Ticker

7/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AWAPA POLE WACHIMBAJI WADOGO WALIOPOTEZA WENZAO SIMIYU, MAVUNDE AWAPA HABARI NJEMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia S. Hassan ametuma salamu za pole kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu mkoani Simiyu kufuatia vifo vya zaidi ya wachimbaji 21 waliofukiwa na kifusi katika kijiji cha Ikinabushi,Wilayani Bariadi-Mkoa wa Simiyu. 

 Salamu hizo zimetolewa leo Januari 14,2024 latika Kijiji cha Ikinabushi,Wilayani Bariadi-Simiyu na Waziri wa Madini Anthony Mavunde alipozungumza na wachimbaji wadogo katika eneo hilo na kuwasilisha salamu za pole za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ndugu na jamaa wa familia zilizopoteza wapendwa wao kufuatiwa kufukiwa na kifusi wakati wakiendelea na kazi ya uchimbaji madini. 

 Waziri Mavunde amesema kwa sasa shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo zitasimama mpaka pale Wizara kupitia kitengo cha Ukaguzi Migodi na Mazingira kitakapojirdhisha juu ya usalama wa eneo hilo kiuchimbaji. 

 Kufuatia maombi ya wachimbaji hao ambao ni zaidi ya 500 ya kuomba kuendelea na uchimbaji wa eneo hilo kwa lengo la kujitafutia riziki, Rais ametoa maelekezo kwa Wizara kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ili wachimbaji hao warasimishwe na kupatiwa Leseni ya madini. 
Aidha Waziri Mavunde amewataka wachimbaji hao waunde kikundi cha pamoja ili kupatiwa leseni na kuzitaka mamlaka za mkoa na wilaya kusimamia zoezi hilo. 

 Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mhandisi Andrew Kundo ameishukuru serikali kwa kuwakimbilia kwa uharaka kutokana na janga hilo. Poa amemshukuru Rais kwa hatua ya upatikanaji wa leseni kwa kuwa wananchi hao shughuli yao kubwa ya kiuchumi ni uchimbaji na ndio maisha yao. 

 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda ametoa pongezi kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga kwa kusimamia vyema zoezi la kutoa miili na kuimarisha usalama katika eneo hilo na ameahidi kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinasimama mpaka taratibu za kiusalama zitakapo kamilika.

Post a Comment

0 Comments