NA JIMMY KIANGO
KWA miaka mingi wakazi wa mji wa Kigambani wamekuwa wakilazimika kuvuka maji ili kwenda katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kusaka huduma bora za afya.
Hatua hiyo ilisukumwa na kukosekana kwa Hospitali yenye hadhi na kiwango cha mkoa kama ilivyokuwa kwenye maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam.
Kwa kuligundua hilo, timu ya wataalamu na watafiti, waliamua kuingia mtaani ili kuangalia ni namna gani watawasaidia wakazi wa Kigamboni ambayo sasa ni wilaya.
Kwa weledi wa hali ya juu, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ukiwemo wa Figo, Egina Makwabe aliliona eneo la Mji mwema Kigamboni kuwa sehemu sahihi ya kuwepelekea huduma ya matibabu bora wakazi wa Kigamboni.
Baada ya kujiridhisha, haraka ujenzi wa hospitali ya kisasa ulianza mwaka 2019, ambapo ujenzi ulisimama mwaka 2020 kutokana na kuibuka kwa wimbi la Corona, ujenzi uliendelea mwaka 2022 na kukamilika mwaka huu, ambapo Machi 27, hospitali ya E.M ilianza kutoa huduma.
Kwanini Mji mwema? Dkt. Makwabe anasema wataalamu wake waliona eneo hilo linafaa kutokana na urahisi wa kufikika.
“Unaweza kufika hapa kwa urahisi kwa namna yoyote na kwa mtu yeyote yule bila kujali anatokea wapi.
“Hospitali ya E.M iko barabarani kabisa, kunafikika katika kipindi chote cha mwaka bila kujali kuna mvua ama kuna jua, mwananchi anaweza kupitia njia ya darajani ama kutumia kivuko.
“kote huko ni mwendo usiozidi dakika 15, unakuwa umefika E.M Hospital na unapatiwa huduma stahiki kwa haraka.”
Jimmy Kiango (kushoto) akizungumza na Dkt. Makwabe |
DHAMIRA YA KUTOA HUDUMA BORA
Tayari timu ya watoa huduma za afya kutoka Hospitali ya E.M,imejipanga na imedhamiria kutoa huduma bora na za kisasa kwa watu wengi.
Dkt. Makwabe ameuthibitishia mtandao wa Afrinews Swahili ambao ulitembelea hospitali hiyo kuwa kuanzishwa kwa hospitali hiyo ya kwanza ya binafsi kwa ngazi ya mkoa ndani ya wilaya ya Kigamboni ni namna mojawapo ya kutoa suluhu ya changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
“Tumechagua kuleta huduma bora na za kisasa Kigamboni na Dar es salaam kwa ujumla, kwa sababu nia yetu ni kuhakikisha huduma zetu zinatolewa kwa weledi mkubwa, tulifanya uchunguzi na tukagundua wilaya hii inahitaji huduma za afya za kibingwa.
“Tuligundua kuwa hakukuwa na hospitali yoyote ya binafsi ya ngazi ya mkoa na wagonjwa walikuwa wanalazimika kwenda mbali na Kigamboni kufuata huduma za matibabu,” alisema Dkt. Makwabe.
Vyumba vyenye mashine ya kufanya usafishaji wa damu, DialysisiYAPI MALENGO YA HOSPITALI YA E.M
Lengo kubwa ni kuhakikisha wanawafikia watu wengi na kwa wakati, huku wakizingatia kuwa dunia ya sasa imebadilika kwenye vifaa vya kisasa na teknolojia za hali ya juu, mabadiliko hayo yanawafanya na wao kuhakikisha wanakwenda na kasi hiyo.
“Pamoja na kuwekeza fedha nyingi hapa, lakini sisi ni watoa huduma, moja ya malengo yetu ni kuhakikisha tunakuwa na tija kwa watu waliotuzunguka bila kujali uwezo wao.
“Tunajipanga ili kuona njia sahihi ya kusaidiana na wananchi waliotuzunguka, hatutaacha kumtibu mtu kwa sababu hana uwezo, kama unaweka hospitali kama hii na umezungukwa na watu ambao hawana uwezo wa kuzipata huduma zako haitaleta maana kwao,” alisisitiza Dkt. Makwabe
Alisema ili kufanikisha utaratibu wa kutoa huduma hata kwa wasio na uwezo wanatarajia kuanzisha mfuko ambao utabeba gharama za kuwachangia wasio na uwezo.
UHAKIKA WA KUHUDUMIWA MUDA WOTE
Pamoja na changamoto za kukosekana kwa madaktari bingwa nchini, hospitali ya EM imejipanga kwenye eneo hilo kwani inao wataalamu wa kutosha.
