JIMMY KIANGO NA ELIAS SHADRACK
Moja ya vipaumbele vyake vitatu muhimu ni Elimu, Elimu na Elimu, aliamini elimu ndio kila kitu katika mafanikio ya Mtanzania.
Hakuona haya kuisemea elimu popote alipokuwa, hakusita kuifungamanisha elimu na mafanikio ya kifedha ambayo kwa lugha nyepesi ni utajiri.
Aliuchukia umasikini kwa maneno na vitendo, hakutaka kusikia kabisa kuwa umasikini ni haki ya Mtanzania, hakulipenda neno mnyonge kwa sababu aliamini neno hilo linahalalisha unyonyaji kwa mwananchi na kumfanya abweteke akiamini yeye ni mnyonge.
Katika kuhakikisha anaupiga vita umasikini kwa vitendo, yeye ndie aliamua kuasisi shule za Kata ili kila mtoto wa Mtanzania apate nafasi ya kusoma bila ubaguzi wala kikwazo cha umbali wa shule ama uhaba wa madarasa.
Huyu ndie Edward Ngoyai Lowassa, ambaye leo hii hana pumzi tena, hasemi, wala haoni chochote mbele ya uso wa dunia.
Edward ama Edo kama alivyoitwa na washakaji zake aliokuwa akicheka na kugonga nao bilauli sasa ni marehemu na kwa hadhi yake tunaweza kusema ni hayati.
Huwezi tena kumuita ama kuandika jina lake bila kutanguliza neno Hayati. Lowassa amekufa leo Februari 10,2024 akiwa kwenye kitanda cha hospitali akipigania uhai wake.
Ndio, ni kweli Lowassa amekufa na kifo chake kimetangazwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Lowassa rafiki mkubwa wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na mwanamtandao kindaki ndani ni moja ya alama za uwanja wa siasa Tanzania.
Historia yake kwenye siasa haitengani na historia ya siasa za vyama vingi nchini, ameanza harakati za kisiasa tangu angali kijana.
Amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu jijini Dar es Salaam kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Taarifa za kifo chake zimeshtua, ingawa amekuwa kimya kwa muda mrefu na hajaonekana hadharani kwa muda pia, lakini jina na matendo yake mema yamesalia mioyoni mwa Watanzania wengi.
Akitangaza kifo cha Lowassa, Dkt. Mpango amesema kuwa mwanasiasa huyo amefariki akiwa katika matibabu ya ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Inasikitisha, Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu kwenye taasisi hiyo na baadae kupelekwa nchini Afrika Kusini tangu Januari 14,2022.
Akisoma taarifa ya Rais Samia, Dkt. Mpango amesema, Tanzania imepoteza kiongozi mahiri, ambapo ili kuuthamini mchango wake Rais ametangaza siku tano za maombolezo na bendera zitapepea nusu mlingoti.
Pamoja na taarifa ya Dkt. Mpango lakini pia Rais Samia ametoa salamu za rambirambi kupitia mtandao wa (Twitter), na kuandika kuwa Lowassa ameitumikia Tanzania katika nafasi mbalimbali katika kipindi cha zaidi ya miaka 35.
“Tumepoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu,” ameandika Rais Samia.
HISTORIA FUPI YA LOWASSA
Edward Ngoyai Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Mondoli akiwa ni mtoto mkubwa wa kiume wa familia ya Mzee Ngoyai Lowassa.
Alianza kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi Monduli mwaka 1961-1967, aliendelea na shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati yam waka 1968-1971.
Aliendelea na elimu ya kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya Milambo iliyopo mkoani Tabora. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwa 1974 hadi mwaka 1977, ambako alihitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) baadae alikwenda nchini Uingereza kusoma Shahada ya uzamili ya Sayansi katika Maendeleo.
Baada ya kumaliza Chuo Kikuu, alifanya kazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ngazi ya afisa wa wilaya, mkoa na baadae makao makuu kati yam waka 1977 hadi 1989.
Aidha aliwahi kutumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambapo alishiriki kwenye vita kati ya Tanzania na Uganda, baadae alikabidhiwa jukumu la kukisimamia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) mwaka 1989-1990.
Baadae aliingia kwenye siasa moja kwa moja na kuchaguliwa kuwa mbunge kupitia kundi la vijana ndani ya CCM kwa miaka mitano kutoka 1990-1995, ambapo akiwa mbunge kijana mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge).
Baadae alihamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi, mwaka 1995 katika kipindi ambacho nchi iliingia kwenye uchaguzi wa vyama vingi Lowassa aliwania Ubunge wa Monduli, ambapo alishinda kwa asilimia 87.3.
Mwaka 1997 alirejeshwa tena kwenye Baraza la Mawaziri akihudumu katika nafasi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na kuondoa umasikini) hadi mwaka 2000.
Mwaka 2000 aligombea tena ubunge na kushinda, ambapo aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Mifugo hadi mwaka 2005.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 aliwania tena ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6 na hapo ndipo swahiba yake Jakaya Kikwete alipomteua kuwa Waziri Mkuu na Bunge lilimpitish kwa kura 312.
Akiwa Waziri Mkuu ndipo aliposimamia harakati zake za kuutokomeza umasikini kwa vitendo kwa kuanzisha shule za Kata zilizokuwa na lengo la kurahisisha upatikanaji wa elimu kwa kila mtoto.
Hata hivyo hakudumu kwenye nafasi hiyo kwani Februari 2008 alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond.
Mwaka 2010 aliwania tena ubunge kwa tiketi ya chama chake CCM, ambapo alichaguliwa kwa asilimia 90.93 ya kura zote.
Mwaka 2015 kipindi ambacho swahiba yake alikuwa akimaliza muhula wake wa pili wa urais, Lowassa alitumbukiza jina lake kwenye mbio za urais, hata hivyo jina lake lilikatwa na miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi aliamua kukimbilia Chadema, ambako alipewa nafasi ya kuwania urais.
Akiwa Chadema aliweza kuisumbua CCM ambayo kwa wakati huo ilikuwa imemsimamisha hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Lowassa aliungwa mkono na kundi kubwa la wanasiasa wa upinzani n ahata wale wa CCM.
Hata hivyo hakufanikiwa kushinda, mwaka 2019 Lowassa alirejea CCM na alipokelewa na Hayati Magufuli katika ofisi ndogo za CCM, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Lowassa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwenye elimu, kwani miongoni mwa jitihada zake kwenye eneo hilo ni kufanikisha upatikanaji wa fedha za kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mwamba wa Kaskazini, ameacha mke na watoto watano.
Apumzike kwa amani…
0 Comments