HOSPITALI ya E.M iliyopo Mji Mwema wilayani Kigamboni, Dar es Salaam, inatarajia kuwanufaisha wananchi walioizunguka kwa kuweka utaratibu wa kutoa huduma kwa wasio na uwezo kwa kutumia mfuko utakaouanzishwa ili kubeba gharama za kuwachangia wasio na uwezo.
Hayo yamebainishwa jijini, Dar es Salaam na mmiliki wa hospitali hiyo Dk. Egina Makwabe alipokuwa akizungumzia hospitali hiyo mpya yenye hadhi na viwango vya hospitali ya mkoa, iliyofunguliwa Machi 27, mwaka huu.
Alisema kuanzishwa kwa hospitali hiyo ya kwanza ya binafsi kwa ngazi ya mkoa ndani ya Wilaya ya Kigamboni ni namna mojawapo ya kutoa suluhu ya changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
"Tumechagua kuleta huduma bora na za kisasa Kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla, tutahakikisha huduma zetu zinatolewa kwa weledi mkubwa kwasababu tulifanya uchunguzi na tukagundua wilaya hii inahitaji huduma za afya za kibingwa.
"Tuligundua kuwa hakukuwa na hospitali yoyote ya binafsi ya ngazi ya mkoa na wagonjwa walikuwa wanalazimika kwenda mbali na Kigamboni kufuata huduma za matibabu.
"Tunajipanga ili kuona njia sahihi ya kusaidiana na wananchi waliotuzunguka, hatutaacha kumtibu mtu kwa sababu hana uwezo, kama unaweka hospitali kama hii na umezungukwa na watu ambao hawana uwezo wa kuzipata huduma zako haitaleta maana kwao,” alisema Dkt. Makwabe
Alisema ili kufanikisha utaratibu wa kutoa huduma hata kwa wasio na uwezo wanatarajia kuanzisha mfuko ambao utabeba gharama za kuwachangia wasio na uwezo.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Makwabe alisema pamoja na kuwapo kwa changamoto ya madaktari bingwa nchini, lakini Hospitali ya EM imejipanga kwenye eneo hilo kwani inao wataalamu wa kutosha.
Dkt. Makwabe aliweka wazi kuwa hospitali imejipanga kutoa huduma zote za kibingwa na zisizo za kibingwa zikiwemo huduma za kusafisha damu, huduma za X-Ray, CT-Scan, maabara kubwa, duka kubwa la dawa, matibabu ya meno, macho, masikio, koo, huduma za upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za kulaza, kuhudumia wagonjwa wa nje, matibabu ya mapafu, vidonda vya tumbo, magonjwa ya ngozi pamoja na huduma za wakina mama na watoto.
Kwa upande mwingine Dkt. Makwabe anaishukuru Serikali kwa ushirikiano alioupata kuanzia hatua ya kwanza hadi walipofikia sasa na anaamini ushirikiano huo mzuri utaendelea.
Pia aliomba kuwe na ushirikiano wa vitendo kati ya Serikali na sekta binafsi, kama vile kubadilishana wagonjwa hasa katika maeneo ambayo hospitali binafsi hazina uwezo wa kuwahudumia au hospitali za Serikali hazina uwezo, ni vema kukawa na utamaduni wa kushirikiana kivitendo.
0 Comments