Ticker

7/recent/ticker-posts

MATOKEO YA WANAFUNZI WA SHERIA BADO NI MABAYA



Pamoja na Kamati ya Dkt. Harrison Mwakyembe kufanya kazi yake juu ya matokeo mabaya ya shule ya Sheria, hali bado ni mbaya.

Tayari matokeo ya kundi la 34, lililohusisha wanafunzi 826 yametoka yakiwa hayaridhishi.

Kati ya wanafunzi hao 826 waliofanya mtihani huo kwenye mkao wa kwanza, waliofanya vizuri ni 23, wanaopaswa kurudia baadhi ya mitihani ni 487 na walioanguka ni 316.

Oktoba 12, mwaka jana Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Damass Ndumbaro aliunda kamati iliyoongozwa na Dkt. Harisson Mwakyembe na kutakiwa kutafuta chanzo cha kufeli wanafunzi wengi katika mitihani ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo (LST).


Kamati hiyo ilifanya kazi yake na Novemba 20,mwaka jana iliwasilisha mapendekezo yake.

 Miongoni mwa mambo ambayo kamati hiyo ilipendekeza ni kuanzishwa kwa  mtihani maalumu wa kuingia LST kama ilivyo katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe saba na iliundwa baada ya malalamiko na kelele za wanafunzi na wananchi.

Matokeo yaliyosababisha kuundwa kwa kamati hiyo yalionyesha kuwa kati ya wanafunzi 633 waliofanya mtihani huo, 26 pekee ndio waliofaulu katika mkao wa kwanza, huku 342 wakifaulu baadhi ya masomo na wana fursa ya kurudia masomo. Wanafunzi 265 walifeli mtihani mzima, ingawa wanaweza kuanza upya.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema changamoto hizo pia zimelalamikiwa na LST pamoja na wadau mbalimbali wa sheria.








Post a Comment

0 Comments