Ticker

7/recent/ticker-posts

MABILIONI ‘YAMWAGWA’ KWENYE MIFUGO

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega 

ILI kuboresha huduma za mifugo na kuiepusha dhidi ya magonjwa, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 257 katika halmashauri 80, ambapo majosho 88 tayari yamekamilika.

Akiwa katika Kijiji cha Narakauo, wilayani Simanjiro mkoani Simanjiro, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi ya ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya mifugo, alisema majosho 169  yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Akiwahutubia wakazi wa Kijiji hicho ambao wengi ni wafugaji Ulega amesema dhamira ya serikali ni kuiondolea mifugo magonjwa.

 Alisema katika mwaka wa fedha wa 2022/23, vifo vya mifugo vinavyotokana na maradhi ya kupe na ndorobo vimepungua kutoka asilimia 72 hadi 56.

Ameongeza kuwa tayari majosho matano yamejengwa katika Wilaya ya Simanjiro mwaka huu wa fedha, majosho mawili mwaka uliopita na majosho saba yatajengwa mwaka ujao wa fedha.
Aidha, amesema licha ya ujenzi wa majosho serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na imetoa dawa ya ruzuku kwa ajili ya kuweka kwenye majosho lita 52,560 kote nchini yenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3, huku takriban lita 400 zikipelekwa katika Wilaya ya Simanjiro kwa ajili kuzitawanya katika majosho mbalimbali.

Kuhusu ombi la wananchi la mitego ya kukamatia mbung’o ambao wamekuwa wakisumbua kwenye maeneo yao, Naibu Waziri Ulega amesema serikali imechukua ombi lao na litafanyiwa kazi.

 

Kundi la Ng'ombe
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Loibosiret, Ezekiel Lesanga amepongeza juhudi za serikali na kuomba kuongezewa majosho mengine mawili ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi wa Kata ya Loibosiret ambao mifugo yao iko katika maeneo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga ametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa wanapata maji kupitia bwawa lililojengwa na serikali katika Kijiji cha Narakauo kwa gharama ya Shilingi Milioni 413 na kukabidhiwa Mei Mwaka 2022, kwa ajili ya kunyweshea mifugo na matumizi mengine ya kibinadamu.
Ulega pia amefanya zira kwenye mradi wa ujenzi wa bwawa la Lelarumo lililopo Wilaya ya Simanjiro, ambalo litajengwa  na serikali kwa fedha za bajeti ya 2022/23 kwa gharama ya Shilingi Milioni 364.

Post a Comment

0 Comments