Ticker

7/recent/ticker-posts

JUKWAA LA WAHARIRI LALAANI MWANDISHI KUSHAMBULIWA NA WAALIMU UBUNGO

                              Mwandishi wa habari wa Kampuni ya The Guardian, Dickson Ng’hily,

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM. 

Mwenendo usiofaa wa kushambulia na kukamata Waandishi wa Habari wanaotekeleza majukumu yao, umeliibua Jukwaa laWahariri Tanzania (TEF) kulaani vitendo hivyo vinavyotekelezwa na baadhi ya watumishi wa umma wanaotumia madaraka yao vibaya.


Leo Julai 12, 2024 TEF limesikitishwa na kukilaani kitendo cha kushambuliwa kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya The Guardian, Dickson Ng’hily, kilichofanywa na baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Kwembe iliyopo Wilayani Ubungo, Dar es Salaam, wakati akitelekeza majukumu yake.

 

Shambulio hilo lilitokea Julai 10, 2024 kwa madai kuwa amewapiga picha wanafunzi wa shule hiyo waliokuwa wakisoma nje ya madarasa. 

 

Baada ya kumshambulia, walimu walikwenda mbali zaidi kwa kumpeleka mwandishi huyo katika ofisi za Serikali ya Mtaa na baadaye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo. 

Licha ya kipigo, walimu hao na baadhi ya wanafunzi waliharibu vifaa vyake vya kazi ikiwamo simu ya mkononi ambayo inadaiwa kupasuliwa kioo pamoja na kufuta picha alizopiga.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deudatus Balile, imeeleza kuwa uandishi wa habari chini ya Kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Huduma za Habari (MSA) ya Mwaka 2016 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2023, ni taalumainayotambulika kama taaluma nyingine nchini.

 

“Tumeona utetezi, kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Ubungo wakisema, “aliwekwa chini ya ulinzi kujiridhisha kama ana kibali cha kupiga picha”. Utetezi huu ni mwendelezo wa jinai sawa na walivyofanya walimu waliompiga Ng’hily.

 

“Tunajiuliza ukaguzi huo walitaka kuufanya kwa kutumia sheria ipi au walipata wapi mamlaka hayo? Nani kawaambia kuwa mwandishi wa Habari akikuta tukio linaendelea anapaswa kuandika barua ya maombi ya kibali cha kupiga picha, kiidhinishwe kwanza ndipo arudi kupiga picha? Hivi hilo tukio atalikuta likiendelea akifuata utaratibu huo? Duniani kote, mwandishi akikuta tukio anapiga picha kwanza kisha anawatafuta wahusika kupata ufafanuzi. Kwa nini Wilaya ya Ubungona Walimu wa Shule ya Msingi Kwembe wanataka kutunga kanuni mpya isiyokidhi vigezo vya uandishi wa habari?” imeehoji taarifa hiyo.

 

TEF imesisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na walimu hao ni jinai na hujuma dhidi ya juhudi anazofanya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kurejesha uhuru wa vyombo vya habari nchini kwa kuzuia waandishi kukamatwa, kupigwa, kuzuiwa kufanya kazi, kunyanyaswa na mengi ya aina hiyo ambayo ameyazuia tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 hali iliyoipandisha Tanzania katika viwango ya Uhuru wa Vyombo vya Hari Duniani kwa nafasi 46, yaani kutoka nafasi ya 143 hadi nafasi ya 97. 

 

“Vitendo vya aina hii vikiendelea nchi yetu itashuka tena na kuathiri kuaminika kwake mbele ya jamii ya kimataifa hivyokukimbiza wawekezaji.

 

“TEF tunalaani kwa nguvu zote kitendo hiki na tunavisihi vyombo vya dola vimpe ushirikiano wa kutosha Mwandishi Ng’hily, ambaye tayari ameanza mchakato wa kufungua kesi ya jinai dhidi ya wote waliohusika katika kadhia hii. TEFtutamuunga mkono hatua kwa hatua kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua   stahiki   ikiwa   ni   pamoja na kulipagharama ya hasara waliyomsababishia.

 

Post a Comment

0 Comments