Ticker

7/recent/ticker-posts

BURIANI RASHIDI MBUGUNI MWANAMAPINDUZI HALISI WA SEKTA BINAFSI TANZANIA

MZALENDO ALIYEDHULUMIWA KIWANDA AMEKUFA HAJAONA HAKI

NAKUMBUKA mwaka 1999. Mara ya kwanza naingia chumba cha habari. Business Times Ltd (BTL).

Newsroom yenye hadhi. Nilivutiwa na chumba kikubwa cha wachoraji. Kizuri sana, kiliundwa kwa vioo. Kila kijana mwenye kipaji cha kuchora, alipaona nyumbani.

BTL, nyumba ya magazeti ya Business Times, Majira, Spoti Starehe, Sanifu, Dar Leo na Maisha. Mamia ya Watanzaia waliajiriwa direct. Maelfu indirect.

Kila kitu kilianza na fikra zilizoishi mbele ya muda, za wazalendo Richard Nyaulawa na Rashidi Mbuguni. Hatimaye, wote sasa ni marehemu.

Nyakati sekta binafsi ikitafsiriwa kuwa mtoto wa haramu, Nyaulawa na Mbuguni walithubutu na waliibeba kwa ujasiri na mawazo yenye ujazo mkubwa.

Kampuni yao, Business Care Limited (BCS), ikazaa BTL, iliyosajili na kuchapa gazeti la kwanza binafsi Tanzania, Business Times. Mwaka 1989.

Wakati wowote, historia ya vyombo vya habari binafsi Tanzania ikiandikwa, majina ya Nyaulawa na Mbuguni, yanastahili wino wa dhahabu.

Gazeti la Business Times, lilizaa Majira mwaka 1992. Baada ya hapo, magazeti zaidi ya kampuni binafsi yalizaliwa, kisha redio na televisheni. BTL ya Nyaulawa na Mbuguni, ilifungua njia.

Nyaulawa na Mbuguni, walianzisha kampuni ya uchapaji ya Business Printers Limited (BPL). Kiwanda cha BPL kilikuza mno tasnia ya habari.

BPL, haikuchapa magazeti ya BTL pekee, bali yote ya kampuni binafsi wakati huo. Vilevile vitabu, majarida na machapisho mbalimbali. Nyaulawa na Mbuguni ni wazazi na walezi wa kila gazeti lililozaliwa miaka ya 1990.

Uchaguzi Mkuu 1995, Nyaulawa na Mbuguni, waliandaa mdahalo wa kihistoria wa wagombea urais. Tukio hilo halijawahi kujirudia nchini.

Nyaulawa na Mbuguni ni Watanzania wa kwanza kuonesha kuwa sekta binafsi inaweza kushirikiana na Serikali, kutatua changamoto za wananchi.

Kupitia BCS, walianzisha miradi ya kushughulikia kero za maji, mikoa mbalimbali nchini. Baadaye, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida), Nyaulawa na Mbuguni, waliendesha Mpango wa Afya kupitia Maji Salama (Hesawa) kwa zaidi ya miaka 10.

Kupitia Hesawa, Nyaulawa na Mbuguni, waliwezesha Watanzania zaidi ya milioni tano wa vijijini, hususan Kanda ya Ziwa, kupata maji safi na salama.

Nyaulawa na Mbuguni, walijenga hamasa ya mtaji kwa Watanzania, na wakashawishi wachache kutoka nje, wakaanzisha Benki ya Biashara ya Akiba – Akiba Commercial Bank (ACB), mwaka 1997.

Desemba 1998, Nyaulawa na Mbuguni, walifanikisha kuileta Tanzania, taasisi ya kimataifa ya Junior Achievement Worldwide, yenye makao yake makuu, Colorado, Marekani.

Junior Achievement (AJ), hufundisha vijana elimu ya biashara na uwekezaji. Tangu kuwasili Tanzania, AJ imetengeneza maelfu ya vijana kuwa wafanyabiashara stadi.

Vicoba ni maarufu hivi sasa. Asili yake ni Vibindo. Nyaulawa na Mbuguni, walianzisha Vibindo mwaka 2002, kuwezesha Watanzania kuweka, kukopa na kusaidiana katika vikundi. Vibindo ndio sasa Vicoba.

Nyaulawa na Mbuguni ni waasisi wa Taasisi ya Utafiti na Kuondoa Umaskini (Repoa), ambayo tafiti zake zimekuwa mwanga kwa Serikali, Bunge na taasisi za kimataifa, katika kukabili umaskini Tanzania.

