Ticker

7/recent/ticker-posts

KINANA: RAIS SAMIA NI MSIKIVU, ANA NAFASI KUBWA YA KUENDELEA KUONGOZA NCHI UCHAGUZI UJAO

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahaman Kinana, amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili ya uongozi wake yanatokana na utulivu, usikivu, kupokea ushauri na kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya Watanzania.

Kinana ameyasema hayo jana Julai 23, 2023 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kondoa  mkoani Dodoma katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dk. Ashatu Kijaji kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2023.

“Kwa hali ilivyo na kwa hatua tuliyopiga tukienda hivi tunavyokwenda mpaka kufika 2025 nina uhakika kila Mtanzania atakuwa na sababu ya kusema tuendelee na CCM, tuendelee na Rais Samia Suluhu Hassan. Hatutokuwa na sababu nyingine yoyote kwanza ni utamaduni wetu CCM hatubadilishi uongozi katikati ya safari, ukitaka kubadilisha sababu itakuwa nini, hakuna.


“Hatusemi haya kwa kujivuna bali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM lakini tunaangalia na wenzetu wa nchi jirani wanakwendaje. Nchi yetu imetulia, ina maani, ina umoja, inamshikamano, nchi ina malengo, na ina mipango ambayo inatekelezwa na kila mtu ni shahidi, CCM itaendelea kuchaguliwa kwa sababu ina sera nzuri ina ilani nzuri inayotekelezeka,” alisema Kinana.

Aidha, amesema kutokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Taifa,  watu waliojaribu kuigawa nchi kwa misingi ya udini wameshindwa.

"Kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ukabila wameshindwa, kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ubara na visiwani wameshindwa," amesema.

Post a Comment

0 Comments