Ticker

7/recent/ticker-posts

EL NINO KIGAMBONI: MFEREJI WASAFISHWA, MTARO WENYE UTATA WAIBUA WASIWASI


 Hatua za kinga zaendelea chini ya daraja,viongozi wahofia athari mtaro unaodaiwa kuzibwa na kifusi.

NA.FATMA JALALA

Wakati tahadhari ya mvua kubwa za El Niño ikiendelea kuwekwa mbele ya wananchi, kazi ya kufukua na kusafisha mfereji ulio chini ya daraja katika eneo la Mikadi kata ya Magogoni Kigamboni, inaendelea. Hata hivyo, wasiwasi bado upo kuhusu mtaro unaodaiwa kuzibwa na kifusi katika eneo la jengo la mwekezaji mzawa Mohammed Scaba Scuba, mwanzoni mwa Mtaa wa PC, ambapo viongozi wa eneo wanaonya kuhusu uwezekano wa maji kuathiri makazi ya wananchi mvua kubwa zikianza kunyesha.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magogoni, Ally Sharrif, ametoa shukrani kwa hatua ya kufukuliwa kwa mfereji, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa na kupunguza hatari ya maji kujaa katika maeneo ya makazi.

Aidha, Mwandishi amejionea kazi ya kusafisha mfereji chini ya daraja ikiendelea, huku Mwenyekiti Sharrif, akieleza kuwa baada ya greda kukamilisha kazi hiyo, linatarajiwa kuelekea eneo la Geti Jeusi kuendelea na shughuli za kusafisha njia za maji.

Hata hivyo, licha ya hatua hiyo, bado kuna wasiwasi kuhusu mtaro ulio karibu na jengo la Scaba, ambao kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo, unadaiwa kuzibwa na kifusi. Wanaeleza kuwa suala hilo linahitaji kufuatiliwa na mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha njia ya maji inakuwa wazi kabla ya mvua kubwa, kwani iwapo njia hiyo haitafunguliwa na mvua kubwa zikaanza kunyesha, wananchi wanaweza kukabiliwa na madhara kutokana na maji kujaa zaidi na shindwa kupita hata kwa njia inayotakiwa.


KAULI “KILA MTU ALINDE NYUMBA YAKE” YAIBUA HOJA YA MASLAHI YA UMMA

Katika mjadala kuhusu usalama wa eneo hilo wakati wa mvua, kauli inayohusishwa na mwekezaji huyo inazua swali kuhusu uwiano kati ya kulinda mali binafsi na wajibu wa kutohatarisha usalama wa watu wengine.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoipata mwandishi kutoka kwa mwandishi mwenzake Ahmed Kombo, alipompigia Scaba kuhusu changamoto iliyopo eneo hilo alimjibu kuwa, “Kila mtu alinde nyumba yake,” akieleza kwa maana ya kauli hiyo kuwa hawezi kukubali nyumba yake ijae maji, jambo linalohusishwa na hatua ya kuziba njia hiyo.

Kauli hiyo inahitaji kuangaliwa katika muktadha mpana wa usalama wa jamii. Ni halali kwa kila mtu kuchukua hatua za kulinda nyumba na mali zake dhidi ya mafuriko, lakini hatua hizo hazipaswi kuhamishia hatari kwa majirani au kuzuia njia ya maji kwa namna inayoweza kuhatarisha makazi ya watu wengine.

WANANCHI MSIWAGAWE VIONGOZI KWA MATABAKA

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Magogoni, Ally Sharrif, viongozi wa ngazi ya mtaa pamoja na Kiongozi wa CCM wamekuwa wakikemea hali ya mtaro unaodaiwa kuzibwa na kifusi katika eneo la jengo la mwekezaji Mohammed Scaba Scuba, wakihofia athari zinazoweza kuwakumba wananchi mvua kubwa zikianza kunyesha.

Hata hivyo, Sharrif anadai, jitihada hizo hazijazaa matokeo yaliyotarajiwa, akieleza kuwa kwa mtazamo wake, mwekezaji huyo haonekani kuyapa uzito maelekezo ya viongozi wa ngazi za chini.

