Ticker

7/recent/ticker-posts

DKT. MPANGO AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUTOA HUDUMA KWA HAKI NA USAWA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewataka Watumishi wa Umma na Viongozi wa Umma kutimiza wajibu wao ipasavyo wa kuwahudumia Wananchi kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kutenda haki wakati wote wanapotoa huduma ambapo amewasihi kufanya kazi kwa hofu ya Mungu na kuachana na tabia za kuwapa kesi Wananchi wasiohusika na kesi hizo. 

 Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiongea na Waumini mara baada ya kushiriki Ibada ya Mwaka Mpya katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma, ambapo amesema ni vema Viongozi wa Umma wanapotunga sera na sheria kuhakikisha zinakuwa na manufaa kwa Wananchi wengi. 

 Amesema ni muhimu Watanzania kuendelea kukemea na kupinga utengano, udini ukabila pamoja na siasa za chuki na pia amewasihi watanzania kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ili kuinua maisha ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla na pia amewaasa Watanzania kulipa kodi halali ili taifa liweze kupata maendeleo ya haraka. 

 Dkt. Mpango ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, vilevile amewasihi wazazi na walezi kuhakikisha Watoto wote wenye umri wa kuanza Shule kwa mwaka huu 2024 wanaanza masomo yao na wakati wote kufuatilia maendeleo ya Watoto hao Shuleni.

Post a Comment

0 Comments