Ticker

7/recent/ticker-posts

TAMSTOA YALIA NA ONGEZEKO KODI YA MAPATO


Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA), Chuki Shaban

Na Sidi Mgumia, Dar Es Salaam

Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA) kimeiomba Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo yao ya namna ya ulipaji kodi ya mapato (adavance tax) ili kuondoa kero zinazowakabili wafanyabiashara wasafirishaji. 

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania, Chuki Shaban alisema kupanda kwa kodi hiyo ya mapato kwa asilimia mia moja kunawatatiza sana wafanyabiashara kwakua mzigo wa ulipaji umeonekana kuwaelemea. 

Mwenyekiti Shaban amesema suala hilo kwao ni shida na wamewaandikia barua Wizara ya Fedha kuwaomba wakae pamoja ili waweze kuzungumza juu ya mapendekezo yao ya naamna ya ulipaji wa kodi.

“Tumepeleka mapendekezo yetu ya namna ya ulipaji wa kodi, bahati mbaya sana mpaka sasa hatujapata majibu na muda wa kulipa kodi hizo umefika, sasa tunaiomba Wizara ya Fedha kama wamepata barua yetu waijibu ili na sisi tuwajibu wasafirishaji, wajue nini kinachoendelea kwasababu mpaka sasa hawaelewi kitu gani kinaendelea,” alisema Shaban

Aliongeza kuwa kuna watu wenye uwezo wakuhamisha biashara zao hapa na kulingana na hali ilivyo wengi wameshahamisha biashara zao kitu ambacho ni kibaya kwa uchumi wa Tanzania, wameomba kabla haijafikia watu wengi wanaoweza kuikimbia nchi hawajakimbia ni vizuri wakae ili watafute muafaka wa nini kifanyike.

Mwenyekiti wa TAMSTOA Chuki Shaban (katikati) akiwa na Muwekahazina wa TAMSTOA Sammy Mkumbwa (kushoto) pamoja na Mark Mgendela  

“Sasa tunamuomba hata na Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine husika watusikilize hoja zetu kwani nia yetu ni kujenga na kufikia malengo yale ambayo serikali inataka kufika tena ikiwezekana zaidi lakini bila kumuumiza mtu,” alisema Shaban

Akifafanua juu ya kupanda kwa kodi hiyo alisema kwa gari moja msafirishaji analipa shilingi milioni 2,790,000 huku akitolea mfano wa namna gani ataumia mfanyabiashara mwenye malori 100 ama 200 ambaye atatakiwa kulipa zaidi ya milioni 500 kwa gari bila yakusahau malipo mengine kama vile mishahara ya madereva na mengineyo jambo ambalo litawafanya wafanyabiashara wakubwa na wa kati wakimbie na kuikosesha nchi mapato.

Katika hatua nyingine, Shaban kwa niaba ya chama chake alitoa shukurani kwa Serikali kwa kuwaunga mkono kwenye safari yao ya kwenda nchi za Zambia na Kongo kwa ajili ya kuangalia ni nini kinasababisha foleni ya malori tangu mwezi wa kumi na mbili mwaka jana mpakani Kasumbalesa.

Alisema baada ya kuwa foleni ile imekaa kwa muda mrefu wakaona ni vizuri wakajionee wao wenyewe ili ikiwezekana warudi Tanzania waongee na viongozi wa Serikali ili waweze kushauriana na nchi husika kwa maana ya Kongo na Zambia na waangalie ni nini kifanyike ili waweze kutatua tatizo hilo kwasababu foleni ikizidi miezi miwili mitatu gari liko njiani na uchumi pia unasimama hiyo miezi.

“Tunaishukuru sana Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tuliwandikia barua ya kuomba ridhaa yao ya kwenda nchi husika hizo mbili na walifanya hivyo mapema sana na tukaondoka mwezi wa tatu tarehe nne kwenda Zambia ambapo tulipokelewa vizuri na balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Methew Edward Mkingule na yeye akashukuru kwa uwepo wetu na akatupa ushirikiano mkubwa sana. Zambia tulipokelewa pia na wanachama wa Chama cha Wasafirishaji wa Zambia (ZAFA), tunafanya nao kazi kwa karibu sana,” alisema Shaban

Alisisitiza kuwa wakiwa mpakani Kasumbalesa, walifanikiwa kufanya mkutano na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zambia, Chipoka Mlenga wakatoa maoni yao na Waziri akayapokea na kuahidi kuyafanyia kazi.

