Afisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambaye pia ni Msimamizi wa Utalii Huduma za Biashara, Kanda ya Dar es Salaam, Weja Lugendo |
Uhaba wa utafiti
wa soko unatajwa kuwa moja ya vikwazo vikubwa katika sekta ya utalii nchini haswa
katika kukabiliana
na ushindani kibiashara.
Hayo
yameelezwa na Afisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA)
ambaye pia ni Msimamizi wa Utalii Huduma za Biashara, Kanda ya Dar es Salaam, Weja Lugendo, wakati wa kujadili masuala ya uhifadhi wa bioanuai.
Mjadala huo uliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa Tuhifadhi Maliasili.
Lugendo amesema kuwa kutokuwepo
kwa utafiti wa kutosha ni moja ya changamoto kubwa kwani ni vigumu kufahamu soko la biashara ya utalii nje na ndani linataka nini lakini pia
kunapelekea
shughuli za utalii kushindwa kufanya vizuri katika ngazi tofauti.
“Kiukweli
utafiti wa soko ni eneo lenye changamoto, ukiangalia Tanzania kwenye hizi
taasisi zetu hatufanyi tafiti za kupata kujua masuala kama fursa za uwekezaji
kwa maana ya wapi tukawekeze na mengineyo lakini pia kuzifahamu changamoto
zilizopo ambazo zikibainika kwa wakati ni rahisi kuzifanyia kazi na kuepusha
vikwazo katika sekta nzima ya utalii,” alisisitiza Lugendo
Pamoja na
hilo, alisema pia kuna changamoto ya serikali kutokuwa na fedha za kutosha kwa
ajili ya kuutangaza utalii, na wao kama sehemu ya serikali wanakwama katika
utekelezaji kwakua fedha za serikali zinaeleweka kuwa sio nyingi.
“Kingine ni
kwamba kuna vivutio vichache, hivyo kunahitajika kuwe na mwendelezo wa vivutio
ili wageni wakija wasiishie kuona wanyama tu bali kuwe na mambo mengine kama
vile ya utamaduni na mengineyo ambayo yatawafanya kuona vitu vipya kila mara
wanaporudi kutembelea maeneo yetu.”
Afisa huyo aliongeza
kuwa bado kuna changamoto katika miundombinu, ili kuwavutia wateja ni lazima
uwe mbunifu kwenye biashara yako na kufanya uboreshaji wa miundombinu ya
utalii kama vile hoteli, barabara, viwanja vya ndege na huduma pia za kitalii,
uboreshaji ambao utaisaidia sekta ya utalii kutimiza lengo lake la kufikisha
watalii milioni 5 na dola bilioni 6 ifikapo 2025.
Akizungumzia
mapambano dhidi ya ujangili, Msafiri Kasara ambaye ni
Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda maalum
ya Dar es Salaam, amesema bado wanaendelea kushinikiza matumizi ya
sheria juu ya udhibiti wa usafirishaji wa nyara zinazongia na kutoka nchini lakini
pia kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali, baadhi ya taasisi
zinazojihusisha na uhifadhi nchini pamoja na wananchi, yote haya ni hakikisha wanadumisha
ushirikiano na kudhibiti ujangili.
Msafiri Kasara Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda maalum ya Dar es Salaam akisisitiza jambo wakati wa majadiliano |
“TAWA tunazielimisha jamii zinazozunguka maeneo ya uhifadhi juu ya faida za uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake, tumefikia mpaka hatua ya kutoa gawio kwa vijiji ambavyo vipo katika maeneo ambayo watalii wanawinda, tunawapatia asilimia 25 ya pato linalopatikana katika pori husika kila mwaka. Lakini pia tunajenga shule, watoto wanasomeshwa katika yale maeneo, wanapelekwa kwenye vyuo vya uhifadhi na huduma nyingine nyingi,” alisema Kasara
Aliongeza kuwa, “Kufanya hivyo kunasaidia wananchi
kuthamini uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa ujumla lakini pia kutofanya
ujangili, na mpaka sasa tayari shilingi bilioni 37 zimetumika kwa ajili ya malipo
hayo,”
Akiwasilisha mada
inayohusu changamoto ya viumbe vamizi katika uhifadhi na maendeleo ya jamii,
Joseph Olila ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Sera za Usimamizi wa Maliasili katika
mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, amesema
kuwepo kwa viumbe vamizi kwenye uhifadhi kumekuwa
miongoni mwa sababu inayochagia kuathiri mazingira na kufifisha kasi ya
ongezeko la vivutio vya utalii nchini.
