Ticker

7/recent/ticker-posts

WANANCHI KANDA YA ZIWA WATOA AHADI NZITO KWA TAWA, WAFURAHISHWA NA UTENDAJI WAO

 

Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja (wa tano kutoka kulia) akiwasikiliza wananchi waliokuwa wakitoa maelezo yao juu ya changamoto ya Wanyamapori wakali.

NA MWANDISHI WETU

Kazi inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -TAWA, katika kuuelimisha umma juu ya kukabiliana na Wanyamapori wakali wanaoingia kwenye maeneo ya makazi ya watu imewakuna wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa na kuahidi kushirikiana na Serikali katika kushughulikia changamoto hiyo.

 

Baadhi ya wananchi wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza wakizungumza na Waandishi wa Habari katika ziara iliyofanywa na TAWA kwenye mikoa hiyo wameelezea  adha  kubwa wanayoipata kutokana na changamoto itokanayo na wanyamapori  hao kiasi cha kuhatarisha maisha yao na kudhoofisha shughuli za kiuchumi.

 

Kufuatia jitihada za TAWA za kuwaondolea kadhia hiyo, wananchi hao wameipongeza TAWA kwa hatua hiyo ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha katika zoezi zima la kukabiliana na changamoto hiyo.

 

"Kumekuwa na malalamiko makubwa kutokana na wimbi la wanyamapori hatarishi hususani fisi na wengine ambao wamekuwa wakishambulia watu.

 


“Watoto wanashindwa  kwenda shule, jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa, lakini ujio wa taasisi hii ya TAWA umekuwa ni faraja kubwa kwetu maana imekuja kwa ajili ya kushirikiana na wananchi ili kukabiliana na changamoto hii ya wanyamapori,..na mimi niseme, sisi wananchi tuko tayari kushirikiana na taasisi hii kwa sababu usalama ni wa kwetu na taasisi hii imekuja na huu mpango kwa ajili ya kutuweka salama, kwahiyo sisi wananchi tunaahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori hao,” " amesema Leonard Mayala mkazi wa Kahama.

 

Kwa upande Robert Wilson mkazi wa wilaya ya Misungwi Kata ya Mbarika ambaye pia  ni Mwenyekiti wa kikundi cha Wagalu ameeleza kufurahishwa kwake na adhma ya Serikali kupitia TAWA ya kuwashirikisha wananchi katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika mapambano hayo ili jamii iwe na salama.

 

Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amewapongeza wananchi hao kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo na kusema kuwa ushirikiano huo unatoa mwelekeo mzuri katika kutatua changamoto inayowakabili wananchi hao.

 


Katika kusisitiza hilo, amesema kutokana na ukubwa wa nchi yetu na upungufu wa rasilimali ni dhahiri kuwa TAWA peke yake haitaweza kuwepo kila mahali, hivyo ushiriki wa wananchi katika uhifadhi na mapambano dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu ni muhimu katika kufikia malengo mapana ya uhifadhi wa wanyamapori nchini, hivyo TAWA inathamini maamuzi yaliyofanywa na wananchi hao.

 

Aidha ametoa rai kwa watanzania wote kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikizingatiwa kuwa jukumu la kulinda raia na mali zao ni la wananchi wote.

 

Karika siku za karibuni kumekuwa na tishio la kuwepo kwa wanyamapori wakali hasa mamba na viboko kwenye maeneo mbalimbali ya nchini kutokana na kuhamishwa kwenye maeneo yao asili na mafuriko yaliyotokana na kunyesha kwa mvua kubwa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.

 

 Katika kukabiliana na changamoto hiyo TAWA imekuwa ikitoa elimu ya namna ya kukabiliana na kujiepusha na madhara yanayoweza kutsababishwa na wanyama hao  kwenye mikoa mbalimbali hasa kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi, mito na maziwa.

 

 


Post a Comment

0 Comments