Washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga imealikwa Ikulu kesho kula chakula cha jioni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Chakula hicho kitaliwa kwenye Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo wa Rais umelenga kuipongeza Yanga kwa kufanya vizuri katika michezo yake ya kugombea Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyohitishwa jana Jijini Algers, Algeria.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia amewapongeza Yanga kwa kucheza vizuri katika mchezo wa pili wa fainali hapo jana kwa kuwafunga wenyeji bao 1-0 na hivyo kuwa na matokeo ya jumla ya mabao 2-2 japokuwa hawakufanikiwa kutwaa ubingwa huo kutokana na kuruhusu kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Tarehe 28 Mei, 2023.
Msigwa amebainisha kuwa pamoja na kutotwaa ubingwa, Rais Samia anatambua kuwa Yanga wameipa heshima kubwa Tanzania na anawapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo ambao ni Mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Timu ya Yanga, viongozi na mashabiki wanatarajiwa kurejea hapa nchini usiku wa leo kwa ndege iliyotolewa na Rais Samia ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono timu hiyo iliyotinga fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza.
0 Comments