Ticker

7/recent/ticker-posts

SERIKALI KUSHUGHULIKA KIKAMILIFU NA WEZI WA DAWA

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameweka wazi kuwa, Serikali imepanga kuchukua hatua kali kwa wote watakaobainika kushiriki kwenye wizi wa dawa.

Amesema watafanya hivyo ili iwe funzo kwa wengine wenye nia ovu ambayo inawanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 23, 2023 wakati akijibu swali la Luhaga Mpina wakati wa Mkutano wa 11, kikao cha 31 cha Bunge kinachoendelea Jijini Dodoma. 

 Serikali kupitia Wizara ya Afya iliona dalili za upotevu wa dawa zenye thamani ya Bilioni 83 hivyo kushirikiana na TAKUKURU ili kuhakikisha wote watakaobainika kuwepo katika upotevu huo wa dawa wanachukuliwa hatua kali.

Amesema, Serikali imefanya mikakati mbalimbali katika kutatua tatizo la wizi na ubadhirifu wa dawa na vifaa tiba ikiwemo kufanya suala la upotevu wa dawa na vifaa tiba kama agenda katika vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya.

Aidha Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bidhaa za Afya ikiwemo kufunga mifumo ya kielectroniki pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa bidhaa hizo.

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Wizara kwa kushirikiana na OR TAMISEMI imeendelea kuimarisha kamati za usimamizi za vituo kwa kuzijengea uwezo kuhusu majukumu yao katika usimamizi wa bidhaa za Afya.

Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema, Wizara imeendelea kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wabunge kushiriki katika upokeaji wa bidhaa hizo na taarifa zote wapewe ili kujenga uwazi zaidi juu ya bidhaa hizo za afya.

Aidha, Dkt. Mollel amesema suala la kupambana dhidi wizi na ubadhilifu wa bidhaa za Afya siyo la Serikali pekee bali ni suala la kushirikiana pande zote, hasa wawakilishi wa wananchi.



Post a Comment

0 Comments