Mwaka 1990, Nyaulawa na Mbuguni, waliratibu mafunzo ya kilimo cha mwani (seaweed) kwa mara ya kwanza, kwa akina mama wa Zanzibar. Wataalamu hao walitoka Ufilipino.

Hivi sasa, mwani inashika nafasi ya tatu Tanzania kwa usafirishwaji nje ya nchi, ni namba tatu kwa mapato Zanzibar, na inachukua hadi asilimia 90 ya huduma za usafiri wa maji Zanzibar kwenda nje.

Nyaulawa na Mbuguni ndio waasisi wa biashara za kutembeza mkononi, yaani umachinga. Waliasisi hilo kupitia kuuza magazeti mikononi. Wakawa na mtandao wa vijana waliozunguka Dar es Salaam. Mtindo huo ukaitikiwa kwa ukubwa. Hivi sasa, mtindo huo umekuwa mtandao mpana wa ajira.

Kwa tafsiri yoyote, Nyaulawa na Mbuguni ni wazalendo wa nchi. Ni nuru ya sekta binafsi. Mageuzi ya ujamaa hadi uchumi wa soko, yana kurasa nyingi za Nyaulawa na Mbuguni. Bila swali, Nyaulawa na Mbuguni ni historia ya Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amewahi kunieleza kuwa partnership ya Nyaulawa na Mbuguni haina mfanowe Tanzania. Walifanya mengi kibiashara na kwa nchi, kwa upacha wa hali ya juu.

Mzalendo Nyaulawa alifariki dunia mwaka 2008, akamwacha Mzalendo Mbuguni, akiendeleza waliyoyaanzisha pamoja.

Mwaka 2016, BPL chini ya Mbuguni, ilichukua mkopo benki za NMB na ECO. Fedha hizo zilitumika kununua mitambo na kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kiwanda chake cha uchapaji. Kiwanda kikawa kipya kabisa.

Mwaka 2017, task force ya Rais wa Tano, Dk John Magufuli, ilivamia BPL. Wamiliki waliondolewa. Kiwanda kikawa chini ya usimamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kuanzia hapo, magazeti ya CCM, Uhuru, Mzalendo na Burudani, ya Serikali, Daily News, Sunday News na Habari Leo, kwa nyakati tofauti, yalichapwa bure BPL.

Magazeti mengine, Tanzanite, Fahari Yetu, La Jiji, Tanzania Perspective, The Echo, Observer na mengine mengi, yaliyoitwa ya kimkakati, yalichapwa bure BPL.

Kura za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020, zilichapwa BPL.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Business Printers Ltd (BPL), Marehemu Rashid Mbuguni (kushoto) alipomkabidhi aliyekuwa Meneja Mkuu wa BPL, Bibi Getrude Nyaulawa, cheti cha utumishi uliotukuka, baada ya kuitumikia kampuni kwa miaka 18

Wakati yote yakifanyika, Mbuguni na familia ya Nyaulawa, walipitishwa kwenye moto unaounguza. Mali zao, ikiwemo nyumba, kupigwa minada. Presha kubwa ya mikopo ya NMB na ECO.

Haitoshi, task force ya Magufuli, ilimtishia Mbuguni kumfungulia mashitaka ya uhujumu uchumi, vinginevyo alipe mamilioni kwa kushirikiana na familia ya Nyaulawa.

Kwa hofu ya kesi ya uhujumu uchumi, walikubali kulipa kwa awamu. Ajabu, wakaelekezwa kulipa benki kwenye akaunti ya mtu binafsi. Na wakalipa.

Nilimshuhudia Mbuguni akiwa kwenye mahangaiko, akipigania kiwanda chake. Panda shuka bila mafanikio.

Jana, Julai 15, 2023, Mzalendo Mbuguni, aliitikia wa wito wa mauti. Naam, kila nafsi itaonja mauti.

Mbuguni amefariki dunia akiwa bado anasotea haki yake. Kiwanda chake ambacho hakurudishiwa tangu kilipoporwa mwaka 2017.

Mtanzania aliyetenda mengi kwa nchi. Aliyebadili maisha ya maelfu kupitia mipango na ajira za moja kwa moja, nyakati za mwisho za uhai wake, zilijaa maumivu makali kwa sababu ya dhuluma. Amekufa maskini na mufilisi.

Kesho (Julai 17, 2023), Mzalendo Mbuguni atazikwa makaburi ya Kisutu. Sala ya maiti, itafanyika Msikiti wa Maamur, Upanga, Dar es Salaam.

Sisi Sote ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake Tutarejea.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments