Ticker

7/recent/ticker-posts

RITA: ZAIDI YA ASILIMIA 99.75 YA VYETI VIMEHAKIKIWA

 
Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Frank Kanyusi kulia na kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Profesa Bill Kiwia wakionesha  hati ya makubaliano   wakati wa  hafla ya kubadilishana hati za makubaliano iliyojumuisha  taasisi  zinazohusika na masuala ya  utambuzi  ambazo ni  Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), CREDITINFO Tanzania Ltd, jana jijini Dar es Salaam.


Na wandishi Wetu, Dar es Salaam

KABIDHI Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Frank Kanyusi amewataka   wananchi  na  waombaji wote wa mikopo ya elimu ya juu    kutosubiri  dirisha la mikopo kufunguliwa ndio waanze  kutuma maombi ya uhakiki RITA  badala  yake  watume  maombi  mapema  kwani mfumo wa kuhakiki  wa vyeti upo wazi mwaka mzima.

 Akizungumza na waandishi wa habari mara baada  hafla  ya kubadilishana hati za makubaliano iliyojumuisha  taasisi  zinazohusika na masuala ya  utambuzi ambazo ni  Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), CREDITINFO Tanzania Ltd ambayo ni taasisi ya uchakataji wa taarifa za waombaji mikopo katika taasisi za fedha.

  “Kwa sasa, mwombaji mkopo, anatuma maombi ya uhakiki wa cheti cha kuzaliwa au cha kifo cha mzazi wake kupitia mfumo wa TEHAMA wa eRITA unaopatikana kupitia tovuti ya wakala ya www.rita.go.tz. Baada ya uhakiki kukamilika, tunampatia mwombaji NAMBA MAALUM ambayo akiingiza kwenye mfumo wa Bodi ya Mikopo – inasomeka RITA moja kwa moja,” alisema Kanyusi.

 Kanyusi alisema tangu dilisha lilipofunguliwa tarehe 1 juni 2024 wamekwisha pokea jumla ya maombi ya uhakiki 244,354 ambapo kati ya hayo, maombi 218,263 ni ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na 26,091 ya uhakiki wa vyeti vya vifo.

“Hadi kufikia leo, Wakala umeshahakiki jumla ya maombi 243,629 sawa na asilimia 99.75 ya maombi yaliyopokelewa. kati ya maombi yaliyofanyiwa uhakiki, jumla ya maombi 26,150 yalikuwa na mapungufu na waombaji walirudishiwa kwa ajili ya kufanya marekebisho na maombi 618 yalikataliwa kwani vyeti vilivyowasilishwa kwa ajili ya uhakiki havikuwa halali,” alisema Kanyusi.

 Aidha Kanyusi alisema maombi 725 bado yanaendelea kuhakikiwa na zoezi linategemewa kukamilika ndani siku 1.

 “Katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kutoa huduma  bora kwa wananchi inatimia sambamba na  kutekeleza agizo la  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan   la kutaka  mifumo ya   yote ndani ya serikali  kusomana  ifikapo Desemba mwaka huu, RITA kwa  kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB)  tumeshalitekeleza agizo hilo,” alisema Kanyusi.

 Na kuongeza kuwa wakala wamejipanga kutekeleza yote yaliyomo kwenye makubaliano na HESLB sambamba na kufanya maboresho ya mfumo wa uhakiki lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi katika utendaji.

Post a Comment

0 Comments