Madai hayo yanaibua swali kuhusu namna maelekezo ya viongozi wa ngazi za chini yanavyochukuliwa uzito, sambamba na wananchi yanavyopaswa kushughulikiwa pale inapohusu hatari inayoweza kuathiri usalama wa jamii. Katika mazingira ambayo mvua kubwa zinatarajiwa, hoja si hadhi ya kiongozi anayewasilisha malalamiko, bali uharaka wa kuchunguza tatizo na kuchukua hatua zinazostahili.

Mwandishi alijaribu kuwasiliana na mwekezaji huyo ili kupata maelezo yake kuhusu madai hayo na hali ya mtaro, lakini hakufanikiwa kumpata hadi wakati wa kukamilisha makala haya. Hivyo, maelezo yake yanabaki kuwa muhimu ili kuweka suala hilo katika uwiano na kufahamu hatua anazochukua kuhusu changamoto inayolalamikiwa.

Hoja ya msingi si kupinga haki ya mtu kulinda mali yake, bali kuhakikisha kuwa hatua za kujilinda hazikiuki wajibu wa kulinda usalama wa jamii na miundombinu ya kupitisha maji.

Wasiwasi wao ni kwamba mvua kubwa zikianza kunyesha kama ilivyotabiriwa, hali ya mtaro huo inaweza kuchangia maji kushindwa kupita kwa njia inayotakiwa na hivyo kuongeza hatari ya madhara kwa wananchi na mali zao.

Hali hiyo inaibua swali muhimu: wakati changamoto ya mfereji wa daraja ikipatiwq ufumbuzi,  je, hatua gani zinachukuliwa ili kuhakikisha na mtaro unaodaiwa kuzibwa unafukuliwa kabla mvua kubwa hazijaanza?

BAADA YA MFEREJI KUFUKULIWA, MTARO NAO UFUATE

Hatua ya kuanza kufukua na kusafisha mfereji chini ya daraja ni maendeleo katika jitihada za kupunguza hatari zinazoweza kusababishwa na maji mengi wakati wa mvua.

Kwa mujibu wa Sharrif, kazi hiyo ikiisha, greda litaendelea na kazi katika eneo la Geti Juesi. Hatua hiyo inaonesha kuwa kazi za kushughulikia baadhi ya changamoto za upitishaji wa maji zinaendelea.

Hata hivyo, kwa viongozi wa eneo hilo, kazi hiyo inapaswa kwenda sambamba na kushughulikia maeneo mengine ambayo yanadaiwa kuathiri mtiririko wa maji, hususan mtaro ulio katika eneo la jengo la Scaba.

Hoja yao ni kwamba kusafisha mfereji mmoja pekee hakuondoi hatari zote ikiwa njia nyingine muhimu za maji bado zina vikwazo.

Kwa hiyo, pamoja na hatua inayoendelea chini ya daraja, kinachohitajika ni ufuatiliaji wa maeneo yote yaliyobainishwa kuwa na changamoto, ili kuhakikisha maji yanapata njia ya kupita bila kuelekezwa kwenye makazi ya wananchi.

HOFU IMEBAKI KWENYE MTARO MBELE YA JENGO LA MWEKEZAJI

Kwa sasa macho na masikio ya wananchi ni kwa viongozi wao juu ya eneo la jengo linalohusishwa na mwekezaji huyo, lililopo mwanzoni mwa Mtaa wa PC, Magogoni, miongoni mwa maswali ya kujiuliza, je, eneo hilo litafikiwa na utekelezaji ? Ambapo baadhi ya wananchi walitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wakimtaka mwekezaji huyo kutumia busara ili kuwanusuru wananchi wa eneo hilo badala ya kutunisha misuli na kumtafuta nani zaidi. 

Hata hivyo, suala hilo linahitaji kufuatiliwa na mamlaka husika ili kuthibitisha hali ya mtaro, kubaini chanzo cha kizuizi na kuchukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria na wajibu wa kila upande.

Jambo la msingi si nani anamiliki jengo, bali ni kuhakikisha kuwa shughuli za ujenzi au matumizi ya ardhi haziathiri njia za maji kwa namna inayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.

Iwapo itathibitika kuwa mtaro umezibwa na kifusi na kuathiri upitishaji wa maji, hatua za kurejesha njia hiyo zinapaswa kuchukuliwa kabla mvua kubwa hazijaleta madhara.



