Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Sera na Tafiti za Uchumi za BoT, Dkt. Suleiman Misango
Na Jimmy Kiango
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewatoa hofu Watanzania juu ya uhaba wa Dola ya Marekani sokoni na kueleza kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya fedha hiyo nah atua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Pamoja na BoT kuwaondolea hofu wananchi, lakini pia imesisitiza kuwa hakuna sababu yeyote kwa mwananchi kutumia dola ya Marekani kwenye manunuzi ya ndani na kuwataka kutumia shilingi ya Tanzania kufanya manunuzi yoyote halali.
Hayo yamesemwa jana Juni 6,2023 na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Sera na Tafiti za Uchumi za BoT, Dkt. Suleiman Misango kwenye semina iliyowahusisha baadhi ya wakurugenzi wa benki hiyo na wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini.
Dkt. Misango aliwaambia wahariri kuwa ni kweli kuna upungufu wa dola ya Marekani sokoni, lakini hadi sasa mwenendo wa uchumi na fedha za kigeni nchini ni wa kuridhisha na himilivu.
Alisema hali ya upungufu wa dola ya Marekani sokoni haujaikumba Tanzania tu, ni changamoto ambayo imeikumba dunia na sababu kubwa ni mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19, vita ya Urusi na Ukraini pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema mara baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa UVIKO 19, mwenendo wa uchumi duniani haukuwa wa kuridhisha na hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka 2022 baada ya kuibuka kwa vita ya Urusi na Ukrain.
Dkt.Misango amesema changamoto hizo pamoja na mabadiliko ya tabia nchi zimeathiri pa kubwa mwenendo wa uchumi wan chi mbalimbali duniani na Tanzania ikiwemo.
“Wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Corona, uchumi wa dunia ulisimama, nchini China uzalishaji ulishuka, baadhi ya shughuli zililazimika kufungwa mara kwa mara.
“Ikumbukwe kuwa China ni nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani n ani nchi ya kwanza kwa shughli za biashara, sasa inapopunguza shughuli zake za kiuchumi, ujue hata dunia itaathirika.”
Aidha vita ya Urusi na Ukrain nayo ilishusha kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji na kupungua kwa bidhaa kama mafuta, gesi, ngano na makaa yam awe.
“Urusi na Ukain wao wanazalisha theluthi moja ya ngano duniani, kupigana kwao maana yake kumeathiri ugavi wa bidhaa hiyo, Urusi inashika nafasi ya pili duniani kwa kuzalisha gesi asilia ya tatu kwa kuzalisha mafuta na inazalisha asilimia sita ya makaa yam awe.
“Ukrain inazalisha kwa wingi mafuta ya kula na mahindi, mapigano yao yamesababisha bei ya bidhaa hizo kuongezeka kwenye soko la dunia.”
Baada ya changamoto hizo, benki kuu za nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani zilibadilisha mwelekeo wa sera ya fedha kwa kupandisha riba kwa lengo la kupunguza ukwasi katika uchumi.
Iliongeza riba kwenye mikopo na shughuli zake za kibenki kwa asilimia 500 kutoka asilimia 0.75 hadi 5.25.
Hatua hiyo ya ongezeko la riba imewavutia wafanyabiashara nan chi nyingi zenye uchumi mkubwa kukimbiza mitaji yao Marekani na kuathiri mataifa mengi yanayoendelea.
“Ongezeko la riba kwenye soko la fedha la Marekani linazinyima uwezo wa kukopa nchi zinazoendelea pamoja na kuuondoa mzunguko wa dola kwenye nchi hizo.
Ongezeko la riba limeziathiri nchi nyingi, Tanzania ikiwemo ambapo sasa gharama za uagizaji bidhaa kwa dola ya Marekani zimeongezeka na kupunguza akiba ya fedha za kigeni.
Hata hivyo Dkt.Misango amesema Tanzania bado ina akiba ya kutosha ya Dola za Marekani, ambazo zinaweza kutumika kwa miezi minne.
“Ni kweli kuna upungufu wa fedha za kigeni, lakini bado ni himilivu, akiba ya fedha za kigeni hapa Benki Kuu ni ya kuridhisha tunacho kiasi cha Dola za Marekani bilioni 4.9 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nyengine kwa zaidi ya miezi minne.
“Tuko vizuri ukilinganisha na nchi nyengine tunazolingana nazo. Sisi hatuko kwenye hali mbaya na fedha hizo tunazitumia kwa uangalifu.”
Aidha amesema katika kusaidia upungufu wa dola ya Marekani sokoni BoT imekuwa ikiuza kiasi cha dola milioni mbili kila siku.
Dkt. Misango amesema wana uhakika hali ya upatikanaji wa dola inazidi kuimarika kwani bei za bidhaa katika soko la dunia zinapungua hasa bei ya mafuta inazidi kushuka.
“Mwezi Julai na Septemba ni msimu wa utalii, lakini pia ni msimu wa mauzo ya mazao ya biashara kama vile katani, tumbaku, pamba na biashaa nyingine za asili.
Dkt. Misango alisema pamoja na kuwa na uhakika wa uhaba wad ola kupungua, lakini bado BoT imekuwa ikichukua tahadhari zaidi ya kujiimarisha kwa kununua dhahabu yenye thamani yad ola milioni 280 kwa mwaka saw ana tani sita, lengo likiwa ni kukuza akiba ya fedha za kigeni.
Aidha Benki Kuu imenunua kilo 418 kutoka kwa serikali, kupata fedha za kigeni kutoka kwenye benki za ndani na nje ya nchi kwa mfumo wa currency swap.
Pia Benki Kuu inauza akiba ya fedha ya Zambia (Kwacha) zilizopo kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania iliyopo Benki ya Kuu ya Zambia.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Misango alitoa rai kwa wananchi wa Tanzania kuacha kufanya malipo halali ya ndani ya nchi kwa kutumia dola za Marekani na badala yake wafanye malipo hayo kwa Shilingi ya Tanzania.
Alisema mtu yeyote akilazimishwa kufanya malipo halali ndani ya Tanzania kwa Dola ya Marekani atoe taarifa haraka ili ashughulikiwe.
0 Comments