Ticker

7/recent/ticker-posts

WADAU WA MISITU WAFURAHISHWA NA KASI YA MABADILIKO NDANI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Wadau sekta ya wanyamapori na misitu waona mwanga utendaji Wizara ya Maliasili, wampongeza Rais Samia

Na John Mapepele

Wadau wa Sekta za Wanyamapori na Misitu nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanywa hivi sasa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii hususan kasi ya utendaji wa viongozi wa wizara, ushirikishwaji wa wadau na kutangaza utalii kimataifa.

Wadau hao wametoa kauli hizo kwenye mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta za Wanyamapori na Misitu uliofanyika leo Mei 25, 2023 jijini Arusha.

Wamefafanua kuwa katika kipindi kifupi baada ya Rais Samia kuteua viongozi wapya wa Wizara, mwanga wa matumaini ya maendeleo na mapinduzi makubwa umeanza kuonekana.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji na Wauzaji wa Nyamapori Tanzania, Fransis Nade amesema katika kipindi hiki cha takribani miezi mitatu kumekuwa na ushirikishwaji mkubwa kwa wadau ambapo kumekuwa na mapitio makubwa ya maeneo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha uhifadhi wa raslimali nchini.


Amesema njia pekee ya kuimarisha sekta hizo ni kuwashirikisha wadau kwa kufanya majadiliano ili waweze kutoa changamoto wanazokabiliana nazo hatimaye sekta iweze kutoa mchango mkubwa katika taifa ambapo mkutano wa leo umeshirikisha wadau wote. 

“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutuletea mabadiliko haya katika kipindi hiki kwenye Wizara yetu, Mungu ambariki sana kwani kazi kubwa imefanywa na viongozi wa wizara tunaamini sekta zetu zinakwenda kuchangia kiasi kikubwa kwenye uchumi wetu." amefafanua mdau wa Wanyamapori Jackson Msome.

Mdau wa asali mwenye uzoefu wa miaka 53 katika sekta hiyo, Kimishua Yona amesema kiwango ambacho Waziri Mchengerwa alielekeza katika kilele cha siku ya Misitu na Asali cha kuzalisha tani 138000 kutoka tani 35000 kwa mwaka za sasa kinaweza kwenda mara mbili zaidi kama wananchi watatumia utaalam.


Akiongea na wadau hao, Mchengerwa amesema katika kipindi hiki kifupi amebaini changamoto kadhaa ambazo amesema zinakwenda kutatuliwa.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na Kampuni za Uwindaji wa Kitalii kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani, (Value Added Tax) kwa huduma zisizotozwa kodi (Non - taxable services).

Kumekuwa na ucheleweshaji wa migawo ya fedha kwa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii kutokana na kubadilishwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa fedha na uhakiki wa viwango vinavyopaswa kutumwa.

Aidha, amesema kuwepo kwa tozo nyingi katika biashara ya mazao ya misitu na amefafanua kuwa Wizara imechukuwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ili kuona uwezekano kupunguza viwango vya tozo.

Mathalani Tozo ya CESS imepunguzwa hadi asilimia 3. Wizara inaendelea kulifanyia kazi suala hili.Pia kukosekana kwa wataalam wa kada ya misitu na ufugaji nyuki katika Halmashauri za Wilaya nyingi nchini hali inayosababisha mwitikio mdogo wa wananchi kushiriki katika shughuli za sekta za misitu pamoja ufugaji nyuki na kukosekana kwa soko la pamoja la mazao ya nyuki.


Amewataka watendaji wa Wizara kubadilika  na kuwa na uchungu wa nchi yao.

Post a Comment

0 Comments