Ticker

7/recent/ticker-posts

VITENDO VYA KUJERUHI TEMBO MVOMERO TISHIO, DC AKEMEA

Badala ya ujangili sasa limeibuka TISHIO jipya dhidi ya Tembo ambapo Baadhi ya wananchi wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, huwajeruhi.

Hali hiyo imemkera Mkuu wa Wilaya hiyo, Judith Nguli ambae amekemea vikali tabia hiyo ya wananchi na kuweka wazi kuwa vitendo hivyo huamsha hasira kwa wanyama hao na hatimaye kuwaletea madhara kwenye makazi yao.

Nguli ameyasema hayo jana Mei 19, 2023 wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro katika warsha ya kujadili utatuzi wa  changamoto ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu inayoikabili Wilaya hiyo, warsha hiyo  iliratibiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)

"Nimepata taarifa kwamba Kuna watu wanachokoza wanyama, mtu anajeruhi tembo,  ukishamjeruhi tayari anakuwa na hasira lazima asumbue hicho Kijiji kwasababu ana maumivu," amesema

"Nimepata taarifa Kuna baadhi ya tembo wanakutwa wakiwa na madonda, hata wakimkamata wanakuta tayari anavuja usaha, sasa tembo wa namna hii haiwezi kuwa rahisi kumzuia lazima atakufanyia fujo kwasababu ana maumivu," ameongeza

Nguli amekemea pia vitendo vya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa hifadhi kama vile kilimo, jambo ambalo linasababisha tembo kuharibu mazao yao.

"Tunaona muache kulima  pembeni ya hifadhi, kulima kwenye maeneo hayo ni hatari mnyama akitoka tu anakumbana na hilo shamba, lazima aliathiri kwasababu mnyama ni mnyama tu hana akili za kujua hili ni shamba nilikwepe."

Kwa Upande wake Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mlage Kabange amesema tathmini iliyofanywa na TAWA katika maeneo mbalimbali nchini imebaini kuwa watu wengi wanaopata madhara yanayotokana na wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo yanatokea wakati wa alfajiri na usiku, hivyo ametoa rai kwa wananchi kuepuka kufanya matembezi yasiyo ya lazima nyakati za usiku na alfajiri.

Kabange amesema katika Kukabiliana na changamoto hiyo, TAWA imejenga kituo cha askari kwa ajili ya muitikio wa haraka Ili kuweza  kuwadhibiti wanyama wakali na waharibifu kilichopo katika Kijiji cha Sangasanga na amewaomba viongozi wa Kijiji kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza wananchi kukutumia kituo hicho kwa kutoa taarifa za matukio ya uvamizi wa wanyama hao


Naye mbunge wa Jimbo la Mvomero, Jonas Van Zeland ameziomba mamlaka zinazohusika na wanyamapori hususan TAWA kuwavuna tembo  kwa lengo la kuwapunguza ili kuwapunguzia wananchi adha wanayokumbana nayo.

Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambapo ilihusisha viongozi mbalimbali katika Wilaya hiyo wakiwemo Mkuu wa Wilaya, madiwani wa kata, wenyeviti na watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wawakilishi wa Wazee Wote kutoka katika Wilaya ya Mvomero

Mawasilisho mbalimbali yaliwasilishwa kwa lengo la kuwapatia elimu viongozi hao 

Mojawapo ya mawasilisho hayo ni njia rafiki za kupambana na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, utaratibu wa kifuta jasho kwa wananchi, mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Post a Comment

0 Comments