANYAMAZISHA WAKOSOAJI WAKE,RAIS SAMIA APONGEZA

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche jana  amewanyamazisha wakosoaji wake ndani ya dakika 90 nchini Algeria.

Kocha huyo raia wa Algeria kabla ya mchezo wake dhidi ya timu ya taifa ya Algeria, alikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka nchini wakiponda uteuzi wake wa kikosi cha timu hiyo.

Waliokuwa wakimkosoa walisimamia kwenye uamuzi wake wa kumuweka kando kiungo Feisal Salum- Fei Toto, walinzi Shomari Kapombe na Mohamed Hussein.

Hata hivyo Amrouche hakuwahi kujibu ukosoaji huo kwa maneno, badala yake alitaka kuwaonesha matendo zaidi ndani ya uwanja kama alivyofanya Algeria.

Akidhihirisha kuwa hajafanya uteuzi wa kikosi chake ili kuwafurahisha wakosoaji wake, kocha huyo aliingia na mbinu ngumu ya kulinda zaidi  iliyowashangaza hata wapinzani wake.

Nia ya Amrouche ilikuwa ni moja tu, kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na alama muhimu kwenye mchezo huo.


Katika kulifanikisha hilo Amrouche aliingiza vijana wa kazi wenye uwezo wa kukaba na kushambulia kwa kushtukiza, mbinu ambayo iliwapa tabu Algeria ambao uwezo wao kisoka ni mkubwa mara dufu ya Taifa Stars.

Wachezaji wa Algeria waliutawala mchezo kwa dakika zote 90, lakini walishindwa kuipenya ngome imara ya Taifa Stars na hatimae kumaliza mchezo bila kufungana.

Matokeo hayo yameifanya Taifa Stars kuandika historia nyengine ya kufuzu mashindano ya AfCON  2033, ambayo yatafanyika nchini Ivory Coast.

Stars imefuzu kwa kupata alama 8 katika michezo 6 iliyocheza ya  kundi F, lililokuwa na timu za Algeria waliomaliza na alma 16, Uganda waliomaliaza na alama 7 na Niger waliomaliza na alama 2.

Mwaka 2019  Stars iliweka rekodi ya kufuzu michuano hiyo baada ya miaka zaidi ya 30.

Hatua hiyo ya Stars, imepongezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Post a Comment

0 Comments