HATUA ZA UFUATILIAJI CHANGAMOTO HIYO

Katika ufuatiliaji wa awali uliofanyika Septemba 21 na 22, 2026, Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Magogoni, Ally Sharrif, alitembelea baadhi ya maeneo yenye changamoto za mifereji na njia za maji, akishirikiana na wataalamu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), na wakati mwingine akiwa na Diwani wa Kata ya Tungi, Ernest Mafimbo.

Katika ufuatiliaji huo, ilielezwa kuwa baadhi ya changamoto za miundombinu ya mifereji zinahitaji pia ushirikiano wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), jambo linaloonesha umuhimu wa mamlaka husika kuweka wazi wajibu wao na kuratibu hatua za utatuzi.

Sharrif pia amekuwa akifuatilia suala la mtaro katika eneo la jengo la Scaba kupitia mawasiliano na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mikaya Tumaini Dalmia.

Kwa mujibu wa Sharrif, baada ya juhudi za awali za mawasiliano kutofanikiwa, aliendelea kutafuta njia ya kumfikia Mkuu huyo wa Wilaya ili kuwasilisha changamoto zinazowakabili wakazi wa Magogoni.

Katika mawasiliano ya simu yaliyofanyika mbele ya waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya aliahidi kutembelea eneo hilo ili kujionea hali ya mifereji na njia za maji na kufuatilia changamoto zilizowasilishwa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sharrif, Mkuu huyo wa Wilaya hakufika katika muda ulioahidiwa, bali alitembelea eneo hilo baadaye. Sharrif amesema changamoto alizokuwa amewasilisha bado zilihitaji kutatuliwa baada ya ziara hiyo.

Taarifa hiyo inaonesha umuhimu wa ziara za viongozi kuambatana na hatua zinazoweza kufuatiliwa, hasa pale changamoto inayohusika inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi wakati wa mvua.

 Kwa kuwa kazi ya kusafisha mfereji chini ya daraja sasa imeanza, hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa maeneo mengine yaliyobainishwa yanafanyiwa tathmini na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

 CCM YATAKA MASHINE YA KUNYONYEA MAJI MAGOGONI

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Magogoni, Hafidh Saleh, amekuwa akitoa wito kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kuchukua hatua za maandalizi ya mvua, ikiwamo kushughulikia mifereji yenye changamoto na kuweka utaratibu wa upatikanaji wa mashine za kunyonya maji katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na maji mengi.

Wito huo unaweka msisitizo katika umuhimu wa maandalizi yanayochanganya hatua za kuzuia au kupunguza madhara na mipango ya kuwasaidia wananchi endapo maafa yatatokea.

Kwa wakazi wa maeneo yenye changamoto za mifereji, hatua za kinga zina umuhimu mkubwa kwa sababu zinaweza kusaidia kupunguza hatari kabla haijageuka kuwa maafa.

Hata hivyo, ufanisi wa maandalizi hayo utategemea kasi ya utekelezaji, ushirikiano wa mamlaka husika na namna changamoto zilizobainishwa zinavyoshughulikiwa.



KINGA NA MSAADA VINA MAJUKUMU TOFAUTI

Katika maandalizi hayo ya kukabiliana na mvua kubwa, jambo la msingi si kujiandaa tu kwa namna ya kuwasaidia wananchi baada ya maafa kutokea, bali pia kutumia muda uliopo kupunguza uwezekano wa madhara hayo kutokea. Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na mamlaka nyingine zinazohusika zina wajibu wa kuhakikisha maeneo yote hatarishi yanafanyiwa kazi kabla mvua hazijaleta madhara.

Ni muhimu kuwa na mipango ya dharura inayohusisha upatikanaji wa chakula, malazi na mahitaji mengine kwa wananchi watakaoweza kuathirika. Hata hivyo, mipango hiyo inapaswa kwenda sambamba na hatua za kinga, zikiwamo kusafisha mifereji, kuondoa vizuizi katika njia za maji na kushughulikia maeneo yanayoweza kuhatarisha makazi na mali za wananchi.

