Ticker

7/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFUTA NA KUPUNGUZA TOZO 232

SERIKALI kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) imefuta na kupunguza jumla ya tozo, ada na faini zisizopungua 232 kati ya 380 zilizobainishwa katika utekelezaji wake sawa na asilimia 61.

Akizungumza Kikao Maalum cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, Dkt Jim James Yonazi alisema ufutwaji wa tozo, ada na faini hizo ambazo zilikuwa kero kubwa kwa ustawi, ukuaji na maendeleo ya biashara na uwekezaji hapa nchini.

“Maamuzi haya yanaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifungua Tanzania na kuwa kivutio cha kufanya biashara na uwekezaji,” alisema Dkt. Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi kazi hicho cha Baraza la Taifa la Biashara(TNBC).

Akielezea zaidi mafanikio yaliyopatikana tangu MKUMBI uanze kutekelezwa, Dkt. Yonazi alisema jumla ya Sheria, Kanuni na Taratibu zipatazo 40 kati ya 88 sawa na asilimia 45.5 zimeshapitiwa na kufanyiwa marekebisho.

“Maboresho haya yote ya Sheria,Kanuni na Taratibu yamesaidia kuchochea ukuaji wa sekta za uchumi hapa nchini zikiwemo sekta za uwekezaji, viwanda na biashara, kilimo, mifugo, afya, maliasili na utalii,” alisema.

Dkt. Yonazi alisema Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC ameelekeza kuendelea kusimamia utekelezaji stahiki wa MKUMBI sambamba na uhamasishaji wa matumizi ya mifumo yaTeknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini.

“Nina agiza Wakurugenzi na Idara za Uratibu, Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Maendeleo ya Sekta Binafsi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,wafuatilie utekelezaji wa Maazimio ya TNBC na kuwaandikia barua Makatibu Wakuu wote ambao bado hawajawakilisha taarifa za utekelezaji wa maazimio hayo,” alisisitiza Dkt. Yonazi.

Post a Comment

0 Comments