NA EMMANUEL KIHAULE
Nimepita mitaa ya Kariakoo hivi karibuni, kinachoendelea kule kinatisha!
Msongamano wa kutisha wa watu na magari ni kero kubwa mno na tishio kubwa la afya ya umma! Biashara zimepangwa kiholela mpaka barabarani! Kuna maeneo mengi hadi alama za usalama barabarani na hata zile za majina ya mitaa zimefunikwa na bidhaa au vibanda vya wafanyabiashara ndogo ndogo!
Karibu kila mfanyabiashara anaita wateja kwa sauti wengine hata wakilazimisha wengine kwa kuwavuta mikono hususan mabinti na kina mama! Wengine wana vipaza sauti vilivyorekodiwa vikipiga kelele kuita wateja! Wengine hususan wanaouza bidhaa za umeme wamefungulia mziki mpaka mwisho! Yaani huwezi amini unachokiona!
Ajabu hata pale Machinga complex wafanyabiashara wengi wameshuka chini na kujenga vibanda vidogo vilivyoziba maeneo yote yanayolizunguka jengo hili! Waliobaki juu ni wale wa vifaa vya umeme na kompyuta tu! Wengine wote wameshuka chini!
Nikajiuliza kama mimi niliyepita tu tena muda mwingi nikautumia kwenye gari hadi kichwa kinauma je vipi kuhusu wafanyabiashara wale wanaoshinda pale kila siku? Vipi kuhusu wateja wao? Vipi kuhusu watu wanaolazimika kupita pale kila siku - madereva na watembea kwa miguu?
Nilijiuliza maswali mengi sana - hivi tunajua kwamba Kariakoo ni kiini kikubwa cha biashara kwa nchi nzima na pia nchi nyingi za Afrika mashariki na kati? Pia hata kusini? Watu wanatoka mpaka hata Botswana achilia mbali Zambia, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Malawi, Congo DRC na hata Sudan Kusini kuja kununua bidhaa hapa? Je kweli hayo ndio mazingira tunataka wayaone na kufanyia ununuzi wao? Je ni kweli hatuwezi kufanya lolote kuboresha hali hii?
Kwa sasa dunia inazungumzia ajenda ya miji endelevu. Je tukiacha jiji letu liendelee hivi miaka 10 ijayo hali itakuwaje? Si tutakuwa tumefikia kiwango cha maafa kabisa? Hivi magonjwa kama kifua kikuu, homa ya uti wa mgongo, na mengine mengi yanayoambukizwa kwa hewa yataisha lini nchini? Na ukitokea mlipuko tutaudhibiti vipi kwa hali ile?
Mimi nina wazo
Kwa nini tusifanye uamuzi wa makusudi kubadilisha maeneo ya Kinondoni, Sinza, Kijitonyama, Manzese, Ubungo na hata Magomeni kuwa sehemu kuu za biashara. Utengenezwe mkakati wa kujenga maduka makubwa na masoko ya wazi pamoja na hoteli na sehemu kubwa za burudani na starehe na kufanya Dar es Salaam iwe kama Dubai ya ukanda huu wa Afrika.
Itawezekanaje?
Kila mmiliki wa ardhi ahakikiwe ukubwa wa ardhi yake kisha utafsiriwe kwenye thamani ya hisa na baadae waunde ushirika/umoja uliosajiliwa kabisa kisheria. Kwenye kilimo hii inafanana na block farming/ukulima wa mashamba makubwa ya umoja.
Wale wamiliki wote watakuwa wanalipwa kulingana na faida zinazotokana na pango kwa uwiano wa hisa zao huku wakiendelea kulipa deni kidogo kidogo. Hisa hizi watazimiliki wao na warithi wao maisha yao yote. Pia wataruhusiwa huko baadae kuzitumia kuombea mikopo benki au hata kuziuza au kuingia ubia na watu wengine wakitaka huko mbele.
Serikali na wadau wawezeshe kuandaa mpango huo ambao utatumika kuvutia taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi. Kisha wapate mkopo na kuanza kujenga na kubadilisha maeneo hatua kwa hatua.
Mpangilio
Tutengeneze kanda mbali mbali/zoning kama vile maeneo ya bidhaa za magari/vipuri na mitambo, nguo/vipodozi/viatu, bidhaa za kilimo na ufugaji, vifaa vya ujenzi na kadhalika. Mji uwe umepangilika vyema na mitaa mipana na misafi yenye huduma za kijamii kama vile bustani za kupumzikia, vyoo (kwa sasa hivi Kariakoo ukibanwa na mkojo unaweza kujikojolea!), na hata mabafu ya umma.
Namna hii tutaifanya Kariakoo na mitaa yake yote ipumue lakini muda huo huo tunakuwa tumepanua wigo wa eneo la biashara hivyo kutoa fursa za ajira na kujiingizia kipato kwa watu wengi zaidi. Achilia mbali vyanzo vya mapato kwa serikali.
Biashara na utalii
Pawepo hoteli na migahawa ya kutosha pamoja na kumbi za burudani na starehe. Mbali ya wafanyabiashara, kuna watu wengi wanaotaka kuja kuitembelea Tanzania zikiwemo fukwe zake safi na nzuri kama kule Bagamoyo, Dar es Salaam, Kilwa, Mafia na hata Zanzibar na hii itakuwa kivutio kikubwa kwani hata baada ya matembezi, pia watafanya shopping kabla ya kurejea kwao.
Miaka ya karibuni nimekuwa nikishuhudia watu zikiwemo familia kutoka nchi zinazotuzunguka wakija Tanzania kwa barabara hususan Dar es Salaam na kisha kuvuka kwa boti hadi Zanzibar kwa mapumziko ya mwisho wa wiki au hata nyakati za siku kuu. Hii ni fursa ambayo tunaweza kuiendeleza vyema.
Tayari maeneo ya Sinza, Mwenge, Makumbusho, Kinondoni n.k. wameshajiongeza na kujenga maduka mengi ya biashara. Sasa wasaidiwe kutoka kwenye kujenga fremu na viosks hadi maduka makubwa yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa. Tusiishie kwenye uchuuzi tu!
Je kweli hatuwezi?
Sasa je hii ni sayansi ya nyuklia ambayo ipo juu ya upeo wetu wa kifikra? Sidhani! Sio mpango rahisi wala wa muda mfupi lakini naamini tukiamua na kujipanga vyema tunaweza! Tuanze hata kwa hatua moja moja...
0 Comments