Olila
amesema viumbe vamizi vinahusisha aina ya mimea, wanyama au kiumbe chochote kile
kinapoingia sehemu kwa mara ya kwanza na kuleta uharibifu.
“Kimazingira
kiumbe vamizi kina tabia ya kuondoa viumbe vya asili na chenyewe kutawala eneo
husika jambo linalosababisha kuleta madhara ya uharibifu wa uoto wa
asili, hatua hii inaathiri viumbe vilivyopo.”
Washiriki wa mjadala juu ya masuala ya uhifadhi wa bioanuai |
Aidha amezitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kupoteza tamaduni, ufugaji, magonjwa kwa binadamu, kupoteza mali kama mazao na mifugo, kwenye biashara lakini pia kwa serikali kutumia fedha nyingi kudhibiti, kusimamia, kupunguza uzalishaji jambo ambalo husababisha kupanda kwa bei za vyakula na nyingine nyingi.
“Changamoto
ni nyingi ikiwemo ya Utalii ambao unaathirika sana, hii ni kwasababu viumbe
vamizi wanaposababisha uharibifu wa mazingira kwa kipindi kirefu, wanyama
wanapungua jambo ambalo linapunguza watalii kwani mazingira asili yanakuwa
yametoweka,” amesema Olila.
Adda Ngoya, Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano-USAID |
Olila aliongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo jitihada nyingi zinafanyika lakini pia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira iliandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na viumbe vamizi wa miaka 10 ambao umeanza mwaka 2019 hadi 2029.
Akiongelea
juu ya uwepo wa sera na sheria za uhifadhi, John Noronha ambaye ni Meneja
Ufuatiliaji kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili alisema sheria zipo na
zinasaidia lakini zina mapungufu jambo ambalo ni changamoto kwenye suala zima la
uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa ujumla.
“Sheria
zipo lakini bado kuna changamoto ya upungufu katika sheria hizo, hivyo basi ni
vyema serikali izipitie na kuziongeza mfano: ni suala la mtu aliyelima kwenye
kingo ya hifadhi, hafidiwi, vitu kama hivi na vingine vinapaswa kuangaliwa kwa
umakini,” amesema.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema kuwakutanisha pamoja waandishi
wa habari na wataalamu wa mazingira ni suala muhimu kwasababu ni njia sahihi
yakufanya majadiliano ya kina juu ya masuala ya bioanuai na uhifadhi kwa ujumla
lakini pia kujifunza ili kwa pamoja kuweza kupata kilichokusudiwa ikiwa ni
mwendelezo wa sehemu ya utekelezaji wa mradi wa USAID Tuhifadhi Malisasili.
Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru akifafanunua jambo wakati wa mjadala
“Mafunzo ya
bioanuai ni muhimu sana katika masuala yote ya uhifadhi wa mazingira, na kama
waandishi kazi yetu kubwa ni kuzishirikisha, kuzifundisha jamii juu ya umuhimu wake
lakini pia taarifa zetu tunazoziandaa zinachangia kuhakikisha kwamba sera, miongozo,
mikakati iliyopo ndani na nje ya nchi zinatekelezwa, wananchi wanazielewa na
wanazitekeleza lengo likiwa ni kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi katika
masuala yote ya uhifadhi wa bioanuai,” alisema Dkt. Otaru
|
0 Comments