Ticker

7/recent/ticker-posts

KWANINI SHIRIKA LINA NDEGE 131 LAKINI ZINARUKA 416 KWA SIKU?"

Kwa kifupi Ndege moja inaweza kuruka zaidi ya mara moja kwa siku 'Multiple flights' kutoka sehemu moja au sehemu tofauti.

Hii inategemea na ratiba zilizopangwa na shirika/kampuni ya usafiri wa anga.

Kwa mfano, tumenunua ndege 01 kwa shirika la kusadikika kisha tuibatize "KICHWA NGUMU AIR" kwa kifupi "KN" kisha ipangwe ratiba ya siku moja kama ifuatavyo:

Dar - Mwanza (Saa 1 asbh)

Mwanza - Kilimanjaro (Saa 3 asbh)

Kilimanjaro - Dodoma (Saa 5 asbh)

Dodoma - Mbeya (Saa 7 mchana)

Mbeya - Dar (Saa 9 mchana)

Katika usafiri wa anga, ratiba hiyo ni sawa na ndege 5 zinazoruka kila siku kutoka vituo na saa tofauti, ingawa ndege ni moja.

Safari au miruko hii inaitwa 'flights' iwe inaruka ndani au nje ya nchi.

Endapo utafika dirisha la Maulizo/Tiketi kuuliza kuhusu safari za shirika la 'KICHWA NGUMU AIR' na mhudumu akakujibu ifuatavyo;

"Kuna ndege 05 zinazoruka kila siku kutoka na kwenda mikoa tofauti.."

Hapo anamaanisha 'miruko' na sio idadi ya ndege.

Pia kila safari inaweza kuwa imesajiliwa namba yake (Flight/Route Number)

Kwa mfano:

Dar-Mwz flight no. "KN001"

Mwz-JRo flight no. "KN002"

Jro-Dod  flight no. "KN003" n.k

Lakini pia inawezekana kuingia ubia wa kuruka kwa niaba kati ya "KICHWA NGUMU AIR" na kampuni au shirika lingine (Code Sharing)

Kiuhalisia sekta ya usafiri wa anga ipo tofauti kidogo (Complex) na sekta nyingine za usafiri endapo hutatuliza kichwa.

Ili uweze kuelewa vizuri huna budi kutenga vitu ulivyojijengea au kukariri ndipo mambo yataingia akilini.

Mfano mwingine mzuri, kwa akili ya kawaida wengi tunafahamu kuwa, Uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere (#JNIA) una barabara mbili tu za kuruka na kutua ndege (Runways) zilizokaa mfano wa X, yaani barabara moja imekatiza nyingine.

Barabara mojawapo ya kuruka na kutua ndege (ambayo ni ndefu) imechorwa namba 05 kutokea kitunda na 23 kutokea Jeti.

Barabara ya pili ya kuruka/kutua ndege (ambayo ni fupi) imechorwa namba 14 kutokea majumba sita na namba 32 kutokea eneo la jeshi.

Kwa maana hiyo, ukimuuliza mtu asiyefahamu kwa ufasaha masula ya usafiri wa anga, anaweza kukuambia uwanja wa ndege Julius Nyerere una Barabara mbili za kuruka na kutua ndege.

Lakini kitaalamu hizi Barabara zinahesabika kama Njia Nne za kuruka na kutua ndege (Four Runways) ingawa kwa kutazama zinaonekana mbili.

Kila namba inahesabika kama Njia inayojitegemea, lakini pia hizo namba sio urembo bali ni uelekeo wa Dira 'Nyuzi°(Compass Bearings)

Hii ina maana nyuzi 360° inawakilisha kaskazini, 90° zikiwakilisha mashariki, 180° zikiwakilisha kusini, na 270° zikiwakilisha magharibi.

Kwahiyo, Barabara namba 23 ni uelekeo wa nyuzi 230°,

Barabara namba 05 ni uelekeo wa nyuzi 050° n.k.

Rubani anapokuwa kwenye njia hizi moja kwa moja anafahamu uelekeo wa ndege yake hata pasipo kusoma Dira.


                      

Post a Comment

0 Comments