Ticker

7/recent/ticker-posts

​WANAOHAMA KWA HIYARI NGORONGORO WAPEWA FURSA YA KUJICHAGULIA MAKAZI

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetoa fursa kwa wafugaji wanaotaka kuhama kwa hiyari kutoka kwenye hifadhi hiyo kujichagulia eneo la kwenda kuishi kati ya maeneo maalum yaliyoandaliwa kwa ajili yao.

Tayari NCAA imeandaa mazingira mazuri ya watu hao kwenye vijiji vya Msomera na Saunyi vilivyopo mkoani Tanga na kile cha Kitwai kilichopo mkoani Manyara.

Kwa sasa NCAA inaendelea na ujenzi wa nyumba 5,000 ambazo zinajengwa kwenye maeneo hayo na zitakuwa na uwezo wa kupokea kaya 10,000.


Nyumba hizo 5000 ni awamu ya pili muendelezo wa ujenzi wa nyumba zitakazotumiwa na wafugaji hao kutoka Ngorongoro na zinajengwa na vikosi vya SUMA -JKT.

Kati ya nyumba 5,000, nyumba 250 zinajengwa eneo la Msomera, nyumba 1,500 zinajengwa Kitwai na nyumba 1000 zinajengwa Saunyi.

Akizungumzia hatua hiyo Meneja Uhusiano kwa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya alisema katika awamu ya pili ya kuhamisha wafugaji kwa hiyari, mamlaka imetoa nafasi kwa kaya 4000, kuchagua maeneo mengine wanayotaka kuhamia kwa hiyari.


Ikumbukwe kuwa katika awamu ya kwanza zilijengwa nyumba 503 katika kata ya msomera wilayani handeni mkoani tanga na kuwekwa miundombinu mbalimbali ya kijamii.

“Katika awamu ya kwanza tulifanikiwa kuhamisha kaya 551 zenye idadi ya watu 3,010 waliohama kwa hiyari pamoja na mifugo 15,321, katika awamu ya pili kaya 4000 pia zimechagua maeneo mengine wanayotaka kuhamia kwa hiyari.”

Amesema kaya zinazohama kwa hiyari zinapewa fidia ya shilingi milioni 10 zikiwa ni mahsusi kwa ajili ya maendeleo ya makazi mapya na motisha kwa kila kaya ili ziweze kuwa na pesa ya kujikimu.


Awamu ya kwanza ya kaya zilizohamia Msomera, kila kaya imepewa nyumba yenye vyumba vitatu kwenye eneo lenye hekari 2.5 na shamba la hekari tano kwa ajili ya kugfanya shughuli za ufugaji. 

 “Wanaohama kwa hiyari tunawasafirisha na mizigo yao bure, tunatoa chakula gunia mbili kila baada ya miezi mitatu kwa muda wa miezi 18, lengo ni kuhakikisha wanaweza kujitegemea katika kipindi hicho na tunahakikisha kila eneo linakuwa na huduma zote za kijamiii.”

Katika kulifanikisha hilo, Dambaya alitoa wito kwa Wahariri na waandishi wa Habari kwa ujumla kuendelea kuunga mkono mpango huo wa serikali wenye lengo la kuliokoa eneo hilo la Ngorongoro.


Alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kutoka watu 8000 waliokuwepo mwaka 1956 hadi sasa kufikia watu 125,000 na ongezeko la mifugo likiwa ni kutoka 261,723 mwaka 1956 hadi sasa kufikia mifugo 890,459.

Dambaya alisema lengo la kuwahamisha watu hao ni kuendelea kuimarisha uhifadhi na kuwaletea maendeleo wananchi tofauti na wanavyoishi sasa ndani ya hifadhi.

Post a Comment

0 Comments