Kwa mazingira ya Kigamboni, ambako baadhi ya changamoto za mifereji tayari zimebainishwa na kazi ya usafishaji imeanza, kinachohitajika ni kuendeleza juhudi hizo na kuhakikisha maeneo mengine yenye changamoto yanapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Kusubiri maafa yatokee ndipo fedha zitafutwe kwa ajili ya kuwasaidia waathirika si ishara ya maandalizi madhubuti; kunaweza kuonesha udhaifu wa ubunifu na uwajibikaji katika kuzuia madhara yanayoweza kupunguzwa mapema. Fedha na mipango ya dharura ni muhimu, lakini thamani yake huongezeka pale inapoambatana na hatua za kinga zinazolinda maisha, makazi na mali za wananchi.

Wananchi wanahitaji kuona maandalizi yakigeuka kuwa matokeo yanayoonekana: mifereji ikisafishwa, njia za maji zikifunguliwa na maeneo hatarishi yakishughulikiwa kabla ya mvua kubwa. Huo ndio msingi wa maandalizi yenye kuweka usalama wa wananchi mbele, badala ya kusubiri madhara yatokee ndipo hatua za dharura zichukuliwe.


WANANCHI WANAHITAJI UONGOZI UNAOTOA MATOKEO

Uongozi unaoweka maslahi ya wananchi mbele hupimwa kwa uwezo wa kutambua changamoto, kuzitafutia ufumbuzi na kuhakikisha hatua zinazochukuliwa zinaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya watu. Katika mazingira ya Kigamboni, ambako baadhi ya maeneo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za mifereji na upitishaji wa maji, maandalizi ya mvua yanapaswa kuwa sehemu ya utekelezaji wa wajibu huo wa kiuongozi.

Kwa viongozi wa Serikali za Mitaa hadi ngazi za juu za utawala, jukumu si kusikiliza malalamiko ya wananchi pekee, bali pia kuyafanyia kazi kwa wakati, kuratibu mamlaka zinazohusika na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi hadi changamoto zinapopatiwa ufumbuzi. Hii ni sehemu ya wajibu wa viongozi katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa weledi, uwajibikaji na matokeo yenye tija, sambamba na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.

Hatua inayoendelea ya kusafisha mfereji chini ya daraja Kigamboni ni ishara ya utekelezaji unaoanza kuonekana. Hata hivyo, ili juhudi hizo ziwe na matokeo yanayokusudiwa, ni muhimu kazi hiyo ikamilishwe na maeneo mengine yanayohitaji hatua za haraka, ikiwamo mtaro unaodaiwa kuzibwa na kifusi, yafanyiwe tathmini na kupatiwa ufumbuzi kabla mvua kubwa hazijaleta madhara.

KINGA IFANYIKE MAENEO YOTE KWA MASLAHI YA WANANCHI

Kazi ya kusafisha mfereji chini ya daraja ni hatua inayoonekana katika maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa Kigamboni. Hatua inayofuata, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Magogoni, ni kuelekea eneo la Geti Jeusi kuendelea na kazi hiyo.

Lakini maandalizi hayatakuwa kamili ikiwa maeneo mengine yenye changamoto yataachwa bila kufanyiwa tathmini na kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Mtaro unaodaiwa kuzibwa na kifusi katika eneo la jengo la Scaba unahitaji ufuatiliaji wa haraka wa mamlaka husika ili kubaini hali yake, athari zake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kabla ya mvua kubwa.

Wajibu wa kulinda mali binafsi haupaswi kutenganishwa na wajibu wa kulinda usalama wa jamii. Kadhalika, jukumu la mamlaka si kusubiri wananchi waathirike ndipo hatua zichukuliwe, bali kuhakikisha kuwa hatari zinazoweza kuzuilika zinashughulikiwa mapema.

Kwa Kigamboni, mafanikio ya maandalizi hayatapimwa kwa idadi ya ziara au kasi ya greda pekee, bali kwa uwezo wa mamlaka na wahusika kuhakikisha kuwa njia za maji zinapitisha maji kwa usalama na wananchi wanalindwa dhidi ya madhara yanayoweza kuzuilika.

Mvua kubwa ikinyesha, maji hayatauliza nani anamiliki nyumba au eneo. Ndiyo maana hatua za kulinda mali binafsi lazima ziende sambamba na wajibu wa kutohatarisha usalama wa wengine.


 

Post a Comment

0 Comments