Ticker

7/recent/ticker-posts

JE, TAHADHARI YA EL NIÑO HAIWAHUSU KIGAMBONI?


Na Mwandishi Wetu

Wasaidizi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Viongozi wa Kigamboni, hili si swali la lawama. Ni swali la tahadhari, uwajibikaji na usalama wa wananchi.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuhusu msimu wa Vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026, ikieleza uwezekano wa mvua kubwa, mafuriko na madhara kwa miundombinu na afya ya wananchi.

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, pia ametoa maelekezo ya kuchukua hatua mapema, ikiwemo kuzibua mifereji na mikondo ya maji, kusafisha mazingira na kuhakikisha miundombinu ya barabara haiwi chanzo cha kuongeza madhara wakati wa mvua.

Lakini katika baadhi ya maeneo ya Kigamboni, swali la wananchi ni moja: maelekezo haya yamefika katika mitaa ipi?

MIKADI, MAGOGONI, PC, TUNGI NA MAENEO MENGINE

Wananchi wa Mikadi, mitaa ya Magogoni, PC hadi Tungi na maeneo mengine ya Kigamboni wanaeleza kuwa baadhi ya maeneo hukumbwa na maji wakati wa mvua.

Hofu yao sasa si mvua yenyewe, bali maandalizi yaliyofanyika kabla ya mvua kuanza.

Je, mifereji imekaguliwa na kusafishwa? Mitandao ya maji imefunguliwa? Makaravati yameondolewa uchafu na tope? Njia za maji zimeachwa wazi?

Wananchi wanasema hawajaona kwa kiwango wanachotarajia jitihada za kufukua mitaro na kusafisha baadhi ya mifereji, licha ya tahadhari iliyotolewa na mamlaka za kitaifa.

Hapa ndipo viongozi wa eneo wanapaswa kutoa majibu na zaidi ya majibu, kuchukua hatua.

DARAJA LIPO, MFEREJI UMEJIANDAA?

Kwenye barabara ya kuelekea Mikadi Beach, limejengwa daraja imara ambalo ni sehemu muhimu ya miundombinu ya eneo hilo.

Lakini swali la wananchi ni rahisi: daraja liko tayari, je, njia ya maji chini na pembeni yake iko tayari pia?

Kwa hali inayoonekana katika eneo hilo, mfereji unaohusiana na daraja unahitaji kusafishwa ili uweze kupitisha maji kwa ufanisi wakati wa mvua kubwa.

Miundombinu ya barabara haiwezi kutenganishwa na miundombinu ya maji. Daraja zuri linahitaji njia ya maji inayofanya kazi vizuri ili kupunguza hatari ya maji kuziba au kujaa katika eneo hilo.

PC: KIFUSI KATIKA NJIA YA MAJI

Katika eneo la PC, hatua kadhaa mbele ya daraja, wananchi pia wameibua hoja kuhusu kifusi kinachodaiwa kumwagwa katika eneo la mfereji kutokana na ujenzi unaoendelea.

Ikiwa hali hiyo itathibitishwa na mamlaka husika, hatua inapaswa kuchukuliwa kabla mvua haijaanza.

Ujenzi haupaswi kuwa chanzo cha kuziba njia za maji.

Mamlaka zinapaswa kukagua eneo hilo na kujibu: Je, kifusi kimeingia katika njia ya maji? Je, ujenzi unazingatia mahitaji ya mifereji na mikondo ya maji? Na kama kuna kizuizi, hatua gani zimechukuliwa?

Wananchi wanahitaji majibu, lakini zaidi wanahitaji hatua.



KIGAMBONI INAJUA MAENEO HATARISHI

Hakuna sababu ya kusubiri mvua kubwa ili kuanza kubaini maeneo yanayowezakujaa maji.

Wananchi wana uzoefu wa mvua zilizopita. Wanajua sehemu ambazo maji hukusanyika, mitaro inayoziba, makaravati yanayoshindwa kupitisha maji na barabara zinazokuwa ngumu kupitika.

Kwa hiyo, kabla ya Oktoba, kila eneo linapaswa kuwa na jibu la swali moja:

Mvua ikinyesha kwa wingi, maji yatapita wapi?

Ikiwa njia iliyopo imeziba, imefukiwa, imejaa taka au haitoshi, hatua inapaswa kuchukuliwa sasa.

SI LAZIMA MAJI YAINGIE NYUMBANI NDIPO HATUA ICHUKULIWE

Maandalizi ya maafa huanza kabla ya maafa. Kwa Kigamboni, hilo linamaanisha kusafisha mifereji na mitaro, kukagua makaravati, kuhakikisha mikondo ya maji haizuiwi na shughuli za ujenzi na kutambua mapema maeneo yenye hatari kubwa ya mafuriko.

Wananchi nao wanapaswa kupewa elimu na kuwajibika kutotupa taka katika mifereji na kutoa taarifa wanapoona njia za maji zimezibwa.

Lakini jukumu hilo haliwezi kubebwa na wananchi pekee. Mamlaka za eneo husika zina wajibu wa kusimamia.

VIONGOZI WA KIGAMBONI, WANANCHI WANAWAULIZA

Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, Mbunge, Madiwani, Watendaji wa Kata na Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Mitaa:

KIGAMBONI IMEFANYA NINI KABLA YA EL NIÑO?

Je, Mikadi, Magogoni, PC, Tungi na maeneo mengine yanayojulikana kwa kujaa maji kipindi cha mvua yamefanyiwa tathmini? Je, mifereji imekaguliwa na kusafishwa?

 Je, mfereji wa daraja lililojengwa barabara ya Mikadi umeandaliwa? Je, eneo lenye kibao cha mtaa wa PC limekaguliwa kuhusu kifusi kilichomwagwa kwenye ujenzi wa jengo kinachodaiwa kuzuia mfereji?

 Na kama hatua tayari zimechukuliwa, wananchi wanahitaji kuziona na kuzifahamu kwa kuzingatiamuda wa tahadhari husika.

TAHADHARI ISIJE KUWA RIPOTI YA MAAFA

Kigamboni bado ina nafasi ya kuchukua hatua kabla mvua haijaanza. Haitoshi kujenga daraja; njia ya maji chini yake lazima iwe tayari. Haitoshi kujenga barabara; mifereji yake lazima iweze kupitisha maji. Na haitoshi kutoa tahadhari; tahadhari hiyo lazima itafsiriwe kuwa hatua katika mitaa.

Uongozi wa maafa huanza kabla ya maafa. Ndiyo maana swali linaendelea kusimama.

JE, TAHADHARI YA EL NIÑO HAIWAHUSU KIGAMBONI?

Kama inawahusu, maandalizi yaonekane. Kama yameanza, wananchi waambiwe yamefikia wapi. Kama kuna maeneo hatarishi, yashughulikiwe kabla mvua haijaanza. Na kama kuna mifereji iliyofukiwa, iliyozibwa au iliyotelekezwa, isubiriwe nini? Maji yafike mlangoni?

Muda wa maandalizi ni kabla ya mvua.

Post a Comment

0 Comments