Ticker

7/recent/ticker-posts

SERIKALI, WFP, UNCDF KUWEZESHA WATANZANIA NISHATI SAFI





Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza wakati wa kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililofanyika jijini Dodoma ambalo lilihusisha wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za Serikali na Wadau wa Maendeleo. 

Zuena Msuya Dodoma

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani (WFP), Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) na wadau wengine wa maendeleo ndani na nje ya nchi wanafanya jitihada mbalimbali ili kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ndani ya kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba wakati akifungua Kongamano la siku mbili la Nishati Safi ya kupikia lililoandaliwa na WFP na UNCDF ambalo limelenga kuzikutanisha pamoja Serikali, Sekta Binafsi na wadau wa maendeleo ili kwa pamoja waweze kufanikisha azma ya Serikali ya kuwezesha watanzania kuhama kutoka kwenye nishati isiyo safi ya kupikia na kutumia nishati safi ya kupikia.

Mramba amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 1 Novemba 2022 wakati wa ufunguzi wa Mjadala kuhusu Nishati safi ya kupikia, kuwa asilimia 80% ya watanzania wanatakiwa kutumia nishati safi ya kupikia ndani kipindi cha miaka 10.

Ameongeza kuwa, Mhe.Rais alielekeza pia kuanzishwa kwa kikundi kazi cha kusimamia ishati safi ya kupikia na kutengeneza mpango mkakati wa miaka kumi wenye sheria,utaratibu na kanuni zitakazotumika katika nishati safi ya kupikia ambapo Kikundi kazi hicho kinaendelea na kazi husika.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (katikati waliokaa), Mkurugenzi Mkaazi na Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani nchini Tanzania, Bi.Sarah Gibson (wa Pili kulia waliokaa) na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam Kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zke waliohudhuria kongamano  la Nishati Safi ya Kupikia lililofanyika jijini Dodoma. 


“Katika kutekeleza na kufanikisha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali kama vile sekta binafsi, wagunduzi na wavumbuzi, wadau wa nishati ya kupikia ili kuhakikisha mipango yote iliyowekwa na Serikali inafanikiwa, na sasa tuko katika hatua za kukamilisha mpango mkakati wa miaka kumi wa kuangalia taratibu na sheria zinazokinzana ili wote tuzungumze lugha moja.’’ amesema Mhandisi Mramba.

Ameongeza kuwa, kwa sasa kumekuwa na mwitiko mkubwa wa wanasiasa pamoja na viongozi mbalimbali  katika ngazi ya Mikoa, Wilaya na Vijiji katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi na Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), Sarah Gibson, amesema kuwa shirika hilo litashirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa mipango iliyojiwekea ya watanzania kutumia nishati safi ya kupiikia inafanikiwa.

Naye, Meneja katika Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Imanuel Muro amesema taasisi hiyo inatoa mitaji kwa wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara ya bidhaa za nishati safi ya kupikia kwa kuwapa masharti ya kupunguza bei ya bidhaa zao ili watumiaji wazipate kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Post a Comment

0 Comments