“Katika hospitali nyingi za serikali na binafsi hapa nchini kuna changamoto za madaktari bingwa, lakini kwetu hali ni tofauti, tunao madaktari bingwa 13, kati yao wapo madaktari wa watoto, wakina mama, daktari wa magonjwa ya ndani, figo na upasuaji wa aina zote.”
Dkt. Makwabe ameweka wazi kuwa hospitali yake imejipanga vilivyo kutoa huduma zote za kibingwa na zisizo za kibingwa zikiwemo huduma za kusafisha damu, huduma za X-Ray, CT-Scan, maabara kubwa, duka kubwa la dawa, matibabu ya meno, macho, masikio, koo, huduma za upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za kulaza, kuhudumia wagonjwa wa nje, matibabu ya mapafu, vidonda vya tumbo, magonjwa ya ngozi pamoja na huduma za wakina mama na watoto.
SHUKURANI KWA SERIKALI
Dk Makwabe ameishukuru Serikali kwa ushirikiano alioupata kuanzia hatua ya kwanza hadi walipofikia sasa na anaamini ushirikiano huo mzuri utaendelea.
Hata hivyo aliiomba Serikali kupunguza baadhi ya changamoto hasa ya ucheleweshaji wa usajili wa vituo.
“Ni vyema Serikali ikarahisisha zoezi la usajili wa vituo binafsi, vituo vikiwa vimeshakamilika kabisa serikali kupitia vyombo vyake husika ifanye usajili mapema, watu waweze kuendelea na kazi, kukawia kusajili kunawagharimu sana wawekezaji kwasababu muda ambao wanasubiri usajili wao wanakuwa tayari wameshaweka wafanyakazi ambao wanalipwa mishahara bila kuzalisha chochote.
Inaumiza sana, kituo kikiwa kimekamilika na kinamaliza miezi sita au mwaka hakijasajiliwa ni tatizo kubwa kweli kweli,” aliongeza Dkt. Makwabe
USHIRIKIANO WA VITENDO
Dkt. Makwabe ameomba kuwe na ushirikiano wa vitendo kati ya serikali na sekta binafsi, kama vile kubadilishana wagonjwa hasa katika maeneo ambayo hospitali binafsi hazina uwezo wa kuwahudumia au hospotali za serikali hazina uwezo, ni vema kukawa na utamaduni wa kushirikiana kivitendo.
“Kama katika hospitali hii hakupatikani huduma fulani basi waweze kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali za serikali ili watibiwe bila kupata kikwazo chochote na walioshindikana katika hospitali za serikali waelekezwe kwenye hospitali binafsi bila vikwazo.”
“Ikumbukwe tu kuwa sekta binafsi inavyowekeza kwenye afya inaipunguzia serikali mzigo mkubwa, hivyo kuwe kuna namna ya kusaidiana katika matumizi ya vifaa tiba kama vile mashine za MRI na nyinginezo, badala ya kupatikana mashine nne kwenye eneo dogo ni vema zikatawanywa katika maeneo mbalimbali, lakini hili litafanikiwa kama kutakuwa na ushirikiano wa kitabibu kati ya serikali na Sekta binafsi,” alisema Dkt. Makwabe
E.M HOSPITAL YAKUBALIKA“Ninashukuru kuwa watu wameipokea huduma vizuri na tuko katika hatua za mwisho kukamilisha suala la matumizi ya bima za afya, tunaamini kuwa hii itatupa nafasi ya kuwahudumia watu wengi zaidi, kila kitu kitakuwa sawa ndani ya muda mfupi na huduma zitaendelea kutolewa kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia taratibu zote muhimu za utoaji wa huduma za afya nchini,” alisema Dkt. Makwabe.
Afrinews Swahili iliongea na baadhi ya wakazi wa Kigamboni juu ya ujio wa Hospitali hiyo, ambao wamefurahia na kusema kuwa wanaamini watapunguza safari za kwenda nje ya Kigamboni kusaka huduma za afya.
Mzee Tulius Sambega alisema amefurahia kupata habari za ujio wa hospitali hiyo,ingawa hajapata nafasi ya kwenda hospitalini hapo, lakini taarifa zilizomfikia zinaonesha ni hospitali bora na itakuwa msaada mkubwa kwao.
Hata hivyo aliwataka waendeshaji wa hospitali hiyo kutobadilika haps baadae. "Nimefurahi sana, ila nawaomba wasibadilike maana tumeshuhudia hospitali nyingi zikianza zinakuwa bora, lakini baadae zinabadilika na kuanza kutoa huduma mbaya."
0 Comments