Kikao cha 22 cha Watu wa Asili cha Umoja wa Mataifa kinaendelea jijini New York, Marekani kuanzia tarehe 17 Aprili hadi 28 Aprili, 2023.
Kikao hicho kimeelezwa na ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Prof. Hamisi Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Tifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Tanzania haina watu wa asili.
Akisoma taarifa hiyo Bi.Zuleikha Tambwe, Afisa Mwandamizi wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ameeleza kuwa Tanzania iliwahi kuwa koloni la Wajerumani 1891 hadi 1919 na baadaye Waingereza 1919 hadi 1961 na ilipata uhuru wake mwaka 1961.
Amebainisha kuwa Tanzania inayo makabila zaidi ya 120, ambayo yamekuwa yakiishi katika eneo ambalo kwa sasa linajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 5,000 iliyopita.
Makabila yaliyopo nchini Tanzania yalihamia kutoka katika makundi ya Kushi na Khoisan.
Kundi la kwanza kuingia Tanzania ni la makabila ya Wabantu ambao walihamia nchini zaidi ya miaka 3,000 iliyopita.
Makabila ya jamii ya Nilotic wakiwemo Waamasai walikuja baadaye na kuendelea kuwasili Tanzania kuanzia karne ya 18.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaundwa na makabila zaidi ya 120, ambayo yanaunganishwa na utamaduni, urithi wa pamoja, maadili na desturi pamoja na lugha ya Kiswahili ambayo kwa sasa inaendelea kusambaa duniani kote.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezea masikitiko na madai yanayotolewa na watu wanaodai ni Waamasai wakijitambulisha kuwa wao ni watu wa asili zaidi kuliko makabila mengine ya Tanzania.
Madai haya ni juhudi za makusudi za kuharibu umoja na mafanikio ya ujenzi wa Taifa la Tanzania.
Madai haya hayana nia njema na yanakinzana na maslahi ya Tanzania na watu wake.
Bi. Tambwe aliueleza mkutano huo kuwa Tanzania imelazimika kutoa ufafanuzi huu kutokana na tuhuma ovu na zilizoenea zinazotolewa dhidi ya Tanzania, na watu na Asasi zisizo za kiserikali ambao wameamua kupuuza juhudi za Tanzania za kujenga jamii ya watu walio sawa na huru.
Ujembe wa Tanzania umeueleza mkutano huo kuwa inavunja moyo kuona kongamano la muhimu kama hili likigeuzwa kuwa jukwaa la shutuma dhidi ya Tanzania kwa kutumia madai ambayo hayana ukweli wala uhalisia.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasistiza kuwa makabila yote ya Tanzania yako sawa na hakuna kabila ambalo wao ni wa asili kuliko Watanzania wengine.
Naye mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho, Prof. Hamisi Malebo, wakati akiongea na Mwandishi Maalumu (Special Rapporteur) wa Jukwaa la Watu wa Asili Bw. Calà Tzay kutoka Guatemala, alimkumbusha juu ya juhudi ambazo Serikali ya Tanzania imekuwa ikizifanya kushughulikia malalamiko ya watu wa jamii ya Waamasai.
Prof. Malebo alibainisha kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, alifanya kikao naye kwa njia ya mtandao na kutoa ufafanuzi wa masuala ya Loliondo na Ngorongoro ambapo alimtaarifu kuwa hakuna Watanzania ambao kabila lao ni la asili zaidi kuliko makabila mengine.
Prof. Malebo pia alimkumbusha kuzingatia mwaliko wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kumtaka atembelee Tanzania ili ajionee hali ilivyo.
0 Comments