Ticker

7/recent/ticker-posts

JET YASHIRIKI KIKAMILIFU KULINDA VIUMBE BAHARI WAKIWEMO KASA


NA MWANDISHI WETU

Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa mazingira na uhifadhi katika kuwalinda viumbe bahari hasa Kas ana matumbawe.

Sea Sense ni miongoni mwa washirika wakubwa wa JET katika kufanikisha kazi hiyo, ambapo moja ya majukumu yao ni kuelemisha jamii ya Watanzania juu ya faida za uhifadhi wa bahari na viumbe vyake, wakiwemo Kasa.


Hatua hiyo inatokana na tishio la kutoweka kwa Kasa nchini Tanzania kutokana na kukithiri kwa shughuli haramu za kibinadamu ndani ya bahari, pamoja na jamii kubwa ya watu wanaoishi kwenye mwambao wa bahari kukigeuza kiumbe hicho kuwa kitoweo.


Katika kuhakikisha elimu juu ya uhifadhi wa viumbe hivyo, JET imekuwa ikishiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Kasa duniani inayofanyika kila Mei 23 ya kila mwaka.


Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alisema moja ya majukumu makubwa ya JET katika kuhakikisha elimu ya uhifadhi wa viumbe bahari hao inafika kwa jamii kwa uharaka na lugha rahisi, imekuwa ikiandaa tahariri, Habari na Makala mbalimbali kwenye vyombo vya Habari kupitia wanachama wake.


Mathalani mwaka 2018, JET ilishiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Kasa duniani yaliyofanyika jijini Tanga katika Kijiji cha Chongoleani, ambako chama hicho kilichapisha makala zaidi ya 25 kwenye magazeti, redio na vituo vya televisheni.


Aidha kwa kutambua umuhimu wa Kasa ambao wanalindwa kwa mujibu wa sheria ya Uvuvi yam waka 2003 na Kanuni za uvuvi za mwaka 2019, JET pia imeweza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuandika Habari za uhifadhi wa Kasa zaidi ya Waandishi wa Habari na Wahariri 110 nchi nzima.  


Ikumbukwe kuwa hatua ya baadhi ya wavuvi kutekeleza uvuvi haramu kwa Kasa kunatajwa kuwa na athari kubwa kwa viumbe hao hao pamoja na maisha ya binadamu kwa ujumla kutokana na umuhimu wao kwa ekolojia ya bahari. 


Katika kuhakikisha viumbe bahari hao wanalindwa, Mei 23,2025 dunia itaadhimisha siku ya Kasa, siku 

hii ni muhimu kwa kuelimisha jamii juu ya hatari zinazowakabili viumbe hai hawa wa baharini. 

Tanzania ambayo inazo aina tano kati ya saba za kasa wa baharini wanaopatikana duniani kote ni miongoni mwa mataifa yaliyoipa nafasi siku hiyo ili kuhakikisha Kasa wanalindwa.

Aina hizo tano za Kasa hupatikana katika mwambao wa Tanzania na zote zimetajwa kuwa katika hatari ya kutoweka. 


Mkurugenzi wa JET, John Chikomo

Ujumbe wa mwaka huu unasisitiza kuwalinda Kasa wa baharini kuwa ni suala la uhai kwao na kwetu.

Licha ya kuishi kwa zaidi ya miaka milioni 100, kwa sasa Kasa wanakabiliwa na vitisho vikubwa vinavyosababishwa na shughuli za binadamu. 


Uwindaji haramu na ulaji wa nyama ya kasa, hasa katika jamii za pwani za Tanzania na Zanzibar, bado unaendelea kuwa tishio licha ya kupigwa marufuku kisheria. 


Uwindaji na biashara ya Kasa na mayai yao ni kinyume cha sheria nchini Tanzania na huambatana na adhabu kali.Hata hivyo watu wengi huamini kuwa nyama na mayai ya kasa yana nguvu za tiba au kuongeza nguvu za tendo la ndoa, lakini imani hizi zinaleta madhara makubwa kwa viumbe hao

 

Aidha ulaji wa nyama ya kasa hauishii tu kuhatarisha maisha yao, bali pia unaweka maisha ya binadamu hatarini. Machi 2024, watoto wanane na mtu mzima walifariki dunia baada ya kula nyama ya kasa kisiwani Pemba, Zanzibar. 


Watu wengine 78 walilazwa hospitalini. Sababu kubwa ilikuwa ni kula sumu ya chelonitoxism, sumu hiyo inatajwa kuwa  ni hatari.Tukio kama hili lilitokea pia mwaka 2021 ambapo watu saba, akiwemo mtoto wa miaka mitatu, walifariki kwa kula nyama ya Kasa.


Pamoja na uvuvi haramu, lakini pia uharibifu wa fukwe nao ni changamoto kwani husababisha Kasa kukosa maeneo ya kutagia mayai, ujenzi wa mejengo karibu na bahari unatajwa kuwa tishio zaidi.

Uharibifu wa maeneo yao ya malisho ni changamoto nyingine. Tatizo kubwa zaidi ni uchafuzi wa mazingira kwa plastiki. Kasa hukosea plastiki na kudhani ni majongoo baharini au mwani, hali inayopelekea kuziba kwa njia ya chakula na hatimaye kifo. 


Ripoti ya “State of the World’s Sea Turtles (SWOT)” inaweka wazi kuwa Kasa wasiopungua 1,000 hufa kila mwaka kutokana na kukwama katika plastiki hii ikiwa ni sawa na kasa mmoja katika kila saa tisa.

Kasa ni muhimu kwa mifumo ya maisha ya baharini na uchumi wa pwani ya Tanzania. 


Kama spishi muhimu (keystone species), kupotea kwao kunaweza kuathiri maisha yote ya baharini. Husaidia kudumisha afya ya matumbawe na mwanimaeneo muhimu kwa samaki, kamba, jodari na kaa. 

Kwa kulisha na kuchimba mashimo ya kutagia, huandaa makazi kwa viumbe wengine. Kama wawindaji na mawindo yao, wanasaidia kusawazisha mnyororo wa chakula baharini.


Ritha Johansen, mwakilishi wa Wild Africa nchini Tanzania, amesema:
“Karibu vitisho vyote vinavyowakabili 
Kasa na makazi yao vinasababishwa na binadamu.

 Ulaji wa kasa si hatari tu kwa spishi hizi zilizo hatarini, bali pia ni tishio la moja kwa moja kwa maisha ya binadamu. Tunahitaji kubadili mitazamo na tabia kuhusu uwindaji haramu na ulaji wa kasa kwa faida ya viumbe hawa na jamii zinazowazunguka. Uwindaji unatuibia sote. Tukiwapoteza kasa, tunapoteza sehemu muhimu ya mfumo wa bahari. Kuwalinda ni kulinda mazingira ya baharini, urithi wetu wa kitamaduni, na vizazi vijavyo.”

 

Post a Comment

0 Comments