Ticker

7/recent/ticker-posts

JESHI LA SUDAN LINAPIGANA NA KINYAGO CHAKE

Na Masudi Rugombana,Goba, Dar es salaam.

Sudan, taifa kubwa la Kiarabu la Kaskazini Mashariki ya Afrika linatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mapigano makali yaliyoanza jana Jumamosi April 15, 2023 baina ya Jeshi la nchi hiyo na kundi la wanamgambo linalojulikana kama Jeshi la Msaada wa haraka (Rapid Support Forces (RSF) yamesababisha mshituko mkubwa nchini humo na pia kwenye eneo zima la Pembe ya Afrika ambalo kwa miaka mingi limekuwa ni eneo lisilokuwa na utulivu wa kisiasa kuanzia Somalia, Eritrea, Sudan Kusini mpaka Ethiopia.

Kufuatia mapigano yaliyoanza jana, kundi la RSF limedai kuteka Ikulu ya nchi hiyo, Makazi ya mkuu wa majeshi pamoja na viwanja vya ndege muhimu ukiwemo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Khartoum. Kutekwa kwa maeneo hayo muhimu kunaashiria mkakati wa kundi hilo kutaka kufanya mapinduzi dhidi ya kiongozi wa sasa wa kijeshi wa Taifa hilo Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan. 

Kinachoendelalea sasa ni Makundi haya mawili kuwania udhibiti wa nchi. Jeshi la Sudan linaloongozwa na Rais Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na Rapid Support Force, kundi lenye nguvu la kijeshi linaloongozwa na Makamu wa Rais Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Hamedti). Ikumbukwe kwamba Majenerali hawa wawili waliungana kuchukua nchi katika mapinduzi kijeshi ya Oktoba 25, 2021. 

Vurugu hizi zinakuja baada ya miaka mingi ya mvutano mkubwa kati ya kundi la RSF na jeshi la Sudan, wakati nchi hiyo ikifanya jitihada za kuhamishia madaraka kwa serikali itakayoongozwa kiraia. Kiini cha mvutano huo ni namna gani kundi hilo la RSF litakavyojumuishwa katika jeshi la Sudan sambamba na majukumu yake ndani ya jeshi hilo. Kujumuishwa kwa kundi hilo ndani ya jeshi ni sehemu muhimu katika makubaliano yatakayowezesha kuundwa kwa Serikali ya kiraia.


Kundi hili la Rapid Support Forces (RSF) lilianzishwa na Serikali ya Sudan wakati wa Utawala wa kiongozi wa kijeshi Field Marshall Omar Hassan Ahmad al-Bashir mwaka 2013. RSF ni zao la kundi la Janjaweed, kundi la wapiganaji wa Kiarabu lililoanzishwa kwa lengo la kupambana na wananchi wa mkoa wa Darfur, Magharibi ya Sudan waliokuwa wakipigania kujitenga kupitia kundi la waasi la Harakat Tahrir Al-Sudan (Sudan Liberation Movement/Army)linaloongozwa na mwanasheria Abdul Wahid Mohamed al Nur aliyekuwa akisaidiwa na mwanaharakati Suliman Arcua Minnawi (Minni Minnawi). 

Kundi hili lilihusika na uhalifu mkubwa dhidi ya jamii za Waafrika weusi mkoani Darfur likibaka, kupora, na kuchoma vijiji. Likipigana kwa kutumia ngamia, farasi na Magari ya Kijapan aina ya Toyota Land cruiser pick up zilizofungwa machine guns, Kundi hili lilimsaidia Omar al-Bashir  kukomesha uasi mkoani Darfur wakati ambao jeshi la Sudan liliposhindwa kupigana kwa ufanisi kwenye maeneo ya vijijini yenye ukame licha ya kusifika kuwa na jeshi imara la anga na jeshi la ardhini lenye nguvu na silaha nzito.

