Baadhi ya Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini wakipatiwa maelezo kwenye kiwanda cha kuchakata nyama cha Nguru Hill, mkoani Morogoro.
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) unashiriki kwa vitendo kwenye zoezi la kutengeneza ajira, ambapo umewekeza kwa ubia katika viwanda vinne ambavyo vinatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 3,000 nchini.
Viwanda hivyo vya kuchakata tangawizi cha Mamba Myamba kilichopo Same mkoani Kilimanjaro, Kiwanda cha chai Mponde kilichopo Tanga, kiwanda cha kuchakata nyama cha Nguru Hills kilichopo Mvomero mkoani Morogoro na Kiwanda cha bidhaa za ngozi kilichopo pia mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 31 Machi 2023 mjini Morogoro na Meneja wa Mipango na Uwekezaji (PSSSF), Herman Gudluck wakati akiwasilisha mada kuhusu masuala ya uwekezaji kwa wa wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wanaoshiriki mkutano wa mwaka wa 12 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Amesema viwanda vyote vitakapokamilika vitagharimu kiasi cha Sh bilioni 164 sawa na asilimia mbili ya mapato ya mfuko huo.
Aidha, amesema uwekezaji huo ambao wameufanya kwa ubia bila kuingiliani na sera za zinazoongoza mfuko huo.
Gudluck ametoa mfano kuwa katika kiwanda cha tangawizi, wameingia ubia na wakulima wa eneo hilo na kununua mashine mpya kwa uwekezaji wa Sh bilioni nane na sasa kiwanda kimekamilika na kuanza kufanya kazi.
Amesema kiwanda cha chai Mponde ambacho wameingia ubia na mfuko wa WCF, kipo katika hatua za mwisho kukamilika vivyo hivyo kwa upande wa kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro nacho kinatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.
Aidha, kuhusu kiwanda cha kuchakata nyama cha Nguru Hills kilichopo Mvomero mkoani Morogoro amesema PSSSF iliweka kiasi cha Sh bilioni 8.3 na sasa tayari kimeashaanza kazi ya kuchinja na kuchakata nyama kisasa ambayo inasafirishwa ndani na nje ya nchi.
Katika kiwanda hicho ambacho wahariri pia wametembelea na kujionea shughuli zinazofanyika kiwandani hapo, ambapo Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, James Mlowe amebainisha kuwa kiwanda kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 1,500 kwa siku, soko kwa wafugaji litaongezeka.
Amesema uwekezaji huo wa PSSSF unalenga kutengeneza masoko ya bidhaa zinazozalishwa na wakulima nchini na kuchochea uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Mradi mradi wa kiwanda hicho cha kuchakata nyama, una miundombinu inayohitajika kama vile eneo la malisho hekta 2,328 lenye uwezo wa kulisha ng’ombe 10,000 na mbuzi 15,000 kwa wakati mmoja.
0 Comments