Wajumbe wa kamati kuu TAMSTOA wakiwa katika mazungumzo na balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Methew Edward Mkingule (katikati). Kikao kilifanyika ofisi za Ubalozi, Lusaka, Zambia

Kikubwa walichokiona ni mapungufu katika suala la muda wa kazi ambapo katika mpaka huo shughuli zinafanyika wakati wa kazi tu, wakati kwa upande wa Tanzania mpaka kutoka Tunduma ofisi zinafanya kazi masaa 24 na hiyo ndio sababu yakukwama magari kwakua hayahudumiwi kwa wakati.

“Kwahiyo tukawaomba napo wafanye kazi masaa 24, tukiamini kwamba kwa kufanya hivyo inaweza ikawa ni moja kati ya utatuzi, walikubali wazo letu na siku hiyo hiyo bahati nzuri wakasaini mkataba wa Zambia na Kongo kuhakikisha wanafanya kazi masaa 24,” alisema Shaban

Hata hivyo, Shaban aliutaja ufinyu wa barabara ya kuingia mpaka wa Zambia kuwa ni sababu nyingine inayosababisha msongamano wa malori, walimueleza Waziri Mlenga juu ya hilo na aliahidi kwamba mvua hizi za sasa zikiisha tu ujenzi wa barabara utaanza rasmi ili kuitanua kurahisisha malori kuweza kupishana kirahisi kupunguza msongamano.

“Kulingana na ushirikiano tulioupata katika kushughulikia sakata la kukwama kwa malaori, tunaishukuru sana serikali yetu pamoja na zile za Zambia na Kongo kwa ushirikiano waliouonyesha na ahadi za kuendelea kuweka mambo sawa. Kwa niaba ya wasafirishaji tunasema tumeridhika kabisa kwakua kazi ilikwenda vizuri,” alisema Shaban

Kama sehemu ya kazi waliyoifanya Zambia na Kongo, wametengeneza ripoti ambayo wataikabidhi Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Ujenzi lakini pia Ofisi ya Waziri Mkuu ili katika vikao vyao vya mara kwa mara waweze kuwa wanakumbushia mambo ya msingi ili zile changamoto zilizopo zisiweze kujirudia tena.

Kwa upande mwingine, Shaban aliongelea suala la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuwasajili madereva, ambapo alisema wamekubaliana kwamba iwepo kanzidata (database) ya madereva ambayo itasaidia kuwafuatilia.

“Sisi kama wafanyabiashara wasafirishaji tunaunga mkono sana suala hilo kwasababu ni rahisi kwa ufuatiliaji, ni rahisi kwa dereva mwizi kujirekebisha kwa kuogopa kwamba taarifa zake ziko kwenye kanzidata. Lakini sasa viambatanisho ambavyo vinatakiwa kwenye kuwasajili ndio imekuwa shida mfano vyeti walivyosomea udereva ambavyo hawana, suala hili limekuwa linasuasua kwasababu ya ukiritimba wa LATRA, wameweka vigezo vingi ambavyo haviwezekani,” alisema Shaban

Alisisitiza kuwa wao kama TAMSTOA wanawashauri LATRA wawasajili madereva wote kwa namba za leseni zao, ambao wanakidhi vigezo vyakusajiliwa kwa maana ya kwamba wale wanaofanya kazi za usafirishaji, wanaoendesha magari ya biashara, halafu ikiwezekana LATRA wawaulize polisi wa trafiki vyeti vya hao madereva viko wapi, kupitia serikali kwa serikali watavipata tu hivyo vyeti, na vinginevyo sio kosa la aliyepewa leseni, ni kosa la mtoa leseni  




Post a Comment

0 Comments