Rais Omar al Bashir alilibadilisha kundi Janjaweed kuwa kitengo rasmi cha kukabiliana na matukio ya dharura ya uasi pamoja na vurugu za kikabila likipewa jina jipya la Vikosi vya Msaada wa Haraka. (Rapid Support Forces)   Bashir aliimarisha kitengo hicho kifedha na makamanda wake walilipwa vizuri na kukabidhiwa vitengo na maeneo muhimu yenye rasilimali na hivyo kwa muda mchache walikua matajiri na wenye nguvu. Serikali ya Sudan ilianza kupeleka kundi hilo nje ya Darfur ili kukabiliana na ghasia za kikabila kwenye mipaka ya Sudan.

Mnamo 2019, Rais Omar al Bashir aliondolewa mamlakani kufuatia maandamano makubwa ya kiraia. Miaka miwili baadaye, wanajeshi na RSF walifanya mapinduzi kabla ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya mseto wa kiraia na kijeshi mwaka 2022 kufuatia shinikizo la kimataifa. Hii ni serikali ya mpito yenye jukumu la kuirejesha Sudan kwenye utawala kamili wa kiraia ndani ya mwezi huu wa April, 2023. Kwa hivyo basi kinachotokea sasa hivi Sudan ni sawa na mtu kupambana na kinyago chake. Yaani Jeshi la Sudan linapigana na kikundi ilichokianzisha. 


RSF inaongozwa na Makamu wa Rais Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana duniani kote kama Hemedti. Kundi hilo lina takriban askari laki moja nchini kote.  Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Hemedti aliendesha kampeni ya haraka ya kuajiri askari wengi ili kusaidia kukuza uwezo wa kundi hilo. Wanajeshi wake wanatoka kwa kiasi kikubwa Magharibi mwa Sudan, karibu na Darfur, na maeneo ambayo yamepuuzwa kwa muda mrefu na serikali, ikiwa ni pamoja na mikoa ya mashariki karibu na Bahari ya Shamu na mpakani na Sudan Kusini.

Kiongozi wa kundi hilo, Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), mwenye asili ya Chad, ni kiongozi wa zamani wa kundi la Janjaweed ambaye aliishi katika eneo la Darfur katika miaka yake ya ujana, anasifika kwa unyenyekevu, ni mchungaji wa ngamia kutoka kabila dogo la Kiarabu huko Darfur. Ni mtu mwenye ushawishi mkubwa nchini Sudan aliyefanikiwa kuigeuza RSF kuwa kundi  lenye nguvu huku akitoa askari mamluki kupigana vita upande wa Saudi Arabia nchini Yemen na pia nchini Libya kwa niaba ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kiongozi huyo wa kundi hatari la RSF pia ana ushirikiano mzuri wa kibiashara na Kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner Group katika uchimbaji wa dhahabu na shughuli za usalama katika maeneo ya uchimbaji dhahabu ya Sudan.

Hamedti anajipambanua kama kiongozi anayetetea watu kutoka maeneo yaliyopuuzwa nchini Sudan kwa kutoa misaada ya kibinaadamu ikiwemo chakula na matibabu. 

Kuibuka kwa mapigano baina ya viongozi hao wakuu wa kijeshi kunavuruga jitihada za kuirejesha Sudan kwenye utawala wa kiraia mwezi huu kama inavyotarajiwa. Jitahada kubwa zinahitajika kutoka umoja wa Mataifa, Marekani, Urusi, Saudi Arabia na mataifa jirani yenye nguvu kama Ethiopia na Misri ili kuzikutanisha pande hasimu kwenye meza ya mazungumzo na kufikia makubaliano ya kuondoa uhasama kwa manufaa ya wananchi wa Sudan na pia kwa maslahi ya kiusalama kwenye eneo la Pembe ya Afrika.

Ruksa kunakili na kusambaza makala hii, kumbuka kufanya acknowledgement.

Napatikana kupitia

masudirugombana@gmail.com

Post a Comment

0 Comments