Ticker

7/recent/ticker-posts

WANAFUNZI 49,000 KUNUFAIKA NA FEDHA ZA BARRICK

 

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu na rais wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Briston mara baada ya mazungumzo Yao yaliyofanyika Ikulu Chamwino, jijini Dodoma. 

SERIKALI ya awamu ya Sita inaendeleza harakati zake za kuboresha elimu na miundombinu yake nchini baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ahadi yad ola milioni 30, zilizoelekezwa kwenye elimu na Kampuni ya kuchimba Dhahabu ya Barrick.

 

Katika kulifanikisha hilo leo Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow alikutana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo pamoja na mambo mengine alithibitisha kutimiza ahadi yake ya Dola Milioni 30 (takriban shilingi bilioni 70.5 ) ambazo zitaelekezwa kwenye upanuzi wa miundombinu ya elimu nchini Tanzania kwa ushirikiano na Serikali.

 

Fedha hizo ni sehemu ya Programu ya Barick-Twiga ya kusaukuma mbele mustakabali wa Elimu, maarufu kama “Barrick-Twiga Future Forward Education Program”.

 

Fedha hizo zimeelekezwa kujenga madarasa 1,090, majengo ya vyoo na vyoo 1,640 na mabweni 270 katika shule 161 nchini kote. Mabweni hayo yanatarajia kusaidia malazi ya wanafunzi 49,000 kati ya wanafunzi wapatao 190,000 wanaotarajiwa kuanza masomo yao ya sekondari ya juu (A-level) Julai mwaka huu. 

 

Dola milioni 10 za kwanza zitalipwa mwezi Aprili na kiasi kinachosalia kitatolewa kadiri programu hiyo itakavyokuwa inaendelea.

“Tunaamini kuwa elimu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Migodi yote miwili ya dhahabu ya Bulyanhulu na North Mara inaendelea kusaidia sekta ya elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa na kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo yanayoizunguka migodi hiyo, jambo ambalo limefanikisha baadhi ya shule hizo kuwa miongoni mwa shule zinazoongoza mara kwa mara katika mikoa hii,” alisema Bristow.

Mgodi wa North Mara tayari umetumia dola milioni 1.9 (shilingi bilioni 4.5) katika shule 87 za msingi na sekondari wilayani Tarime, shule 14 kati ya hizo zikiwa zile zilizofanya vizuri zaidi wilayani humo. 


Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 30,000,000.00 kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Mark Briston 
Mgodi wa Bulyanhulu umetumia dola milioni 1.8 (shilingi bilioni 4.2) katika miradi 80 ya elimu katika eneo linalouzunguka mgodi huo na hivi sasa inajenga Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Kijiji cha Bunango. 

 

Uwekezaji wa Barrick katika eneo linalouzunguka mgodi huo umewezesha wasichana wa Kitanzania 7,557 kupata elimu mwaka 2022.

“Licha ya msaada wa kampuni wa kustawisha elimu, mwaka jana, North Mara ilitambuliwa rasmi kama mlipakodi mkubwa zaidi nchini Tanzania na Bulyanhulu ilitunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora anayezingatia matakwa ya sheria, ambayo ilitolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii. North Mara na Bulyanhulu pia zilipata tuzo za mshindi wa kwanza na wa pili, mtawalia, kwa uuzaji wa madini nje ya nchi na kwa kuingiza fedha za kigeni nchini. Kampuni zote mbili zimetoka mbali sana na tunatarajia kuendelea na safari hiyo kupitia ubia wetu wa Twiga na serikali.”

Bristow alisema tangu Barrick ilipoichukua migodi hiyo mwaka 2019, imeingiza dola bilioni 2.4 katika uchumi wa Tanzania. Kupitia kamati zake za maendeleo ya jamii, migodi hiyo imewekeza zaidi ya dola milioni 10 katika miradi ya kuboresha huduma za afya, elimu, upatikanaji wa maji ya bomba na miundombinu ya barabara.

Post a Comment

0 Comments